MAJARIBIO YA UTAFITI WA HALI YA UMASIKINI UNAENDELEA KUFANYIKA MKOANI DODOMA NA KILIMANJARO
Benny Mwaipaja, WFM - Dodoma

29 Juni, 2017.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), inakamilisha majaribio ya utafiti wa hali ya umasikini katika mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro kabla ya kuanza utafiti huo nchi nzima mwezi Agosti, mwaka huu.

Hayo yamesemwa mjini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ulipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu mjini humo.

Amesema kuwa ana matarajio kwamba mchakato wa taarifa za utafiti huo zitafanywa mjini Dodoma baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi hiyo inayojengwa kwa gharama ya shilingi 11.6 bilioni, zikiwa ni fedha za mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Dkt. Chuwa ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa wakusanya taarifa za utafiti huo ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi za hali ya umasikini nchini kwa ajili ya kutathmini programu mbalimbali na kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi wake.

Nae Mshauri wa Masuala ya Kitakwimu kutoka Benki ya Dunia nchini Tanzania, Elizabeth Talbert amesema kuwa Benki yake imetoa mkopo huo kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Bara na Zanzibar kutokana na Benki hiyo kuona mchango mkubwa wa takwimu katika maendeleo ya nchi yoyote ile duniani.

“Tumefurahishwa na kasi ya ujenzi wa Ofisi hii hapa mjini Dodoma na tunaamini ujenzi wake utakamilika kwa wakati ili kazi za kitakwimu ziweze kufanyika katika mazingira mazuri na tunaamini hatua hii italeta mchango mkubwa katika masuala ya kitakwimu hapa nchini” alisema Bibi Talbert.

Amesema kuwa Jengo la Ofisi ya Takwimu kwa upande wa Zanzibar limekamilika na huenda likaanza kutumika mapema Julai mwaka huu hatua ambayo inaleta mageuzi makubwa katika tasnia hiyo ya ukusanyaji wa takwimu mbalimbali zinazoisaidia nchi kupanga mipango ya maendeleo ya watu wake.

Kwa upande wake Mkandarasi Msanifu Majengo Mhandisi Ramadhani Shomvi anayesimamia ujenzi wa jengo hilo litakalo kuwa na ghorofa 6, amesema kuwa kampuni yake itakamilisha ujenzi huo mwezi Februari, 2018.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina chuwa (wa pili kushoto) akingalia kitofali kinachotengezwa na mkandarasi anayejenga jengo la Taasisi hiyo wakati Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ulipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu linalojengwa mkoani Dodoma.
Mshauri wa Masuala ya Kitakwimu kutoka Benki ya Dunia nchini Tanzania, Elizabeth Talbert (kushoto) akisisitiza jambo wakati Ujumbe kutoka Benki hiyo ulipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu linalojengwa mkoani Dodoma.
Mkandarasi Msanifu Majengo, Mhandisi Shomvi (aliyevaa sweta kulia) anayesimamia ujenzi wa jengo la ofisi ya Taifa ya Takwimu linalojengwa Mkoani Dodoma akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo wakati Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ulipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo hilo mjini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina chuwa (wa pili kushoto) akifurahia jambo na timu ya wataalamu wa ujenzi na ujumbe kutoka Benki ya Dunia ulipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu linalojengwa mkoani Dodoma.

(Picha: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MATOKEO YA KIDATO CHA PILI, DARASA LA SABA YATANGAZWA ZANZIBAR

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

ZAIDI YA WANANCHI 500 KUSHIRIKI MAFUNZO YA MKIKITA YA KILIMO CHA PAPAI SALAMA

MKIKITA YATOA OFA KWA KILA HEKA YA PAPAI SH. MIL. 2 KUTANDAZA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI

WATEJA WA NSSF DAR WATIMULIWA KWA MTUTU WA BUNDUKI

DIAMOND AITWA NA NYOTA YAJAA GOMS

KAMISHNA MARIJANI AZINDUA CHAMA CHA WAFUGAJI MBWA TANZANIA (TCA)

PICHA:NYOKA AINA YA CHATU AUWAWA KANISANI BAADA YA KUKUTWA NYUMBANI KWA MFANYABIASHARA MAARUFU JIJINI ARUSHA AKISADIKIWA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA