MCHENGERWA: KULA SAHANI MOJA NA WANAOINGIZA MIFUGO MIPYA RUFIJI


MBUNGE wa jimbo la Rufiji, Mohammed Mchengerwa, aliyempakata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, akiwa na baadhi ya wananchi wa jimbo hilo baada ya mkutano. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji

MBUNGE  wa jimbo la Rufiji, mkoani Pwani, Mohammed Mchengerwa ameahidi kula sahani moja na baadhi ya viongozi wakiwemo wa vijiji ambao wanadaiwa kushirikiana na wafugaji kuingiza mifugo kiholela jimboni hapo.

Mbali na hilo amesema amejipanga kuvalia njuga suala la migogoro ya ardhi inayotokana na jamii ya wafugaji na wakulima.

Ameeleza pande hizo zimekuwa zikisigana mara kwa mara wakigombania maeneo hali inayosababisha kutokea kwa vurugu ambapo wakati mwingine hupelekea uvunjifu wa amani.

Aidha Mchengerwa alisema kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwa wakulima na wafugaji  katika halmashauri ya Rufiji kunatokana na  baadhi ya wafugaji kuamua kuvunja sheria na taratibu zilizopo.

Alisema hayo juzi huko utete, wilayani Rufiji ,wakati akizungumza na viongozi mbalimbali namna ya kukabiliana na kero hiyo.

Mchengerwa alisema hawezi kuwavumilia wale wote ambao wataonekana wanakwenda kinyume na sheria za nchi, na kuhakikisha kila mfugaji na mkulima anatengewa maeneo rasmi kwa ajili ya kufanyia shughuli zao.

Alielezea kuwa nia yake kubwa ni kusimamia mikakati iliyowekwa na serikali ambayo itaweza kuwasaidia wote wafugaji na wakulima kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri.

“Ninatambua kuwepo kwa changamoto kubwa baina ya pande hizi , lakini kuna kila sababu ya kuliondoa ama kupunguza kwa kuwa na kikomo cha mifugo hii"

" Wafugaji wanapaswa kuheshimu maeneo ya wakulima kwakuwa sidhani kama shamba linahama ila tatizo ni mifugo kuingia kwa wakulima "alisema.

Akizungumza juu ya viongozi wanaoshirikiana na wafugaji kuingiza mifugo yao kiholela, Mchengelwa alisema atakula sahani moja na viongozi hao ili kukomesha iingizwaji wa mifugo mipya kwenye maeneo ya Rufiji.

Mbunge huyo alisema, anatambua wananchi wa jimbo lake wanategemea sana shughuli za kilimo hivyo wafugaji waendelee kuelimishwa juu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Alisisitiza kundi la wafugaji litumie maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao na kuacha kupindisha sheria za nchi.

Mchengerwa alisema hata kwa upande wa wakulima kuwaeleza waheshimu maeneo ya wafugaji.

Aliwashauri wafugaji walio na ng'ombe wengi kuwauza kwa tija na kubaki na ng'ombe wachache watano ama kumi ambao wataweza kuwachunga na ndio ufugaji wa kisasa.

Mchengelwa aliwataka wafugaji kubadilika na kuacha ufugaji wa kudhurula na mifugo mingi ili kuondoa migogoro isiyo na manufaa kwenye jamii.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji, Saidina Malenda, alisema atashirikiana bega kwa bega na viongozi wenzake kwa lengo la kuweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi wa Rufiji.

Saidina alisema tatizo la wakulima na wafugaji ni lazima lisichukuliwe ajizi hivyo viongozi kwa umoja kuanzia ngazi ya kijiji wanapaswa kulisimamia na kuwachukulia hatua wale wanaopindisha sheria.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.