Ni ijumaa nyingine tena. Kama kawaida yetu ni
wakati wa kupumua kidogo na kutafakari yaliyojiri na kupanga yajayo
hata kama hatuna uwezo kamili wa kujua yatakuwaje.Ni mipango tu.Bila
mipango hakiendi kitu.Ni wakati mwingine wa burudani. Leo tunayo heshima
kubwa kumkumbuka Hayati Freddy Supreme Ndala Kasheba(pichani). Huyu ni miongoni mwa magwiji wa muziki ambao Tanzania imewahi kuwa nao.
Wimbo unaitwa Dunia Msongamano.
Ndala Kasheba hapa alikuwa na kundi zima la Orchestra Safari Sound.
Ujumbe uliomo ndani ya wimbo huu, kama binadamu yoyote akiuzingatia, ni
wazi kwamba kuna mambo fulani fulani ambayo atayaepuka.Migongano
mbalimbali tuliyonayo wanadamu, kuanzia kimawazo mpaka kivitendo ni kwa
sababu wengi huwa tunasahau kwamba kila mtu ana akili zake.Kizuri
kwangu, kibaya kwako na mambo kama hayo.
Hapo chini ni baadhi tu ya maneno kutoka kwenye beti za kwanza kwanza za wimbo Dunia Msongamano. Zisome kwanza kisha bonyeza player hapo chini uusikilize wimbo wenyewe. Ijumaa Njema. R.I.P Ndala Kasheba.
DUNIA MSONGAMANO
Mawazo yamenijia leo,
Ya Mzee wangu alokuwa akisema,
Dunia ni msongamano wa watu wenye akili tofauti,
Mawazo yamenijia leo,
Ya Mzee wangu alokuwa akisema,
Dunia ni msongamano wa watu wenye akili tofauti,
Ukitaka kuishi vema fikiri kabla ya kujibu,
Jifunze kwa walimwengu, na walimwengu wajifunze kwako,
Dunia ni kuona mambo,
Na halafu kuyasahau
Wengine hupendelea kufurahia,
Wanaposikia fulani kafa,
Kufa kwa binadamu hupangwa na Mungu,
Namuomba Mwenyezi anipe maisha ooh
Comments