NDUGAI AWAGAWA WABUNGE WA CCM

Hatua ya Naibu Spika, Job Ndugai, kukataa ombi la Mnadhimu Mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu, kuwasilisha hoja ya kutaka ajali ya MV Skagit, imekosolewa na kuwagawa wabunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ndugai akiongoza kikao cha Bunge juzi Ijumaa, alimzuia Lissu kuwasilisha hoja ya kutaka kusitishwa hoja ya hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Chakula, Kilimo na ushirika, ili kufanyike mjadala kuhusu ajali hiyo.

Naibu Spika huyo, alisema ingawa hoja ya Lissu ilikuwa nzito, lakini haikutolewa kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
Hata hivyo, Lissu alitoa taarifa akitetea kwamba alifuata utaratibu kwa mujibu wa ibara ya kanuni ya 47 (3), ili apewe idhini na kiti cha Spika, ndipo atoe hoja.

Lakini Ndugai alisimamia katika uelewa na tafsiri yake kuwa Lissu alipaswa kuzungumza baada ya kusimama kama ishara ya kutoa hoja, ili iungwe mkono na wabunge wengine, lakini haikuwa hivyo.
Baadhi ya wabunge kupitia CCM wameliambia NIPASHE Jumapili kuwa, hatua ya Ndugai kuzuia hoja ya Lissu kwa kile kinachofananishwa ‘ubabe wa kisiasa’, inakitia doa Chama Cha Mapinduzi.

Hata hivyo, wabunge wengi hawataki kutajwa majina yao kwa kile wanachosema kuepuka kuandamwa, kama ilivyotokea kwa Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe.

Filikunjombe aliyeunga mkono hoja ya ajali ya MV Skagit kujadiliwa bungeni, alifuatwa na baadhi ya mawaziri na kuulizwa kwa nini alifikia hatua hiyo huku akijua hoja iliyotolewa ilitoka kwa wapinzani.

Mbunge huyo kijana mwenye misimamo ya kuunga hoja zenye maslahi ya umma pasipo kuathiriwa na itikadi za vyama, alisema ajali ya MV Skagit iliwaathiri Watanzania bila kujali tofauti za itikadi zao.

Mbunge wa Nzega (CCM), Hamis Kingwangalla, aliiambia NIPASHE Jumapili kuwa ingawa Ndugai alitumia mamlaka ya Unaibu Spika, lakini alipaswa kutumia busara zaidi kuhusu hoja ya Lissu.

“Hawa jamaa (upinzani) hawakutaka kuahirishwa kikao ama mkutano wa bunge, bali kujadili hoja ya ajali ya MV Skagit, kwa mtazamo wangu nadhani angekubali hata kwa nusu saa, isingetuathiri,” alisema.

Mbunge mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema kukataa kuijadili hoja iliyohusu maisha ya watu, iliifanya CCM ionekane haipo kwa ajili ya wananchi wanyonge.

“Waliokufa si wageni wale, ni raia wa Tanzania sasa kuikataa hoja ile, tena kwa lugha ya mabavu ikichochewa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, haitoi taswira nzuri ya chama mbele ya umma,” alisema.

Hata hivyo, Mbunge mmoja kutoka jimbo moja la mkoani Kagera ambaye hakutaka pia jina lake litajwe gazetini, alisema hapakuwa na haja ya kuijadili ajali hiyo kwa vile mamlaka nyingine zilikuwa zinaendelea kuifanyia kazi.

“Binafsi sijaona tatizo la Ndugai kuikataa hoja ya Lissu hata kama ingefuata kanuni, kwa maana tayari kuna mamlaka nyingine zinalifanyia kazi, hatuwezi kuwa taifa ambalo yakitokea majanga nchi nzima inaelekea huko,” alisema.

Mbunge huyo alisema, ndio maana licha ya kutokea ajali hiyo, taasisi nyingine kama mashule, majeshi, wizara za serikali na nyinginezo hazikufungwa, bali zilishiriki uzalishaji na utoaji huduma.
Kusitishwa kwa Lissu kutoa hoja hiyo, kulisababisha baadhi ya wabunge wa upinzani kutoka nje, kwa madai kuwa Bunge ‘linaburuzwa’ na serikali katika kuwajibika kwa umma.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.