Tanzania yakanusha tuhuma za kukandamiza haki za Wamaasai


Mfugaji Parakapooni na ndugu yake na mwanawe Serengeti, Tanzania.
Tanzania imekanusha ripoti mpya inayoishutumu serikali ya Tanzania na baadhi ya kampuni za kitalii na uwindaji kwa kuendelezwa kwa vitendo vya unyanyaswaji na ukiukwaji wa haki za binaadamu kwa watu wa jamii ya Kimaasai wanaoishi katika baadhi ya vijiji wilayani Loliondo.
Serikali ya Tanzania inasema tuhuma hizo ni "potofu" na kwamba zina lengo la kuipaka matope serikali ya Tanzania.
Katika ripoti hiyo, taasisi ya Oakland inadai kwamba, ukiukwaji huu wa haki za binaadamu unahusiana na mgogoro wa ardhi ambao umekuwepo kwa miaka mingi kati ya watu wa Jamii ya Kimaasai wanaopigania urithi wa ardhi yao na serikali kwa upande wingine inayodai kutaka kutunza ardhi hiyo kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.
Ripoti hiyo yenye kurasa zaidi ya arobaini imesheheni shuhuda za watu wa jamii ya Wamaasai wanaoishi katika ardhi hiyo inayopiganiwa.
Watu hao wamewaambia watafiti wa ripoti hiyo kwamba serikali ya Tanzania imekuwa ikitumia sheria za uhifadhi kuwatoa kwa nguvu katika ardhi ya urithi kutoka kwa mababu zao.
Wameongeza pia kwamba, kampuni hizo za kitalii na uwindaji zimekuwa zikiwazuia kutumia vyanzo muhimu vya maji na kushutumu kampuni hizo kutumia polisi kuwapiga na kuwakamata
Awali, kampuni mojawapo inayoshutumiwa iliwahi kuiambia BBC kwamba, wakati pekee ambao jamii hizi zinazuiliwa kuingia katika maeneo ya uwindaji kufikia vyanzo vya maji ni miezi kati ya Julai na Desemba ambao ni msimu wa uwindaji - kitu ambacho ni msimu wa upungufu wa maji pia.
Serikali kwa upande wake imekuwa ikikataa kuhusika na unyanyasaji wowote ule wa jamii hizi za Wamasai na kudai kwamba sheria za uhifadhi zilizopo zinalenga kutunza na kuendeleza tu maeneo ya uhifadhi na viumbe vilivyomo ndani ya maeneo hayo
Wamasai wakataa kuondoka katika ardhi ya Serengeti Tanzania
Mwishoni mwa mwaka jana serikali ilikatisha mkataba wa ruhusa ya uwindaji wa takribani miaka 25 wa kampuni ya OBC huku waziri wa Maliasili na Utalii Hamis Kigwangala akiamuru uchunguzi ufanyike juu ya utendaji wa kampuni hiyo.
Kwa takribani miaka sita sasa, sekta ya utalii imekuwa ndio chanzo kikubwa zaidi cha fedha za kigeni kwa Tanzania, huku ikikadiriwa kwamba sekta hiyo inaiingizia nchi kiasi cha Dola Bilioni 2 za Kimarekani kila mwaka.

Serikali ya Tanzania imesema nini?

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangalla amesema kupitia taarifa kwamba Watanzania na jamii ya kimataifa wanafaa "kupuuza taarifa hiyo potofu yenye lengo la kuipaka matope serikali na kuleta uchonganishi baina yake, wananchi na wawekezaji kwa lengo la kuleta uvunjifu wa amani."
Amesema kutokana na umuhimu wa eneo hilo kwa uhifadhi, uwepo wa vyanzo vya maji, eneo la mzunguko wa uhamiaji wa wanyamapori na maisha ya watu, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilichukua hatua stahiki za kutatua mzozo huo.
Dkt Kigwangalla amesema serikali ilichukua hatua hizo ikihusisha wadau wote muhimu yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, wawekezaji pamoja na wananchi.
"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wenye nia njema kwa uhifadhi na maendeleo ya wananchi katika kusimamia na kuendeleza rasilimali zilizopo katika eneo la Loliondo na maeneo mengine nchini kwa maslahi mapana ya Taifa," amesema waziri huyo.


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.