MBITA ALIVYOLETA UHURU WA SAO TOME NA PRINCIPE

 Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalenda, Zitto Kabwe (kushoto)  akimfariji Shella Mbita mmoja wa watoto wa marehemu, alipokwenda kuomboleza msiba huo Chang'ombe, Dar es Salaam leo.
                                             Marehemu Brigedia Jenerali Hashim Mbita
Mtanzania aliyetukuka na Mwafrika asiye na chembe ya mashaka anapumzishwa katika nyumba yake ya milele. Huyu ni Brigedia Jenerali Hashim Mbita aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) 1972 - 1994 na mtumishi wa Umma wa Tanzania akiwa Balozi na nafasi nyingine mbalimbali ikiwemo kuwa msaidizi wa Mwalimu Nyerere.
 Wakati tunampumzisha Mzee Mbita nimeona kuwashirikisha habari moja ambayo watu wengi hawaifahamu na mimi niliisoma kwenye Kitabu nikiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya mwisho ya Tisini. Hii ni hadithi ya kipekee kabisa ya namna Hashim Mbita alivyoharakisha Uhuru wa nchi mojawapo ya Afrika kwa mazungumzo yasiyo rasmi tu. 

 Moja ya kazi ambayo Kamati ya Ukombozi ya OAU ilikuwa ikifanya ilikuwa ni kutafuta vikundi vya ukombozi katika mataifa ya Afrika yaliyokuwa yakitawaliwa na wakoloni. Visiwa vya Sao Tome na Principe vilikuwa chini ya ukoloni mkongwe wa Ureno lakini hapakuwa na vyama vya ukombozi vyenye nguvu. 

Hashim Mbita alipoteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi alianza jitihada za kutafuta watu wa visiwa hivi ili kuunda vyama vya ukombozi. Huu ulikuwa ni wakati wa mapambano makali dhidi ya Wareno katika nchi za Msumbiji,

 Angola na Guinea Bissau na Cape Verde kwa Amilcar Cabral. Baada ya jitihada kidogo wakajulishwa kuwa kulikuwa na kikundi kinaitwa Committee for the Liberation of Sao Tome and Principe (CLSTP). 

Hata hivyo chama hiki hakikuwa hata na ofisi na hivyo Hashim Mbita akaagiza kutoka kwenye Bajeti ya Kamati ya Ukombozi kuwa wapewe dola 1000 za kimarekani ili kuweza kufungua ofisi jijini Libreville, Gabon.
Chama hiki cha ukombozi kilikuwa chini ya mtu anayeitwa Miguel Travaola. Hata hivyo mahusiano yalikuwa sio mazuri sana kutokana na kukosekana kwa umakini wa chama hiki cha ukombozi.

Lakini Mbita hakuchoka aliendelea kuwasiliana nao na kuwataka wajipange vizuri ili kuanza kazi ya ukombozi. Kamati ya Ukombozi iliendelea kuwalipia ofisi na kuwasaidia kuendesha migomo na maandamano katika visiwa hivyo ili kupaza sauti ya ukombozi.

Hata hivyo CLSTP haikuwa na nguvu kabisa nchini mwao na viongozi wao walikuwa wakitoa taarifa za uongo kwa Brigedia Mbita hali ambayo iliwafanya washindwe kuanza mashambulizi ya kumtoa Mreno Sao Tome and Principe.
 Akiwa safarini jijini Maputo kwa ajili ya kuandaa shughuli za uhuru wa Msumbiji, akiwa ameambatana na Joachim Chissano aliyekuwa Waziri Mkuu wa Msumbiji wakati wa mpito, Hashim Mbita akakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno Mario Soares.

 Kiutani tu lakini akiwa amekunja ndita Mbita akamwuliza Soares “ lini mnawapa uhuru watu wa Sao Tome and Principe”? Soares akamwuliza Mbita kama kuna watu wan chi hiyo wanaotaka Uhuru. Mbita akamjibu ndio wapo. 

Akamwuliza tena kama kuna chama chochote cha ukombozi huko ambacho anaweza kuongea nacho ili kuwapa uhuru, Mbita akajibu ndio kipo. Waziri huyu wa Ureno akasema basi nikutanishe nao tuanze mazungumzo.

Hashim Mbita aliporudi Dar es Salaam akatuma ujumbe kwenda Libreville na wakati huo CLSTP ilikuwa imepata kiongozi mwingine Dkt. Manuel Pinto da Costa. Akamwita aje Dar es Salaam, akampa salaam zile na wakakubaliana na Serikali ya Algeria kuwa mkutano wa mazungumzo ya uhuru wa Sao Tome and Principe yafanyikie huko. Ndani ya mwezi mmoja mazungumzo yakaanza mnamo tarehe 23 novemba 1974 na Chama cha CLSTP kikaunda Serikali ya Mpito.

Tarehe 12 Julai 1975 nchi ya Sao Tome and Principe ikapata Uhuru wake kutokana na mazungumzo ya utani tu na kukunja ndita ya Brigedia Jenerali Hashim Mbita na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno. Wakati watu wa Angola, Msumbiji na Guinea Bissau walishi

ka mtutu wa Bunduki kutafuta Uhuru wao, Sao Tome and Principe walipata uhuru wao kwa kazi ya mtu mmoja tu asiye raia wa nchi hiyo lakini mkombozi mkubwa wa bara la Afrika Hashim Mbita kutoka Tabora, Tanzania.

[Habari hii imesimuliwa kutoka kutabu cha Inside OAU – Pan-Africanism in Practice kilichoandikwa na C.O.C Amate. ]

Mungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Hashim Mbita mahala pema peponi. Amin

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.