Serikali
imeona umuhimu wa kuingiza elimu ya mlipa kodi kwenye mitaala ya elimu
nchini ili kwajengea Watanzania tabia, mwenendo na mazoea ya kulipa kodi
kwa maendeleo ya Taifa.
Kauli
hiyo imetolewa leo, Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu
Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Lupembe Mhe. Joram Ismael Hongoli juu ya kwa nini Serikali
isiingize kwenye mitaala ya elimu somo la umuhimu wa kulipa kodi ili
lifundishwe kuanzia shule ya msingi ili wananchi wapate uelewa wa kodi
na waweze kulipa kodi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea.
"Serikali
inatambua umuhimu wa elimu ya mlipa kodi katika kumjengea mwananchi
tabia ya kulipa kodi. Katika somo la Uraia na Maadili kuanzia darasa la
III na kuendelea, mtaala umelenga kumjengea na kumuandaa mwanafunzi kuwa
mwajibikaji katika kutekeleza majukumu ya kila siku," alisema Mhe. Ole
Nasha.
Vile
vile mtaala umelenga kumjengea mwanafunzi kuiheshimu na kuithamini jamii
yake kwa kuwa mwadilifu na mzalendo ikiwa ni pamoja na kutekeleza
majukumu ya kitaifa ikiwemo kulipa kodi.
Aidha
amesema, kutokana na umuhimu wa kuwajengea vijana utamaduni wa kulipa
kodi, elimu ya mlipa kodi ni jambo muhimu, Serikali kupitia Taasisi ya
Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikisha Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA)
itaendelea kuboresha elimu hiyo ili isisitizwe na kuwekewa mkazo katika
mitaala ya elimu kuanzia elimu ya Msingi.
Wakati
huo huo, Mhe. Ole Nasha amesema Serikali ilifuta ada na michango ya
lazima katika shule za umma ngazi ya elimu ya msingi (elimu ya awali
hadi kidato cha Nne) na mpango huo hakuhusisha kidato cha tano na sita
pamoja na shule binafsi.
Ameyasema
hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Seter
Alexander Mahawe juu ya lini, Serikali itafuta ada kwa wanafunzi
wanaosoma katika shule binafsi.
"Ada
na michango iliyokuwa inalipwa na wazazi/walezi kwa sasa hugharamiwa na
Serikali. Mpango huu haukuzihusu shule binafsi pamoja na shule za Umma
ngazi ya kidato cha Tano na Sita. Hivyo shule hizo zitaendelea na
utaratibu wa wazazi/walezi kuchangia gharama za uendeshaji wa elimu
ikiwemo kulipa ada za mitihani.
Hata
hivyo amesema, Ili kuhakikisha mazingira rafiki katika utoaji wa elimu,
Serikali imekuwa ikifanya majadiliano na sekta binafsi kwa lengo la
kuondoa changamoto zinazowakabili ambapo hadi sasa Serikali imeweza
kuondoa baadhi ya kodi na tozo mbalimbali ambazo awali walikuwa
wakitozwa wamiliki wa shule binafsi.
Ametoa
mfano wa kodi hizo kuwa ni kodi za mabango, kodi ya kuendeleza ufundi
standi stadi (Skills Developmentt Levy), tozo ya Afya na Usalama mahala
pa kazi (Occupational Safety and Health Administration - OSHA) na tozo
ya zimamoto.
Comments