HOTUBA YA MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA MHE. SAMUEL SITTA KATIKA UFUNGUZI WA AWAMU YA PILI YA BUNGE HILO, DODOMA TAREHE 5 AGOSTI 2014
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta
Karibuni tena Dodoma Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge Maalum la kutunga Katiba ya nchi yetu. Sote tuna kila sababu ya
kumshukuru Mwenyezi Mungu wetu kwa kuendelea kutupa uhai na afya hadi leo
kutuwezesha kuwepo ndani ya ukumbi huu. Tupo humu ili tuitekeleze kazi
waliyotukabidhi Watanzania wenzetu milioni arobaini na sita (46) ya kuwapatia
Katiba mpya. Dhamana hii ni nzito na haistahili kufanyiwa ajizi.
Tunaendelea na shughuli zetu za
Bunge Maalum kwa kuzingatia Kanuni ya 30 (1) inayosema
"Akidi kwa kila kikao cha Bunge Maalum isipokuwa wakati wa kupitisha
uamuzi wa Bunge Maalum itakuwa ni nusu ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum".
Nimetaarifiwa na Katibu kwamba
wajumbe waliokuja Dodoma kuhudhuria ni zaidi ya robo tatu ya Wajumbe wote wa
Bunge Maalum. Nawashukuruni nyote kwa kuja hapa Dodoma ili kutimiza wajibu
wenu.
Kwa niaba yenu, nawashukuru
Watanzania wenzetu wote ambao kwa mamilioni wamedhihirisha utashi mwema wa
kisiasa kwa kuunga mkono hatua ya Bunge Maalum kuendelea na kazi zake hadi
tuipate Katiba inayopendekezwa ambayo wataipigia kura ya maoni. Kipekee na kwa
niaba yenu, nawashukuru kwa dhati viongozi wetu wa dini wa madhehebu yote wanaloliombea
Taifa hili mafanikio Bunge Maalum, wakitanguliza utaifa pamoja na amani ya nchi
na umoja ndani ya nchi na siyo ubinafsi na maslahi ya makundi.
Kwa leo sikupenda sana
kuzungumzia hoja mbali mbali zinazotawala magumzo ya mchakato wa Katiba mpya
hapa nchini, magumzo yanayoendeshwa na makundi maalum kwa jazba na hata matusi.
Hata hivyo nalazimika kutoa maelezo ya ufafanuzi kuhusu upotoshaji mkubwa
unaoendeshwa na baadhi ya watu kuhusu Bunge Maalum. Nikiwa Mwenyekiti wenu ninao
wajibu wa kuwafafanulia wananchi kuhusu uhalali wa shughuli za Bunge Maalum linaloendelea
na utaratibu wa shughuli zetu.
Ni
Rasimu ya Tume au la
Wapo wanaodai kuwa eti hapa
Bungeni hatujadili Rasimu ya Tume. Tuhuma hii haina ukweli hata kidogo. Msingi
wa majadiliano yote tangu tumeanza ni Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume
ya Katiba. Utaratibu ni kwamba pale ambapo wajumbe wanaona panafaa kurekebishwa
wanafanya hivyo. Maana ya rasimu ni andiko ambalo halijajitosheleza bila kupata
ithibati ya taasisi ya juu zaidi. Anayekabidhiwa rasimu anayo haki na mamlaka
ya kuirekebisha. Vinginevyo kujadili rasimu hakuna sababu. Itakuwa ni jambo la
ajabu na lisilo na mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka ya kujadili
Rasimu ikishaijadili iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati ilipowasilishwa!
Je
suala ni muundo wa Muungano tu?
Maudhui ya Rasimu yanajumuisha
baadhi ya masuala muhimu yafuatayo:
- Kuimarisha
Muungano wetu kwa kuleta uwiano bora
zaidi wa mamlaka ya Zanzibar na Tanzania Bara
ndani ya Muungano
- Kuimarisha
haki za binadamu ili kuwawezesha raia
wa kawaida kufaidi uhuru wa demokrasia bila
ubabe na dhuluma
- Kuzuia
wachache kufuja rasilimali za taifa bila kujali
maslahi ya wengi na ya vizazi vijavyo.
- Kujenga
uwiano sahihi na wenye haki baina ya wanawake
na wanaume katika nafasi za uongozi.
- Kubainisha
hatua zenye kuleta matumaini mapya ya maendeleo
kwa makundi maalum ya vijana wakulima
wadogo, wafugaji, wafanyakazi wa ngazi za
kawaida, walemavu, wafanya biashara wadogo na
wajasiriamali wengine.
- Kuweka
msingi imara wa kutungwa kwa sheria kakamavu
za kuzuia ukandamizaji wa raia, unyonyaji,
wizi wa mali ya umma, rushwa, hujuma
dhidi ya uchumi na kuzuia mapato haramu
na fedha chafu.
- Kutambua
haki za ardhi kwa wakulima, wafugaji na
wajasiriamali wengine ili kupunguza migongano
na migogoro.
- Kuweka
Misingi ya utawala bora inayozingatia uadilifu,
sifa stahiki na ufanisi.
- Kuwezesha
kutungwa kwa sheria bora zaidi zitakazosimamia
chaguzi zilizo za haki na huru zaidi
pamoja na kuwepo Tume za Uchaguzi zilizoboreshwa.
Zaidi ya hivyo, yapo mapungufu
katika Rasimu iliyopo kwa kuachwa masuala ya kuwezesha Serikali za mitaa; kutoa
maelekezo kuhusu masuala ya matumizi ya ardhi na rasilimali nyingine za Taifa.
Nini kinatuzuia kuiboresha Rasimu kwa kuyaongeza mambo haya ndani ya Katiba kwa
faida ya Taifa?
Yote haya ni masuala muhimu
ambayo yamo ndani ya rasimu na wakati wake wa kuyaweka sawa ndiyo huu. Pamoja
na umuhimu wake suala la muundo wa Muungano si suala la kutulazimisha
tuyaahirishe mazuri yote yaliyomo katika Rasimu tuliyopewa.
Uhalali
wa Shughuli za Bunge Maalum
Pamoja na uhalali wa kisheria wa
Bunge hili Maalum kuendelea kufanya kazi zake, linao pia uhalali wa kisiasa
kutokana na sifa za uwakilishi wetu na pia maudhui yaliyomo ndani ya Rasimu. Kutofautiana
maoni hakuwapi hadhi tofauti baadhi ya wajumbe kujiona wao wana uhalali zaidi
mbele ya wananchi kuliko wenzao. Ndiyo maana utaratibu umewekwa wa kupiga kura
na wa maridhiano. Utamaduni mpya unaoanza kujengwa na baadhi ya viongozi wa jamii
wa kususia mijadala halali na kwenda nje kuelezea hoja za upande mmoja hauna
nafasi katika Tanzania jamii isiyotaka fujo na utengano.
Wajumbe wa Bunge Maalum wanaoendelea
na kazi mjini Dodoma ni wateule wa Rais kwa niaba ya wananchi kwa kazi ya
kutunga Katiba. Kazi hii haiwezi kusitishwa kwa sababu tu wajumbe wachache
wameisusia. Tutazingatia matakwa ya sheria katika kufikia hatma ya mchakato wa
Katiba.
Mabadiliko
ya Kanuni
Kama nilivyoeleza hapo mwanzo, Rasimu
ina jumla ya sura kumi na saba (17) zenye mambo mengi yenye maslahi kwa
Watanzania wote. Kwa muda tuliopewa wa siku sitini (60) isingewezekana
kuikamilisha kazi tuliyopewa ndani ya muda. Ikumbukwe kwamba kwa Kanuni zilivyo,
kila sura mbili zinahitaji siku tisa kuzifanyia kazi. Kwa njia hiyo, ingetuchukua
siku takriban mia moja thelathini (130) ili kuikamilisha kazi hii! Pendekezo la
msingi hapa ni kwamba Kamati zetu kumi na mbili (12) zizingatie na kuzijadili
sura kumi na tano (15) za Rasimu na pia zikamilishe uandishi wa sura mbili
zilizojadiliwa awali na ikibidi ziongeze sura ambazo zitadhihirika kuwa ni
muhimu. Naamini mtiririko huu utatuwezesha kuwa na mpangilio bora zaidi wa sura
na ibara katika Katiba mpya. Tusingependa na wala isingefaa kuomba tena muda wa
ziada wa kazi ya Katiba ndio maana tunafanya mabadiliko ya Kanuni. Kamati ya
Uongozi iliyoketi Dar es Salaam tarehe 28 Julai 2014 imependekeza yafanywe
mabadiliko ya Kanuni za Bunge Maalum kuwezesha kazi ikamilike ndani ya muda tuliopewa.
Kwa hiyo nitawaomba tuyatafakari mapendekezo ya mabadiliko ya Kanuni na
hatimaye kuyapitisha ili ratiba ya kazi zetu iende sawa. Nitawaomba muikubali
ratiba iliyogawanywa leo na pia mkubali kuzibadilisha Kanuni kwa lengo nililolieleza
hapa.
HITIMISHO
Pamoja na maoni ya kila namna
yanayoendelezwa kujadili mchakato wa Katiba nje ya Bunge hili, ni muhimu wahusika
wapunguze jazba, chuki na upotoshaji. Bunge Maalum lisaidiwe kwa mawazo chanya
ili limalize kazi yake.
Sisi tuliomo humu katika Bunge
Maalum tuna wajibu wa kuifanya kazi yetu kwa umakini na kwa uadilifu ili kazi
yetu iwe bora. Tujadiliane kwa uungwana. Tofauti za mawazo zisitufanye tuingize
chuki na maneno yasiyofaa. Katika mabadiliko ya Kanuni nashukuru sasa Kiti
kimepewa mamlaka ya kushughulikia utovu wa nidhamu ndani ya wakati. Lakini
ninaamini haitakuwa lazima kwangu mimi au Makamu Mwenyekiti kutumia nguvu za
mamlaka yetu ila tu pale itakapobidi.
Nawatakia nyote Mkutano wenye
mafanikio kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
MUNGU
IBARIKI TANZANIA!
MWENYEKITI
BUNGE MAALUM LA KATIBA
Comments