MANARA AAHIDI KUWA MWADILIFU BAADA YA KUFUTIWA ADHABU


Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ameahidi kufanya kazi hiyo kwa weledi, nidhamu na kuzingatia miiko ya mchezo wa soka, baada ya kufutiwa adhabu ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo, mtoto huyo wa nyota wa zamani wa Yanga, Sunday Manara ‘Computer’ amesema; “Nawaahidi kuendelea kufanya kazi zangu kwa weledi, nidhamu na kwa kuzingatia miiko ya mchezo huu, unaobeba dhamana za maisha ya watu walio wengi, sambamba na kuendelea kuitetea na kuilinda klabu yangu kwa nguvu zote,”.
Maneno ya Manara yanafuatia kufutiwa adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka leo na Kamati ya Nidhamu ya TFF, chini ya Mwenyekiti wake, Tarimba Gulam Abbas baada ya kuitumikia kwa karibu miezi mitatu tu.
Hajji Manara ameahidi kufanya kazi kwa uadilifu baada ya kufutiwa adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja na TFF

Mapema katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Tarimba amesema kwamba mbali na Manara aliyefungiwa Aprili mwaka huu, chini ya Kaimu Mwenyekiti wa zamani wa Kamati hiyo, Wakili Jerome Msemwa viongozi watatu wa Chama cha Soka Rukwa, James Makwinya, Blasi Kiondo na Ayoub Nyaulingo nao wamesamehewa baada ya wote kuomba marejeo ya kesi zao.
Pamoja na hayo, Tarimba amewasihi Wasemaji wa Klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Daraja la Kwanza kuzingatia miiko na maadili wakati wa kutoa taarifa zao.
Akiwa mwenye furaha, baada ya kufutiwa adhabu hiyo, Manara amesema; “Leo ni siku kubwa kwa mchezo wa mpira wa miguu nchini, hususan mashabiki na mchezo huo muruwa, baada ya kamati ya nidhamu kuitengua adhabu yangu ya kufungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya kandanda ndani na nje ya nchi,”. 
Manara amesema adhabu hiyo ilikuwa inaiumiza sana klabu yake na kuiondolea haki yake muhimu ya kuwapa habari kwa wakati Watanzania juu ya kinachoendelea kwenye klabu. 
“Kiukweli niishukuru kamati ya nidhamu chini ya Mwenyekiti wake, Tarimba Abbas kwa kuiondoa adhabu hii, kiukweli aliyeondolewa adhabu si Hajji, ni Simba na mchezo wenyewe wa Soka,”amesema. 
Hajji alifungiwa mwaka mmoja sambamba na faini ya Sh. Milioni 9 Aprili mwaka huu, baada ya kukutwa na hatia katika makosa matatu dhidi ya TFF waliomlalamikia, ambayo ni kuituhumu na kuidhalilisha TFF, kueneza chuki za ukabila na la tatu kuingilia utendaji wa shirikisho hilo.
Kosa la kwanza alihukumiwa kwa mujibu wa kanuni ya 41 kifungu cha tisa ambalo analipa faini ya Sh. Milioni 1, la pili alihukumiwa kwa kanuni ya 53 kifungu cha kwanza na cha pili na anafungiwa miezi mitatu na faini ya Sh. Milioni 3 na kosa la tatu alihukumiwa kwa kanuni ya kwanza na ya pili inayohusu Maadili, ambayo alitakiwa afungiwe miaka saba na faini ya Sh. Milioni 5.
Lakini kutokana na kwamba hilo lilikuwa kosa lake la kwanza, Kamati ilitumia mamlaka yake kwa kumpunguzia adhabu hadi miezi 12 na faini ya Sh. Milioni 5 – na adhabu hizo ziliunganishwa, hivyo akatakiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh. Milioni 9
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MATOKEO YA KIDATO CHA PILI, DARASA LA SABA YATANGAZWA ZANZIBAR

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

ZAIDI YA WANANCHI 500 KUSHIRIKI MAFUNZO YA MKIKITA YA KILIMO CHA PAPAI SALAMA

MKIKITA YATOA OFA KWA KILA HEKA YA PAPAI SH. MIL. 2 KUTANDAZA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI

DIAMOND AITWA NA NYOTA YAJAA GOMS

WATEJA WA NSSF DAR WATIMULIWA KWA MTUTU WA BUNDUKI

MATOKEO YA DARASA LA SABA YATANGAZWA

KAMISHNA MARIJANI AZINDUA CHAMA CHA WAFUGAJI MBWA TANZANIA (TCA)