NEC YAMSAFISHA DK MAGUFULI


By Waandishi Wetu, Mwananchi.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC) Jaji Damian Lubuva amesema mgombea urais mteule wa CCM, Dk John Magufuli hapigi kampeni bali kinachofanyika ni utambulisho wa mgombea wao kwa wananchi.
Kauli ya Lubuva imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Chama cha ACT-Wazalendo kuandikia barua NEC, ikilalamika kuwa Dk Magufuli ameanza kampeni kabla ya wakati.
Alisema NEC imepokea barua ya malalamiko ya ACT-Wazalendo inayolalamika kuwa Magufuli ameanza kampeni kabla ya muda na pia kulalamika kualikwa kwa mteule huyo wa CCM kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Michuano ya Kombe la Kagame, inayoanza leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Tume ina maadili yake, kwa mfano eti tumzuie asiende kwenye mechi , sisi tumzuie kama nani, huu si wakati wetu, wakati wetu ukifika tutakunjua makucha yetu” alisema.
 Alisema NEC haihusiki hata  na yale yanayotokea Dodoma,  bali itaanza kazi yake ifikapo Agosti 21 mara baada ya uteuzi rasmi wa wagombea.
Akizungumzia zaidi ziara hizo, Jaji Lubuva alisema tume hiyo haina kauli juu ya ziara ya Magufuli, bali akifanyacho ni mchakato tu wa ratiba ya chama chake.
 Jaji Lubuva alisema  kwa upande wa Sheria na Katiba, Nec itaanza kuchukua hatua kwa wale watakaokiuka kanuni kuanzia Agosti 22, pindi kipyenga cha kampeni kitakapoanza hadi Oktoba 24 kitakapomalizika.
“Katika kipindi hicho, tume inakuwa na nguvu ya kuwashughulikia wagombea, kwa sasa kinachotokea ni mambo ya vyama, sisi kwenye tume hatuna msingi wa kushughulikia hayo,” alisema.
Wakati Jaji Lubuva akisema hayo, Chama Cha Kijamii (CCK) wameamua kutumia wanasheria ili kuandaa mipango ya kumwekea pingamizi Dk Magufuli, kuwa anakiuka Sheria ya Uchaguzi kwa kufanya kampeni kabla ya wakati.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa CCK Renatus Muhabi, alisema Tume ya Uchaguzi (NEC) huenda nayo ikashtakiwa kwa kushindwa kuwajibika licha ya kuwa ndiyo msimamizi wa Sheria ya Uchaguzi.
“Tumeshampa kazi mwanasheria, Aloys Rugazia kuandaa pingamizi baada ya kutoridhishwa na majibu ya Jaji Lubuva.
“ Majibu yake Jaji Lubuva ni wazi yanaonyesha kuwa anaiogopa CCM, maana ndiyo iliyompa hiyo nafasi, hapo unaweza kuona kwa nini tumekuwa tunalilia tume huru, yeye anapodai hahusiki na kufuatilia mambo anayofanya mgombea huyo, eti hadi pale atakapochukua fomu ya NEC, huu siyo utawala bora ni ukiukwaji mkubwa,” alisema.
Muhabi alisema CCK imeamua kujitolea kulifuatilia jambo hilo kwa karibu licha ya kwamba wapinzani wenzao wakiwamo Ukawa wapo kimya, wanaamini kwamba ukimya huo unatokana na kutingwa kusaka mgombea wao wa urais, hivyo wao watajitahidi hadi dakika ya mwisho kutetea haki na demokrasia ndani ya vyama. 
Wakili anayeshughulikia utaratibu wa kufungua kesi hiyo, Rugazia, alikiri kuwapo kwenye mchakato wa kufungua kesi, lakini hatua hiyo itafuata pale watakapojiridhisha kuwa kuna makosa ya kisheria kwenye matendo ya Dk Magufuli na mikutano anayofanya.
“Wanasiasa wana utazamaji wao wa mambo nasi kama wanasheria tuna utazamaji wetu, hivyo tunachofanya sasa ni kwamba tupo kwenye hatua za kujiridhisha kwanza kuangalia vipengele vya sheria ya uchaguzi kwa ujumla, ikiwamo masuala ya kampeni baada ya hapo ndiyo tutajua mwelekeo mzuri wa jambo hili,” alisema Wakili Rugaziya.
 Magufuli kutambulishwa Mwanza
 Wakati  kukiwa na ombwe hilo jijini  Dar es Salaam, leo Magufuli anatarajia kutambulishwa kwa wakazi wa Mwanza katika tukio litakalofanyika Uwanja wa Furahisha.
Dk Magufuli anatarajiwa kuwasili jijini Mwanza saa 8:00 mchana, na kwenda moja kwa moja Uwanja wa Furahisha ambako atahutubia mkutano wa hadhara.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya CCM Mkoa wa Mwanza, mara baada ya utambulisho huo, atakwenda jimboni kwake Chato ambako atafanya  mkutano na kufanya misa ya shukrani na kesho atakuwa Geita kwa ajili ya utambulisho mwingine.
Akizungumza ofisini kwake juzi, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu alisema Dk Magufuli anakuja kutambulishwa rasmi baada ya kufanya hivyo miji ya  Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar tangu alipopitishwa na chama chake Julai 12.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alilieleza Mwananchi wiki hii kuwa chama hicho hakina kawaida ya kumtambulisha mgombea wake nchi nzima, bali hufanya hivyo Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza pamoja na Zanzibar.
“Tunaunga mkono na kupongeza mkutano mkuu kutuchagulia mgombea urais anayeaminika, hatuna shaka naye tunamfahamu alivyo mchapakazi na mwadilifu asiyepindisha maneno na kuchukia uvivu, hivyo tumuunge mkono kwa ajili ya maendeleo ya Wanamwanza na taifa,” alisema Mtaturu.
Imeandaliwa na Beatrice Moses, Florence Majani, Dar na Jesse Mikofu, Mwanza.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.