Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa mwaka wa Benki ya Dunia na IMF jijini Washington DC, Marekani

 Ujumbe wa wataalamu wa Fedha, Sera na Uchumi kutoka Tanzania wakifuatilia kwa makini Mazungumzo ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose (hawapo Pichani), Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Washington DC, Marekani, ambapo unafanyika Mkutano wa Mwaka wa Benki hiyo ambayo Tanzania ni Mwanachama, wa kwanza kushoto ni Kamishna wa Sera Augustine Ollal, Kamishna wa Bajeti John Cheyo na Kaimu Kamishna wa Fedha za Nje Mamelta Mutagwaba.
 Ujumbe wa wataalamu wa Fedha, Sera na Uchumi kutoka Tanzania wakifuatilia kwa makini Mazungumzo ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose (hawapo Pichani)
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose walipokutana ofisini kwake Jijini Washington DC, Marekani, ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Tanzania na namna Benki hiyo ilivyojipanga kuhakikisha kuwa inaiwezesha Tanzania kufikia ndoto yake ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025
 Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakishikana mikono kuonesha umoja na mshikamano mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya ujumbe huo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, Jijini Washington DC nchini Marekani, ambako ujumbe huo unahudhuria Mkutano wa Mwaka wa Benki hiyo.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Katikati, Akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia kanda ya Afrika mara baada ya viongozi hao kumaliza mazungumzo yaliyogusia Nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi, Jijini Washington DC, nchini Marekani, ambapo Tanzania inashiriki Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF.
 Baadhi ya wajumbe wa Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF, baada ya kumalizika kwa kikao kati ya ujumbe huo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, wakiwa nje ya Majengo ya Benki hiyo Jijini Washington DC nchini Marekani. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Kamishna wa Fedha za nje, Wizara ya Fedha na Mipango, Mamelta Mutagwaba, Kamishna wa Bajeti, John Cheyo, Kamisha wa Madini James Andilile na Kamishna wa Sera Augustine Ollal.
 Wajumbe kutoka takribani nchi 180 duniani kote, wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF, wakiwa katika Siku ya kwanza ya Mkutano wa Mwaka wa Taasisi hizo Jijini Washington DC nchini Marekani, Tanzania inawakilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt, Philip Mpango ambaye ameongoza ujumbe wa wataalamu wa Fedha na Uchumi katika mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (wa kwanza kushoto), Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (wa pili), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania BOT, Prof Benno Ndulu (wa tatu kutoka Kushoto), Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania BoT Dkt. Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Kamisha Msaidizi wa Nishati, Wizara ya Nishati na Madini, James Andilile, wakiangalia ripoti iliyotolewa na timu ya wataalamu wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF, kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini Tanzania kwa ufadhili na mkopo kutoka Taasisi hizo.
Ujumbe wa Tanzania na badhi ya  viongozi wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF wakikatisha Mitaa ya Jiji la Washington DC nchini Marekani kwa miguu  kuwahi vikao mbalimbali vinavyoendeshwa na Taasisi hizo kabla ya kufikiwa kwa kilele cha Mkutano wa Mwaka wa Taasisi hizo Oktoba 9 mwaka huu. Picha zote na Wizara ya Fedha na Mipango.

Na Benny Mwaipaja, MoFP
Washington DC, Marekani
8.10.2016

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo na Utalii ili ziweze kutoa mchango mkubwa kuinua uchumi wa Taifa pamoja na kuwaondoa wananchi wake kutoka katika lindi la umasikini
Waziri Mpango ameyasema hayo Jijini Washington DC, nchini Marekani, wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala yanayohusu utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na taasisi hiyo.
Amesema kuwa kilimo kinaajiri asilimia kubwa ya watanzania hivyo mapinduzi yanayokusudiwa katika sekta hiyo ni kuendesha kilimo biashara kwa kuongeza uzalishaji na  thamani ya mazao ya wakulima.
Kuhusu sekta ya Utalii, Dkt. Philip Mpango anayeongoza ujumbe wa wataalamu wa Uchumi na Fedha katika Mkutano wa Mwaka ulioandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, IMF, amesema kuwa serikali inakusudia kupitia upya kodi zinazoleta kero mbalimbali katika sekta hiyo pamoja kilimo.
Eneo jingine alilotaka Benki ya Dunia kuingilia kati, ni kuipatia Tanzania Mkopo na ruzuku utakaosaidia kukabiliana na madeni yake makubwa inayodaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja madeni ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini, TANESCO, ili shirika hilo liweze kujiendesha kwa faida na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa haraka.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, ameihakikishia Tanzania kuwa pamoja na miradi mingine, itafadhili mradi mkubwa wa kilimo wa ukanda wa kusini “Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT)” ili kukifanya kilimo kuwa na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Mimi nimefika Tanzania na ninaifananisha nchi hiyo kuwa itafikia ama kuzidi hadhi ya Dubai kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo ambazo zikisimamiwa vizuri zitaibadili kabisa nchi hiyo kimaendeleo” alisema Larose.
Ameitaka Tanzania kutosita kuitumia ipasavyo benki hiyo kufanikisha malengo yake ya maendeleo na kwamba yeye mwenyewe binafsi pamoja na kwamba anaongoza kundi la nchi 22 za kiafrika katika Benki hiyo, atahakikisha Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, inanufaika na uwepo wa Taasisi hiyo.
Mkurugenzi huyo Mtendaji amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, namna anavyosimamia mambo kwa nguvu zake zote na ametoa pole kwa nchi hiyo kutokana na madhara iliyoyapata kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililoukumba mkoa wa Kagera na mikoa mingine jirani.

Ameahidi kuwa Benki hiyo itatuma wataalamu watakaosaidia kufanya utafiti na kuishauri nchi kitaalamu na kimiundombinu namna ya kukabiliana na majanga ya matetemeko pamoja na vifaa vitakavyosaidia kutoa tahadhari kabla ya kutokea kwa majanga kama hayo.

0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MATOKEO YA KIDATO CHA PILI, DARASA LA SABA YATANGAZWA ZANZIBAR

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

ZAIDI YA WANANCHI 500 KUSHIRIKI MAFUNZO YA MKIKITA YA KILIMO CHA PAPAI SALAMA

MKIKITA YATOA OFA KWA KILA HEKA YA PAPAI SH. MIL. 2 KUTANDAZA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI

WATEJA WA NSSF DAR WATIMULIWA KWA MTUTU WA BUNDUKI

DIAMOND AITWA NA NYOTA YAJAA GOMS

KAMISHNA MARIJANI AZINDUA CHAMA CHA WAFUGAJI MBWA TANZANIA (TCA)

PICHA:NYOKA AINA YA CHATU AUWAWA KANISANI BAADA YA KUKUTWA NYUMBANI KWA MFANYABIASHARA MAARUFU JIJINI ARUSHA AKISADIKIWA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA