NA BASHIR YAKUB -
Mtu akimuumiza mwingine na aliyeumizwa akapata jeraha linalosababisha alazwe hospitali au asilazwe lakini aendelee kuishi na jeraha lake hilo, Swali litakuwa je mtu huyo akifa baada ya miezi sita, saba , kumi au zaidi tokea siku alipoumizwa kifo chake kitakuwa kimesababishwa na yule aliyemuumiza ?.
1.NINI MAANA YA KUSABABISHA KIFO.
Kusababisha kifo kunaweza kuelezwa katika namna nne tofauti. Na hii ni kwa mujjibu wa Sura ya 16, kifungu cha 203, Kanuni za adhabu.
( I ) Mtu amemtia jeraha mtu mwingine. Na kutokana na jeraha hilo mtu huyo anakufa. Haijalishi amekufa akiwa anapata matibabu au laah. Na haijalishi kama matibabu hayo yalikosewa au laah. La msingi ni kuwa matibabu hayo yalifanywa kwa nia njema na hiyo yatosha kusema fulani aliyesababisha jeraha ndiye huyohuyo aliyesababisha kifo.
( ii ) Pengine ni pale ambapo mtu anamlazimisha mtu mwingine kwa kumtishia akimtaka atende tendo ambalo linasababisha kifo cha mtu mwingine. Mtu huyo aliyetishia atahesabika kusababisha kifo.
(iii) Zaidi, kutotekeleza wajibu ambako kunapelekea kifo nako ni kusababisha kifo. Kwa mfano daktari aliyetakiwa kumpokea mgonjwa na kumtibia akishindwa kufanya hivyo na mgonjwa akafa basi atakuwa amesababisha kifo.
( iv) Pia ikiwa mtu ana jeraha au ugonjwa ambao kwa vyovyote vile ungemsababishia kifo lakini akatokea mtu mwingine akatenda tendo ambalo linasababisha mgonjwa afe haraka basi mtu huyo aliyetenda anahesabika kusababisha kifo.
2.KUTOCHUKULIWA KUUA BAADA YA MWAKA NA SIKU.
Kifungu cha 205 ( 1 ) kanuni za adhabu kinasema kuwa mtu hatachukuliwa kuwa amemuua mtu mwingine kama kifo hakitatokea ndani ya mwaka mmoja na siku moja tangu siku ya sababu ya kifo.
Maana yake ni kuwa iwapo mtu atamsababishia mtu mwingine jeraha au maumivu yoyote , na kutokana na jeraha hilo au maumivu hayo mtu akafa ndani ya mwaka mmoja na siku moja tangu siku aliposababishiwa madhara hayo, basi yule aliyesababisha madhara atahesabika kusababisha kifo.
Ikiwa atakufa baada ya mwaka na siku moja basi yule aliyeumiza au kujeruhi hawezi kuhesabika kama amesababisha kifo.
3. KUHESABIKA KWA MUDA.
Kawaida muda huanza kuhesabika mara tu tendo lililosababisha kifo linapotendeka. Kuna siku tendo lilipotendeka halafu kuna siku tendo lilipoacha kutendeka. Siku tendo lilipotendeka ni kwa mfano siku mtu alipopigwa au siku aliyoumizwa.
Wakati siku tendo lilipoacha kutendeka ni kwa mfano siku daktari alipoacha kumpa matibabu mgonjwa, au siku fulani alipoacha kumpa fulani chakula na hivyo kupelekea kifo chake. Ni kuanzia siku hiyo ambapo muda huhesabika hadi mwaka na siku moja.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MWANDISHI WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE. ”. 0784482959, 0714047241 bshiryakub@ymail.com
Comments