Sheria za usafiri majini sasa ziangaliwe upya

UOKOAJI wa watu na miili ya waliopoteza maisha katika ajali ya meli ya Mv Skagit unaelekea ukingoni, huku tukio hilo likizidi kugonga vichwa vya Watanzania.

Hadi sasa hakuna jibu la moja kwa moja kubainisha sababu ya ajali hiyo. Serikali imeahidi kuunda tume kuichunguza, ingawa hata tume za namna hiyo zilizoundwa awali kutokana na ajali kama hii, hazijatoa majibu sahihi kwa wananchi.

Katika ajali hiyo miili ya watu 70 hadi juzi ilikuwa imeopolewa, 140 waliokolewa wakiwa hai wengine zaidi ya 100 hawajulikani walipo. Hata hivyo, idadi kamili ya abiria waliokuwa kwenye meli hiyo mpaka sasa ni kitendawili kutokana na uzembe na mfumo mbovu wa kutambua idadi ya abiria wanaosafiri katika vyombo kadhaa.

Suala la utata katika idadi ya abiria wa meli, boti au treni limeendelea kuwa tatizo sawa na donda ndugu ambalo kwa miaka mingi halifanyiwi kazi.

Hata kwenye meli iliyozama katika Bahari ya Hindi mwishoni mwa mwaka jana na ile ya MV Bukoba iliyozama katika Ziwa Victoria Mei 21, 1996 tatizo hilo lilijitokeza na halikufanyiwa kazi.

Mfano, katika ajali ya Mv Bukoba iliyokuwa na uwezo wa kubeba abiria 400, hadi leo haijulikani ilizama na abiria wangapi. Baadhi wanataja zaidi ya 600, wengine zaidi ya 800, lakini idadi ya vifo vilivyosajiliwa katika Ofisi ya Vizazi na Vifo Wilaya ya Mwanza wakati huo ni 1,024.

Leo tumelazimika kuzihoji mamlaka zinazohusika, Sumatra na ZMA kwamba, kwa nini zimeshindwa kuweka utaratibu wa kufahamu idadi ya abiria wanaokuwamo kwenye vyombo vya usafiri na hasa vinavyosimamiwa kwa sheria za ndani na za kimataifa?

Ingawa hadi sasa hakuna taarifa rasmi kuhusu tatizo la meli ya Skagit, inafahamika kuwa imesajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) na kupewa cheti cha ubora, kuanzia Agosti 24, 2011 kinachomalizika Agosti 24, 2012.

Pia tunatambua kuwa, ingawa Sumatra inajivua suala la usajili, meli hiyo inatakiwa kukaguliwa kila inaporuhusiwa kuelea katika maji ya Tanzania Bara, kama utaratibu ulivyo kwa meli zote za Tanzania au zilizopata cheti cha usajili wa meli za kimataifa.

Kwa jumla, ajali hii ina mambo mengi ya kujiuliza, mojawapo likiwa sababu za sheria ya ZMA, kuruhusu usajili wa meli bila ukomo wa umri wake (open registry). Hivi sheria hiyo ilitungwa kwa masilahi ya nani? Je, hawakuona kama ni sheria ya kuifanya nchi yetu kuwa dampo la vyuma chakavu?

Je, waliotunga sheria hii hawakuona umuhimu wa kuweka ukomo wa umri kama ilivyo kwa Sumatra ambayo hairuhusiwi kusajili meli yenye umri zaidi ya miaka 20? Maswali yote yanabainisha umuhimu wa kupitia upya sheria za vyombo hivi na usimamizi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI