UNAMPENDA MTU KISA MASILAHI? JIFUNZE HAPA!

JUMAMOSI nyingine, tunakutana katika uwanja wetu wa kupeana darasa la uhusiano. Naamini kupitia hapa tunapata kujifunza mengi, karibu na leo tujifunze pamoja.Tuanze kuidadavua mada iliyopo mezani. Mapenzi siku zote ni hisia. Raha ya penzi ni kumpata mpenzi akupendaye ambaye nawe unampenda vivyohivyo.
Asikwambie mtu, mnapoogelea kwenye penzi ambalo kila mmoja anampenda mwenzake sawasawa na anavyopendwa maisha huwa ni matamu sana. Hakuna kinachoharibika, mnafurahia penzi lenu.Penzi la namna hiyo huwa linawaacha huru wapendanao. Kila mtu anakuwa na amani. Haijalishi mnapitia changamoto gani katika maisha lakini linapokuja suala la upendo, mnasahau changamoto zote mnazokutana nazo.
Wawili mnapopendana, penzi huwa linageuka faraja. Linageuka dawa ya kupoza machungu ya matatizo mliyonayo. Linaondoa sononeko la moyo kama lipo. Mathalani, mwanaume anapokuwa ametoka katika mihangaiko ya kila siku na amechoka, mwanamke huchukua jukumu la kumpa faraja mpenzi wake.
Yawezekana akawa ametibuliwa na bosi wake kazini. Akifika kwa mpenzi au mke wake, anasahaulishwa ‘nakozi’ zote alizopigwa na bosi wake. Atafurahia mapokezi, anafarijika kwa penzi shatashata analooneshwa na mpenzi wake.
Katika mazingira hayo, taratibu mwanaume analainika. Na yeye anajikuta anajibu mashambulizi, anarudisha penzi analopewa, wanakuwa kwenye ulimwengu wa tofauti kabisa. Anasahau kabisa maneno yote mabaya aliyoambiwa na bosi wake.
Kama alikashifiwa, alidharauliwa, vyote hivyo anavitupa kapuni. Anaanza upya. Kesho atakwenda akiwa na furaha kama si yule aliyekorofishwa.Watu wanaopendana huwa wanaaminiana. Hakuna anayemhofia mwenzake. Hakuna anayemhisihisi vibaya mwenzake. Kila hatua wanayopiga katika penzi lao ni furaha. Wanapokuwa pamoja, wanakuwa huru. Kila mtu anajiachia.
Hakuna anayekuwa na hofu kwamba mwenzake anaweza kupigiwa simu na mchepuko, achilia mbali ujumbe mfupi utakaopotea njia. Hata ukipotea njia, hakuna mwenye shaka ya kuujadili kisha kuyamaliza.
Penzi la namna hiyo huwa halichochewi na masilahi. Hutoka moyoni. Kila mmoja anamkubali mwenzake kwa hali yoyote. Si kwamba ana fedha, gari au kitu chochote cha thamani. Anaguswa kupenda kwa kusukumwa na moyo wake.
Kinyume cha penzi hilo, yapo mapenzi ya masilahi. Kutokana na hali ya sasa kuwa ngumu kiuchumi, penzi la masilahi limeshamiri. Watu wengi wanaingia kwenye uhusiano kwa kigezo kwamba atahakikishiwa maisha mazuri. Siwalaumu lakini ukweli ni kwamba baadaye wanaambulia mateso.
Anabadilika na kuwa mtu asiyekuwa na penzi la dhati. Kwa yeyote ambaye atakuwa na masilahi mazuri, haoni tatizo kuwa naye.Anaingia kwenye uhusiano kwa kuwa amehakikishiwa mlo wa kila siku. Amehakikishiwa kutembelea gari zuri, kuvaa vizuri.
Penzi la aina hiyo ni hatari sana. Moja kati ya athari kubwa zinazotokana na penzi la aina hiyo ni kupotezewa muda. Utaishi kwa kutumika kila siku. Penzi lako litakuwa haliangalii ‘future’.
Utaongozwa na tamaa. Utakuwa na huyu, ikitokea uchumi umeyumba kwa huyo mhusika, unahamia kwingine. Muda unazidi kuyoyoma. Magonjwa ni mengi, tamaa inaweza kukuponza. Ukajikuta unaambulia magonjwa hatari ikiwemo Ukimwi.
Kwa wanawake ni hatari zaidi, ndicho kipindi anapojikuta akizalishwa bila mpangilio. Watoto ambao wanakosa baba maalum.Soko lake linapungua na kubaki kujilaumu kwa kuzisikia ndoa kwa wenzake. Unageuka kuwa uwanja wa mazoezi, anayetaka kuzaa na wewe mwenye fedha zake anakutumia kisha anakuacha solemba. Hiyo ndiyo hatima ya maisha yako.
Unajiepushaje na tatizo hili? Kuwa makini sana katika suala zima la kuchagua mtu sahihi pindi unapoanza kuingia penzini. Kigezo cha kwanza kiwe penzi la dhati na si masilahi. Jijengee hali ya kuridhika. Jenga utamaduni wa kutafuta fedha zako. Ridhika na kile unachokipata, pambana kufikia malengo yako.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.