ACHARANGWA MAPANGA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA, MWINGINE AUAWA KWA KUPIGWA NONDO.
Na Ezekiel
Kamanga,Mbeya
Ajuza mwenye umri wa miaka 80
aliyefahamika kwa jina la Bi. Janeth Nenje, amenusurika kifo baada ya
kucharangwa na mapanga na mtu aliyefahamika kwa jina la Pato Lwiza Mkazi wa
Kitongoji cha Chang'ombe,Kijiji cha Mbuyuni Wilaya ya Chunya Mkoani
Mbeya.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea
kijijini hapo Septemba 19 mwaka huu majira ya saa mbili usiku ambapo mtuhumiwa
alimfuata ajuza huyo nyumbani kwake na kuanza kumcharanga kwa mapanga na kisha
kumjeruhi vibaya hali iliyopelekea kukimbizwa katika Kituo cha Afya kilichopo
kijijini hapo.
Imedaiwa kuwa siku za hivi karibuni
mtuhumiwa Bwana Lwiza alimtuhumu ajuza huyo kuwa ni mshirikina hali iliyomfanya
kuingiwa na hasira na kumtendea ukatili huo sehemu mbalimbali za mwili
wake.
Aidha Bi. Nenje hivi sasa amelazwa
katika kituo hicho cha afya cha Mbuyuni na hali inaendelea
vema.
Baada ya msako mkali wananchi
walifanikiwa kumkamata Bwana Lwiza na kuanza kumsulubu kabla ya kuokolewa na
Afisa Mtendaji wa Kijiji Bwana Mwashiuya kwa kushirikiana na Mgambo wa Kijij
hicho kabla ya kukabidhiwa mikononi mwa polisi wa Kituo cha
Mkwajuni.
Katika tukio jingine Mwananchi mmoja
Mkazi wa Kijiji cha Lulasi,Kata ya Mpombo Wilaya ya Rungwe Mkoani hapa ameuawa
na mtu au watu wasiuofahamika kisha kutumbukizwa katika Kisima cha Maji safi
kinachomilikiwa na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.
Tukio hilo limegunduliwa na wananchi wa
kijiji hicho waliokuwa wakiteka maji katika kisima hicho na kubaini harufu kali
katika maji hayo yanayotumika katika matumizi ya nyumbani kama vile
kunywa,kupikia na kufulia.
Hali ilizidi kuwa mbaya Septemba 22
mwaka huu majira ya saa 8 mchana baada ya wananchi kadhaa waliokuwa wakiteka
maji hayo kuambua kukivunja kisima hicho kinachomilikiwa na Bwana Noah
Mwambalaswa na kuukuta mwili wa marehemu ukiwqa kichwa chini miguu juu,hivyo
taarifa kutolewa kwa viongozi wa kijiji hicho.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Jimmy
Mwalupaso amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo Daktari wa Hospitali ya
Wilaya hiyo alifika eneo la tukio na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na
kubaini kuwa alipingwa na kitu kizito(nondo) kichwani hali iliyompelea marehemu
kuvuja damu nyingi mpaka mauti yalipomfika.
Hata hivyo baada ya uchunguzi wa
daktari mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya
mazishi yaliyofanyika kijijini hapo Septemba 23 mwaka
huu.
Comments