RAIS KIKWETE AZINDUA JENGO LA KITEGA UCHUMI LA NSSF MOSHI



 Jengo jipya la Kitega Uchumi la NSSF Moshi, lililozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete,Waziri wa Kazi na ajira Mh.Gaudensia Kabaka(watano kushoto) Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt.Ramadhani Dau(wapili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama(wapili kushoto) pamoja na viongozi na wadau wengine wakikata utepe kufungua rasmi jengo la kitega uchumi la NSSF Kilimanjaro Commercial Complex mjini Moshi,Mkoani Kilimanjaro leo.

 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt.Ramadhani Dau baada ya hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la kitega uchumi la NSSF mjini Moshi leo.Katikati ni Waziri wa Kazi na Ajira Mh.Gaudensia Kabaka
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikagua jengo la upasuaji katika hospitali ya rufaa ya Mawenzi mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro muda mfupi baada ya kulifungua leo.Kulia ni Naibu Waziri wa Afya Dkt.Steven Kebwe.
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wauguzi wa hospitali ya rufaa ya Mawenzi mjini Moshi muda mfupi baada ya kufungua jengo la upasuaji na kuweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa wodi ya mama na watoto katika hospitali hiyo leo.(wanne kulia ni Naibu waziri wa Afya Dkt.Steven Kebwe,wanne kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama,Kushoto ni Mbunge wa Vunjo Agustino Lyatonga Mrema,na wapili kushoto ni Mbunge wa Moshi Vijijini Dkt.Cyril Chami.

 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt.Ramadhan Dau pamoja na wadau wengine wakitazama ramani ya jengo jipya la kitega uchumi la NSSF mjini Moshi Kilimanjaro Commercial Complex wakati wa hafla ya ufunguzi leo.


Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na chipikizi wa Tanzania Girl Guides wakati wa hafla ya ufunguzi wa jengo la kitega uchumi la NSSF mjini Moshi leo.Tanzania Girl Guides,UMATI,Tanzania Red Cross ni wadau wa NSSF katika mradi huo.

a.
 



Uongozi siyo kujisifu – Rais Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa uongozi siyo kujisifu na kujisifia tu bali ni kutenda vitendo na kufanya maamuzi yanayothibitisha na yanayolingana na sifa hizo.
Rais Kikwete ameyasema hayo, Jumanne, Februari 10, 2015, wakati alipofungua jengo la kisasa kabisa la kitega uchumi lenye thamani ya sh. bilioni 64 kwenye Manispaa ya Moshi katika siku yake ya kwanza ya ziara ya siku mbili ya kikazi Mkoani Kilimanjaro.

Jengo hilo linalojulikana kama Kilimanjaro Commercial Complex na lililoko katikati ya Manispaa ya Moshi limejengwa kwa ubia wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii la NSSF, taasisi ya Girls Guide Tanzania,  taasisi ya Red Cross na Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) na ndilo jengo kubwa kuliko yote katika manispaa hiyo.

Amelisifia uongozi na visheni ya maamuzi ya NSSF akisisitiza kuwa shirika hilo limethibitisha kwa vitendo sifa ambazo shirika hilo linazo na zimethibishwa. “Uongozi siyo kujisifia na kujisifu tu bali ni kutenda vitendo na kufanya maamuzi yanayothibisha na kulingana na sifa hizo na katika hilo NSSF imeonyesha njia.”

Jengo hilo ambalo ujenzi wake ulianza Desemba 2011 na kuchukua miaka mitatu limejengwa kwa pamoja na Kampuni ya Group Six International ya China na Advent Construction ya hapa nchini na litakuwa na maduka makubwa na madogo, maofisi, mabenki na kumbi za mikutano.

Akizungumza katika shughuli hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya wananchi na viongozi wa taasisi zilizoko katika ubia wa ujenzi wa Jengo hilo, Waziri wa Kazi na Ajira, Mheshimiwa Gaudencia Kabaka amesema kuwa ni muhimu kwa NSSF kuendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati na inayolipa, badala ya fedha hizo kubakia kwenye mabenki tu ambako zinaweza kukumbwa na athari za mfumuko wa bei.

Mapema, Rais Kikwete katika shughuli yake ya kwanza baada ya kuwasili Mkoani Kilimanjaro, alifungua wodi ya upasuaji na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa jengo la wodi ya akinamama na mtoto katika Hospitali ya Mkoa ya Mawezi katikati ya Manispaa ya Moshi. Mawenzi ni moja ya hospitali kongwe zaidi nchini ikiwa imeanzishwa mwaka 1920

Akizungumza kabla ya kufanya shughuli hizo mbili kubwa, Rais Kikwete ameelezea mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Sera ya Afrika ya mwaka 2007 iliyochukua nafasi ya sera ya mwaka 1997, ikiwa ni pamoja na kujenga maabara za kisasa katika kila hospitali ya Mkoa nchini na kuzifanya hospitali hizo kuwa za rufani ndani ya mikoa.

Rais Kikwete pia ameelezea jitihada za Serikali kupambana na magonjwa mbali mbali ikiwemo malaria na ukimwi na juhudi za kupunguza vifo vya watoto na akinamama kwa sababu ambazo zinazuilika.

Aidha, Rais amefafanua hatua zilizochukuliwa na Serikali yake kuongeza idadi ya madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya ambazo ni pamoja na ujenzi wa vyuo vya kufundishia madaktari katika hospitali mbili kubwa na mpya za Mlongazila na ile ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na upanuzi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhas cha Dar es Salaam.

Rais Kikwete pia amezungumzia matatizo ya kudumaa kwa watoto wadogo nchini akisema kuwa matunzo na lishe ya watoto wadogo katika siku 1,000 za kwanza za maisha yake ni muhimu sana katika maisha ya baadaye ya watoto.

Amesema kuwa kwa watoto wadogo lishe duni inasababisha kudumaa kwa watoto, watoto kuwa na kimo kidogo kuliko umri wao, watoto kuwa na uzito mdogo kulinganisha na umri wao, watoto kuwa na upungufu wa madini joto na upungufu wa vitamin A.

Rais Kikwete ataondoka kesho kurejea Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara hiyo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
10 Februari, 2015


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.