SERIKALI YATOA BILIONI 2.3 KUWALIPA WAFANYAKAZI WA NIDA



SERIKALI imeipatia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Shilingi Billioni 2.3 (Bilioni mbili na milioni mia tatu) kwa ajili ya kuwalipa waliokuwa watumishi wa muda wa mamlaka hiyo, wapatao 597, waliosimamishwa kazi hivi karibuni.
Malipo hayo yanahusisha mishahara yao ya miezi minne, ukiwemo mshahara wa mwezi mmoja wa notisi ya kusimamishwa kazi, pamoja na malimbikizo ya madeni yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Kabla ya NIDA kuwalipa watumishi hao fedha hizo, Wizara ya Fedha na Mipango iliamua kufanya uhakiki ili kujiridhisha kama madai hayo yalikuwa sahihi.
Uhakiki huo ulihusisha mahojiano ya ana kwa ana na watumishi hao pamoja na kupitia nyaraka mbalimbali zikiwemo majalada, mikataba ya ajira, madaftari ya mahudhurio, taarifa za kazi za kila siku na namba zao za akaunti za benki zilizokuwa zikitumika kulipa mishahara.
Katika uhakiki huo imebainika kuwa kulikuwa na kasoro ama changamoto kadhaa zikiwemo za kimikataba kati ya NIDA na watumishi hao.
Wakati wa zoezi hilo, jumla ya watumishi 597 walipaswa kuhakikiwa lakini majina ya watumishi yaliyowasilishwa kuhakikiwa ana kwa ana kutoka NIDA, Tanzania bara yalikuwa 565.
Hata hivyo, watumishi 516 pekee ndio waliojitokeza katika zoezi hilo na wengine 49 hawakujitokeza.
Watumishi wa muda 32 kutoka NIDA Tanzania Zanzibar, wanaofanya jumla ya watumishi wa Mamlaka hiyo waliosimamishwa kazi kufikia 597, walihakikiwa kwa kupitia majalada yao yaliyoko ofisi za NIDA Makao Makuu, na kubaini mikataba yao haikuwa na kasoro.
Kwa mantiki hiyo watumishi 427 kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ndio waliokidhi vigezo vya kulipwa stahili zao za kuachishwa kazi.
Aidha, watumishi wengine 121, walibainika kuwa na kasoro mbalimbali ambazo zinapaswa kurekebishwa na Menejimenti ya NIDA kabla ya kufanya malipo hayo.
Baadhi ya kasoro zilizobainika katika uhakiki huo ni pamoja na kukosekana kwa mikataba na majalada yao katika Ofisi ya mwajiri, kukosekana majina yao kwenye daftari la mahudhurio kazini, kuwa na utata kwenye mikataba (kutofautiana tarehe na sahihi za wahusika), kufanana kwa namba za majarada, na kukosekana kwa barua za kusitishwa kazi.


Wizara ya Fedha na Mipango imemaliza kazi yake ya uhakiki na kwamba jukumu la kuwalipa watumishi wa NIDA wanaostahili limeachwa mikononi mwa menejimenti ya NIDA.


Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO


13 Mei, 2016

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.