Mwakyembe: Tutaimarisha viwanja vya ndege kimataifa

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema Serikali imejizatiti katika kukarabati viwanja vya ndege ili kuyavutia mashirika ya kimataifa ya ndege kuleta huduma zao nchini na hivyo kukuza sekta ya utalii.

Alisema bila kuimarisha viwanja vya ndege, mashirika mengi yatashindwa kutoa huduma hiyo katika miji mbalimbali nchini na hivyo kushindwa kuongeza idadi ya watalii.

Dk Mwakyembe alisema hayo jijini Arusha akiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki wakati wa uzinduzi wa safari za shirika la ndege la Qatar Airways ambalo ndege zake zimeanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).

“Tunaomba mashirika mengine ya kimataifa yaanze kufika kwenye miji yetu kama Arusha ambako ndiko kitovu cha utalii, tunawahakikishia kuwa tutaendelea kuimarisha miundombinu yetu kwa ajili ya usalama wa ndege zao,” alisema Dk Mwakyembe.

Naye Balozi Kagasheki alisema itakuwa ni aibu kwa watalii wa kigeni wanaokuja nchini kutua katika uwanja wa ndege wa Nairobi nchini Kenya wakati hapa nchini kuna viwanja vyenye sifa ya kutua ndege kubwa.

“Wakati tunatangaza utalii wa nchi yetu tunayahamasisha mashirika ya kimataifa ya ndege kuleta ndege zao nchini,” alisema Kagasheki.

Alisema kukiwa na usafiri wa uhakika ni rahisi kuongeza idadi ya watalii ambao wanatembelea kujionea vivutio vya utalii nchini.

Alisema nguvu kubwa itatumika kuhakikisha kwamba kunakuwa na usafiri wa uhakika wa ndege hasa kwenye viwanja vya Kilimanjaro na Arusha.

“Arusha na Kilimanjaro ndiyo kitovu cha utalii kwa sababu ya mbuga za wanyama na mlima Kilimanjaro, hivyo juhudi za makusudi zinatakiwa kufanywa ili kutumia fursa hiyo ili kuongeza pato la taifa,” alisema Kagasheki.
Naye Mtendaji Mwandamizi wa Qatar Airways, Marwan Koleilat alisema uamuzi wa kuleta safari katika uwanja huo unatokana na sekta ya utalii kukua kwa kasi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Alisema Tanzania itafaidika kwa kuongeza idadi ya wageni wa kitalii ambao kutoka katika nchi mbalimbali duniani.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.