DC amkwida diwani chakulani • Ni kwenye hafla aliyoandaliwa Pinda

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, juzi alimkwida na kumuondoa kwenye mstari Diwani wa Kata ya Nyihogo, Amos Sipemba (CHADEMA), wakati akielekea kupata chakula cha mchana kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya msafara wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Tukio hilo lilitokea kwenye viwanja vya Rest House ambapo viongozi wengi wa kitaifa hufikia, ambapo Mpesya alianza kuwakaribisha wageni wa kimkoa kutangulia kupata chakula hicho huku akiwataka baadhi ya viongozi na wawakilishi wa wananchi kuungana na msafara huo.

Mpesya ambaye alionekana kuwa makini zaidi na ugeni huo wa kitaifa ambao ulikuwa wa kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo miezi minne iliyopita, alisimamia ugawaji wa chakula kwa watu wote waliokuwa katika msafara huo.

Baada ya kumaliza kutangaza wageni wa kimkoa aliwachagua Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji, Machibya Jiduramabambasi na makamu wake, Lucas Makulumo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Alfred Mahanganya na makamu wake, Mibako Mabubu pamoja na Diwani wa Kahama Mjini waungane kwa pamoja na wageni hao kupata chakula.

Diwani huyo wa Kahama Mjini, Abbas Omari, aliambatana na wenzake wa Kata ya Mwendakulima (TLP), Ntabo Majabi na Sipemba wa Kata ya Nyihogo (CHADEMA) katika msafara wa kupata chakula.

Mkuu huyo wa wilaya baada ya kuona hivyo, alimfuata Sipemba na kumzuia kuingia kwenye mstari huo lakini akaonekana kukaidi ndipo akanyanyuliwa kwa kushikwa kwenye mkanda wake wa suruali maarufu kama Tanganyika Jeki na kuondolewa katika mstari huo wa wageni na kukabidhiwa kwa polisi waliokuwa wakilinda usalama wa eneo hilo.

Kutokana na kitendo hicho cha udhalilishaji kwa diwani huyo, baadhi ya wenzake walianza kulalamika wakihoji kama tatizo ni kutoalikwa ni kwa nini yule wa TLP aliyeingia naye kwenye mstari ameachwa akiendelea kupata chakula.

Baada ya malalamiko hayo, Mpesya alikwenda tena kwenye mstari wa wageni na kumtaka diwani wa TLP naye atoke, ambapo alitii na kuondoka kurejea nyuma kusubiri zamu ya wageni wa wilaya.

Mkuu huyo alisikika akizungumza kwa ukali kuwa madiwani mara nyingi wamekuwa wakivuruga utaratibu wa itifaki katika misafara mbalimbali ya wageni wa kitaifa, hivyo aliwataka kuheshimu.

Baadaye wakati wageni wakiendelea kupata chakula, Mpesya alimfuata diwani huyo na kumnasua mikononi mwa polisi alikokuwa amemkabidhi na kumpeleka ndani walikokuwa wakipata chakula wageni wa kitaifa ili aungane nao.

“Mzazi hutakiwi kuwa na kinyongo na mtoto akifanya kosa kwani akikunyea mkono huwezi kuukata, leo diwani huyo atapata chakula na wakubwa humo ndani,” alisema Mpesya mbele ya wageni baada ya kumpeleka diwani huyo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.