Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
akitoa taarifa ya mkutano wa wawekezaji (Round Table Investment Forum)
na wakuu wa nchi 5 za ukanda wa Afrika Mashariki utakaofanyika jijini
Dar es salaam kuanzia Machi 25 hadi 26 mwaka huu.
……………………………………………………………………….
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Tanzania inatarajiwa kuwa
mwenyeji wa mkutano wa wawekezaji (Round Table Investment Forum) na
Marais wa nchi 5 za ukanda wa Afrika Mashariki utakaofanyika jijini Dar
es salaam kuanzia Machi 25 hadi 26 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya mkutano huo
Mkuu wa wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki amesema kuwa
Marais hao Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Yoweri
Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Joseph Kabila wa Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo watahudhuria mkutano huo wakiwa wameambatana na
jumla ya wawekezaji 350.
Amesema Tanzania kwa mara
nyingine imepata heshima ya kuandaa mkutano huo na kufafanua kuwa
wawekezaji hao wamekwisha anza kuwasili jijini Dar es salaam kuanzia
Machi 22 , Machi huku marais nchi hizo wakitarajiwa kuwasili jijini humo
kuanzia Machi 24,2015.
Amesema wakiwa nchini Tanzania
Marais hao watashiriki kwenye mkutano wa wawekezaji utakaofanyika ukumbi
wa Mikutano wa Kimataifa Mwalimu J.K.Nyerere kuanzia Machi 23 hadi 26,
watatembelea bandari ya Dar es salaam ili kuona namna nchi za Ukanda wa
Afrika Mashariki zinavyoshirikiana katika masuala ya ushuru wa forodha
na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Amebainisha kuwa kabla ya
kuaondoka nchini Tanzania Machi 26, 2015 Marais hao pia watatembelea
miundombinu ya reli inayotumika kusafirisha mizigo nchi za maziwa makuu
kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika usafirishaji wa bidhaa
mbalimbali baina ya nchi zao.
KUHUSU MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA JIJINI DAR ES SALAAM.
Aidha, kuhusu mvua zinzoendelea
kunyesha katika jiji la Dar es salaam na kusababisha madhara, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amewataka wananchi kuzingatia
agizo la kuhama mabondeni na maeneo mengine hatarishi ili waepuka maafa
kufuatia watu 7 kupoteza maisha kutokana na kutokana na athari za mvua
zinazoendelea kunyesha.
Akifafanua kuhusu matukio hayo
Mhe. Sadiki amesema maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo na kupata
maafa hayo ni bonde la Mto Msimbazi na eneo la Buguruni kwa Myamani.
Amesema kuwa maeneo yaliyokumbwa
na mafuriko hayo yameonekana kuwa na wingi wa takataka ngumu na wingi
wa mifuko ya plastiki iliyotupwa na wakazi hao hali iliyochangia kuziba
mifereji inayopeleka maji katika bonde la mto Msimbazi na maji hayo
kuhamia kwenye makazi ya watu.
Ameeleza kuwa kazi ya uokoaji ,
kumwaga dawa kwenye maji yaliyotuama ili kuzuia athari ya magonjwa ya
milipuko, kuzibua mifereji na kukusanya taka katika maeneo hayo
inaendelea ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kuwataka wakazi hao
kuepuka kutupa taka ngumu zinazoziba mifereji ya maji.
Amesema Serikali inasubiri
taarifa kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa kwa maeneo ambayo
wakazi wake wanaishi kihalali ili waweze kupatiwa misaada ya kibinadamu.
Kwa upande wake Kamishina wa
Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova amethibitisha vifo
vya watu hao 7 waliopoteza maisha kutokana na maeneo yao kukumbwa na
mafuriko pamoja na athari ya Umeme.
Akitoa ufafanuzi wa vifo hivyo
amesema kuwa watu 5 wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji na wengine 2
wamepoteza maisha kutokana na ajali iliyosababishwa na Lori moja kugonga
Transfoma ya umeme eneo la Buguruni Mnyamani.
Kamishna Kova amesema tayari
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na
Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) wameunda kikosi kazi cha uokoaji.
Ametoa wito kwa madereva wa
magari ya mizigo, mgari binafsi na yale ya abiria kuepuka kupita katika
maeneo yaliyojaa maji ili kuepuka ajali na vifo vinavyoweza kuzuilika.
Comments