Serikali, walimu vitani

SERIKALI na Chama cha Walimu Nchini (CWT) wameendelea kuvutana juu ya mgomo wa walimu unaotarajiwa kuuanza rasmi kesho kutwa nchi nzima.

Wakati Wizara ya Elimu na Mafunzo ikishindwa kutoa majibu ya kuridhisha juu ya hatma ya madai ya walimu hususan ongezeko la mishahara na malimbikizo ya stahiki zao, CWT imeipa serikali saa 48 ili kuipa nafasi ya kutimiza madai hayo vinginevyo wataanza mgomo.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CWT Ezekiel Oluoch alisema kuwa asilimia 95 ya walimu nchini wameunga mkono mgomo huo.

“Mgomo huo utawahusisha walimu wote walioko wilayani na mikoani, tunatarajia kuuanza rasmi Julai 30 asubuhi, kwa pamoja tutashikamana imara hadi serikali itekeleze madai yetu,” alisema Oluoch.

Naye Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo, Philipo Mulugo, aliwataka walimu hao kusitisha mgomo huo na badala yake wakutane na wizara kwa ajili ya majadilino na kuyatafutia ufumbuzi.

“Endapo dhamira yao itakuwa pale pale, watafakari madhara ya mgomo kwa sababu kuna taratibu zake na watakuwa wamekiuka, ukichukulia kwamba watakuwa hawajawatendea haki wanafunzi hivyo kwa pamoja washirikiane kufikisha hoja zao wizarani.

Hata hivyo alikwepa kuzungumzia suala la ongezeko la mshahara kwa walimu akidai kuwa si hao wanaokabiliana nalo tu, bali hata wafanyakazi wa sekta nyingine kama kilimo, afya, na wanakabiliwa na changamoto hiyo.

Vile vile alilitaka baraza lililotumika kuandaa mgomo huo litumie busara ya kukutana na serikali kwa maana hawatatenda haki kuingia katika mgomo wakati serikali haijashirikishwa.

“Hatuwezi kutoa tamko la moja kwa moja kuhusiana na ongezeko la mshahara la walimu ila ushauri wangu walimu waingie darasani kufundisha na kuipa serikali nafasi ya kutatua tatizo hilo,” alisema Mulugo.

Wakati walimu wakijiandaa kuanza mgomo Jumatatu ijayo, Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete imetoa taarifa kupinga mgomo huo kwa madai kuwa ni batili kwani kuna kesi mahakamani.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Peniel Lyimo, mgomo huu siyo halali kwa sababu shauri hili bado liko mahakamani.

“Kwa sasa, shauri hili liko Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na leo hii siku ya Ijumaa Julia 27, 2012 majira ya saa sita mchana pande zote mbili zilifika mahakamani na mahakama ikaamuru kwamba pande zote zikamilishe maelezo yao ifikapo siku ya Jumanne Julia 31, 2012 saa sita mchana ili kuiwezesha mahakama kuendelea kusikiliza shauri hilo na hatimaye kutoa uamuzi. Kwa hiyo mgomo huo sio halali kwa vile shauri hilo bado liko mahakamani,” alisema Lyimo.

Lyimo alisema kwa msingi huo, hatua ya CWT kutoa notisi ya kuanza kwa mgomo kabla ya kukamilika kwa shauri hili ni kukiuka taratibu halali za kimahakama ambazo kila mmoja anawajibika kuziheshimu.

“Serikali inapenda kuwafahamisha walimu wote kuwa kujihusisha na mgomo huu ni kwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za kazi. Hivyo, walimu wanapaswa kupima madhara ya mgomo huu usiokuwa halali na serikali inawataka walimu kupuuza mgomo huo na kutokujihusisha nao. Walimu wote wanatakiwa waendelee na kazi kama kawaida,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Lyimo, serikali imepokea notisi ya saa arobaini na nane (48) ya kusudio la walimu kuanza kugoma Julai 30 mwaka huu, lakini kabla ya notisi hiyo, serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kujadiliana na viongozi wa CWT kuhusu jinsi ya kuboresha maslahi ya walimu kwa nia ya kumaliza suala hili kwa maelewano.

Juzi chama hicho kilitangaza mgomo rasmi huku kikikamilisha taratibu za mgomo kwa kupiga kura kuunga au kukataa mgomo huo ambapo asilimia 95 ya walimu walipiga kura kuunga mkono.
Hatua hiyo imekuja baada ya serikali na CWT kushindwa kufikia makubaliano katika siku 30 walizoipa kuanzia Juni 25 mwaka huu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.