WANAFUNZI WATAKIWA KUJILINDA DHIDI YA TABIA HATARISHI ZA KIMAPENZI

Na Anna Nkinda –Maelezo
20/4/2015 Wanafunzi wametakiwa kujilinda, kujiepusha na mazingira na tabia hatarishi ikiwemo vishawishi rika kama vile kutoanza mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo, utoro na ulevi kwa kufanya  hivyo watajiepusha na mimba za utotoni.

Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Temeke Sophia Mjema wakati akifunga mafunzo ya elimu ya afya ya uzazi, ujinsia na stadi za maisha kwa wanafunzi  na walimu wa shule za sekondari  za wilaya hiyo iliyopo  mkoani  Dar es Salaam.

Mjema alisema mimba za utotoni  ni  moja ya kikwazo cha  kuleta maendeleo katika jamii hivyo basi  kila mtu hana budi kuhakikisha anatokomeza tatizo hilo.

“Vijana  hasa wanafunzi ni kundi linalokabiliana na mabadiliko makubwa katika miili yao mabadiliko ambayo huwaweka katika hatari kubwa ya kukumbwa na matatizo ya kujamiiana na kupata mimba  katika umri mdogo, vifo vitokanavyo na uzazi, utoaji mimba na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana ikiwa ni pamoja na Ukimwi”.

Nawaomba sana mzingatie yale mliyojifunza ili muweze kukabiliana na tatizo la mimba za utotoni ambalo ni janga la taifa letu. Mimba za utotoni zinasababisha kuongezeka kwa umaskini katika jamii ikiwamo kukosa huduma muhimu, kukosekana kwa wasomi kwani watoto wa kike hushindwa kuendelea na masomo”, alisema Mjema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema mimba za utotoni zinasababisha kuongezeka kwa watoto wa mitaani, kuongezeka kwa vijana tegemezi na kushamiri kwa uhalifu, kuhatarisha maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua na watoto kukosa baba maalum na malezi bora.

Kwa upande wake  Meneja Uraghibishi  na Mawasiliano kutoka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Philomena Marijani alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa shughuli ya uzinduzi wa kampeni ya jilinde utimize ndoto yako iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana katika viwanja vya Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam na kuzinduliwa na Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete.

Philomena alisema, “Taasisi ya WAMA ina dira ya kuwawezesha wanawake na wasichana ili wawe na maisha bora kwa kufanya juhudi kuhakikisha wasichana na wanawake wanakuwa na maendeleo ya kielimu, afya na uchumi  kwani tatizo hili la mimba ni moja ya sababu inayowarudisha nyuma kimaendeleo wasichana wa kike wasiweze kufikia ndoto zao”.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mradi waEngenderhealth Tanzania Richard Killian, Dkt. Martha Kisanga ambaye ni Meneja wa Kanda ya Pwani aliipongeza Serikali kwa mchango wake katika kuendeleza  elimu ya afya hususan afya ya uzazi kwa vijana kwa kuweka mikakati na sera kwa ajili ya kuhakikisha vijana wanapata malezi na elimu bora ya afya ya uzazi.

Dkt. Martha alisema iwapo mikakati hiyo itatekelezwa  kwa umakini itasaidia kuhakikisha vijana wetu wanapata elimu bora ya afya ya uzazi ili kuepuka mimba zisizotarajiwa, utoaji wa mimba ovyo, magonjwa ya zinaa na Ukimwi na kujiepusha na vitendo vinavyohatarisha maisha yao.

“Nichukue nafasi hii kuhakikisha sisi wadau wa maendeleo tuko bega kwa bega na Serikali ili kutekeleza mikakati ya sera zinazohusu vijana, Taasisi yetu itaendelea kushirikiana na wilaya ya Temeke na zingine zitakazopendekezwa na WAMA kupitia Idara ya Afya ya Elimu kuhakikisha kwamba vijana wengi zaidi wanafaidika kutokana na elimu hii ambayo  itakuwa endelevu”, alisema Dkt. Martha.

Mafunzo hayo yako chini ya mradi wa kuzuia mimba za utotoni katika shule za sekondari unaotekelezwa na Taasisi ya WAMA na Engenderhealth kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la watu wa Marekani yalihudhuriwa na wanafunzi 65 na walimu 11 kutoka shule za Sekondari za Kibasila, Minazini, Miburani, Kurasini, Aboud Jumbe, Chang’ombe, Tandika, Keko, Lumo, Buza na Mbagala.

Mada zilizofundishwa ni uelimishaji rika, mila na desturi zinazoathiri Afya ya uzazi kwa vijana na elimu ya Afya ya uzazi itolewayo shuleni na katika vituo vya afya, ujinsia, stadi za maisha, dhana ya ushauri na unasihi, elimu ya magonjwa ya ngono, Ukimwi, njia za kujikinga  na mimba za utotoni na mamna ya kupanga matumizi ya muda katika saa.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.