RAIS KIKWETE AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI DARAJA LA KIGAMBONI


Thursday, September 20, 2012


* Aonya 'wenye viwanda' vya kutunga uongo kuacha tabia hiyo na kuelekeza nguvu kwenye maendeleo
* Asema viongozi wa vyama vya upinzani badala ya kupigania maendeleo, wapo tayari nchi iyakose
*Asema tukio la kuwekwa jiwe la msingi ujenzi huo, leo litawanyima usingizi badala ya kufurahi
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Rais Jakaya Kikwete leo, Alhamisi, Septemba 20, 2012, ameweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Daraja la Kigamboni, Dar es Salaam, huku akiwaonya watu ambao amewaeleza kuwa wanavyo viwanda vya kutunga uongo kuacha tabia hiyo na kuelekeza nguvu kwenye maendeleo.

Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia wakazi wote wa Kigamboni ambao wanaondolewa katika maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa daraja hilo na ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni kuwa watalipwa stahili na haki zao zote.

Daraja hilo la Kigamboni ambalo wazo la kujengwa kwake lilibuniwa kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka 30, tokea mwaka 1978, wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, linajengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 214.6 na litakuwa tayari katika muda wa miezi 36 ijayo, ingawa muda huo unaweza kupungua na kubakia miezi 30.

Daraja hilo ambalo litakuwa na urefu wa mita 680 linagharimiwa kwa pamoja na Serikali na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF ambalo litachangia kiasi cha asilimia 60 na Serikali asilimia 40.

Daraja hilo ambalo litakuwa na barabara sita za kupitisha magari kwa wakati mmoja linajengwa na kampuni mbili za China ambazo ni China Railway Construction Engineering Group na China Railway Major Bridge Engineering Company na mhandisi msimamizi wa ujenzi huo ni Kampuni moja ya Misri.

Daraja hilo linatarajiwa kupunguza adha ya usafiri kati ya Kigamboni na Dar es Salaam ambao kwa sasa unategemea vivuko au boti ndogo, mitumbwi ama wenye magari kulazimika kufanya mzungumo wa kilomita 52.

Kwa uamuzi wa sasa, wavuka kwa miguu ambao watakuwa na njia maalum kwenye daraja hilo pamoja na waendesha baiskeli watavuka bure bila malipo yoyote.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali haiwezi kudhulumu wananchi wake na hivyo watu wote ambao wanastahili fidia kutokana na ujenzi wa daraja hilo na mji mpya wa Kigamboni watalipwa haki na stahiki zao.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake haitaruhusu mtu yoyote kuzuia ama kuchelewesha miradi ya maendeleo ambayo inalenga kunufaisha watu wengi.

Rais Kikwete pia amewaonya watu ambao wamelifanya suala la kutunga na kusema uongo kama sehemu ya utamaduni wao. “Watu wana viwanda vya kuzalisha uongo. Wanashinda wanasambaza uongo kwenye mitandao, kila mahali. Wamepata hata kusema kuwa mimi nimemuuzia George Bush eneo la Kigamboni. Bush aje kufanya nini Kigamboni?”

Rais pia amesema kuwa wapo watu ambao hawapendi maendeleo ya nchi. “Wanatamani kila siku tushindwe kuwaletea wananchi maendeleo. Lakini watakufa kwa kihoro kwa sababu hatutashindwa. Kila tulilosema tutalifanya, litafanyika”.

Amesema kuwa thamani kubwa ya vyama vya siasa ni maendeleo ya wananchi. “Lakini wapo wenzetu ambao wanaudhika wakiona maendeleo. Wanapenda hata daraja hili lisijengwe. Leo hawatalala usingizi. Kazi ya vyama vya siasa ni kuweka maslahi yetu sote mbele.”

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.