- Get link
- Other Apps
NA BASHIR YAKUB -
Jirani yako au mtu mwingine yeyote amejenga na kuziba njia. Njia yoyote iwe kubwa kama barabara ama ndogo ambayo hata gari haiwezi kupita. Iwe tu kama ya pikipiki au baiskeli au hata ya miguu tu. Yote haya hayajalishi na hizi zote ni njia kwa mujibu wa sheria.
1.HAKI YA NJIA KISHERIA .
Kifungu cha 151 cha sheria namba 4 sheria ya ardhi ya mwaka 1999 kinaeleza haki hii. Kinaitambua haki hii kwa kusema kuwa haki ya njia ipo kwa njia zile ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya umma. Umma hapa humaanisha watu wote lakini pia wakazi wa eneo fulani wanaotumia njia hiyo kwa ajili ya shughuli zao mbalimbali.
Kifungu kimepanua matumizi ya njia ya umma kwa kumaanisha hata njia zilizotengwa kwa ajili ya makampuni binafsi. Kwa mfano kuna sehemu ukipita utaona njia au sehemu ya lami ya barabara imekatwa maalum kwa ajli ya kuruhusu watu au magari ya kampuni fulani kupata sehemu ya kuingilia.
Lakini pia zipo njia zimetengwa kwa ajili ya shughuli za serikali. Haraka utaona kuwa haki ya njia haijagusa tu kule mitaani wanakoishi watu tu bali hata sehemu za makampuni binafsi nk.
2. KUZIBA NJIA YA UMMA.
Kuziba njia ya umma ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 177( 4 ) cha sheria ya ardhi. Wako watu wakorofi huko mitaani huziba njia kwa makusudi. Yawezekana kabisa mtu akiwa anajua kabisa eneo fulani ni njia na watu hupita hapo lakini kwa makusudi au bila kujali akajenga ukuta au akaweka uzio wa sinyenge au akapanda mti pale au akaweka kifusi au kwa namna nyingine yoyote.
Na wengine huambiwa na watu lakini wasisikie kwasababu ya pesa, au urafiki na viongozi wa serikali au cheo au rushwa au vinginevyo. Basi yatupasa kujua kuwa watu hawa huwa wakitenda makosa na si wakunyamazia.
Njia kuzibwa si lazima iwe imezibwa yote. Hata kuibana na kuitoa katika uhalisia wake katika kiwango chochote nako ni kuziba njia. Njia yafaa iachwe vilevile ilivyo.
3. NINI UFANYE IKIWA NJIA IMEZIBWA.
Yako mambo mawili unaweza kufanya ikiwa mtu amewazibia njia. Moja ni jepesi na la pili sio jepesi. La kwanza ni kwenda mahakamani kwa kufungua malalamiko na pili ni kupeleka malalamiko kwa kamishna wa ardhi.
Kwenda mahakamani ni njia ambayo sio nyepesi sana. Ina gharama , na inapoteza muda zaidi. Na ikiwa utaamua kwenda mahakamani basi mahakama inayotumika katika mambo kama haya ni mahakama ya ardhi.
Baraza la ardhi la kata na la kijji ni sehemu ya mahakama za ardhi. Hata hivyo kama utaamua kwenda mahakamani ni vema zaidi ukaanza na mabaraza haya ya kata na kijiji.
Na uzuri mabaraza haya hayana gharama, na kesi haichukui mda mrefu. Ni tofauti na ukiamua kutumia baraza la ardhi la wilaya au mahakama kuu ya ardhi.
La pili ambalo sasa ni ndilo jepesi ni kupeleka malalamiko kwa kamishna wa ardhi . Kifungu cha 176 ( 1) kinasema kuwa kamishna wa ardhi ana mamlaka ya kutoa amri kuhusu njia iliyozibwa ikiwa ataridhika kuwa ni kweli njia imezibwa tena kimakosa.
Kwa hiyo badala ya kuhangaikia mambo mengine ni bora basi ukapeleka malalamiko yako kwa kamishna wa ardhi naye atatoa amri ambayo ni lazima kwa aliyeziba njia kuitekeleza.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE. 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
Comments