TBN YAANZA KAMPENI YA KUSAMBAZA TAARIFA CHANYA


Yaungana na PSSSF kuongeza elimu ya hifadhi ya jamii

Msimbe: Mafanikio ya Taifa yasizidiwe na habari za udaku

Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) umetangaza mpango mkakati wa kutumia nguvu ya majukwaa ya kidijitali ya wanachama wake zaidi ya 200 kusambaza kwa kasi taarifa sahihi na chanya kuhusu maendeleo ya Tanzania, huku ukitaka mafanikio ya Taifa yapewe nafasi kubwa katika ulimwengu wa habari za mtandaoni.

Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, amesema wakati umefika kwa taasisi za umma, binafsi na wadau wa habari kushirikiana kubadili mwelekeo wa maudhui yanayotawala mitandao ya kijamii, ili taarifa za maendeleo, uchumi, huduma za jamii na mafanikio ya Taifa zifikie wananchi kwa wingi zaidi.

Msimbe aliyasema hayo wakati wa mkutano kati ya viongozi wa TBN na ujumbe kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), uliofanyika Makao Makuu ya TBN, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Alisema kasi ya maendeleo ya teknolojia, ikiwemo akili unde, imefanya taarifa kutafutwa, kuzalishwa na kusambazwa kwa kasi kubwa, hivyo Tanzania inapaswa kutumia fursa hiyo kuhakikisha taarifa muhimu kuhusu maendeleo yake zinafika ndani na nje ya nchi.

“Ni jambo la kusikitisha kuona taarifa zinazoongoza katika mifumo ya habari za kidijitali na kusambaa duniani kote kuhusu Tanzania mara nyingi ni zile zinazotokana na matukio ya udaku mitandaoni, badala ya habari muhimu za maendeleo,” alisema.

Msimbe alitoa mfano wa uzinduzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, akisema licha ya kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa kwa uchumi na maendeleo ya Taifa, baadhi ya taarifa zilizopata umaarufu zaidi mtandaoni wakati huo zilihusu maisha binafsi ya wasanii na mastaa.

Alisema hali hiyo ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa taasisi za serikali, sekta binafsi na wadau wa habari katika kuhakikisha mafanikio ya Tanzania yanapata mwonekano unaostahili katika majukwaa ya kidijitali.

“TBN ipo tayari kushirikiana na taasisi mbalimbali kuongeza wingi wa taarifa chanya katika mifumo ya habari za kidijitali. Tunapaswa kuhakikisha Tanzania haitambuliki kwa habari zinazohusu maisha binafsi ya watu pekee, bali pia kwa mafanikio yake makubwa ya kiuchumi na kijamii,” alisema.

TBN, PSSSF KUUNGANISHA NGUVU

Msimbe pia alieleza kufurahishwa na dhamira ya PSSSF kushirikiana na TBN katika kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu hifadhi ya jamii, mifumo ya pensheni na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo.

Alisema TBN ina mtandao mpana wa wanachama zaidi ya 200 waliopo ndani na nje ya Tanzania, jambo linalouwezesha mfuko huo kutumia majukwaa mbalimbali ya kidijitali kuwafikia wananchi kwa wakati.

“Tupo tayari kutumia uwezo, uzoefu na wigo mpana wa majukwaa ya wanachama wetu kutoa elimu sahihi kuhusu shughuli, huduma, uwekezaji na mifumo mbalimbali inayosimamiwa na PSSSF,” alisema.

Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo una historia kubwa katika kukuza habari za kidijitali nchini na unajivunia kuwa na wanachama wenye weledi, uzoefu na uwezo wa kuwafikia wananchi kupitia majukwaa mbalimbali.

Michuzi alisema TBN ilianzishwa kwa dhamira ya kuchangia ujenzi wa taswira nzuri ya Tanzania katika medani za kidijitali kupitia taarifa sahihi, zenye manufaa na zinazochochea maendeleo.

“TBN ipo tayari kushirikiana na PSSSF kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wananchi kwa lugha nyepesi, sahihi na inayoeleweka kupitia majukwaa ya kidijitali,” alisema.


Kwa upande wake, Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema mtandao huo utatumia waandishi wake mahiri pamoja na majukwaa ya wanachama kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zinazoaminika kuhusu hifadhi ya jamii.

Alisema elimu hiyo itawasaidia wananchi kuelewa haki na wajibu wao pamoja na fursa zinazopatikana kupitia mifumo ya hifadhi ya jamii.

Pallangyo alisema ushirikiano huo unaweza kuwa daraja muhimu kati ya PSSSF na wananchi, hasa wakati ambapo majukwaa ya kidijitali yamekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya habari, elimu na maarifa.

PSSSF YATOA AHADI

Akizungumza kwa niaba ya PSSSF, Mkuu wa Msafara, Abdul Njaidi, alisema ziara hiyo ilikuwa sehemu ya jitihada za mfuko kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya habari na kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii.

Njaidi aliwahakikishia viongozi wa TBN kuwa maombi, mapendekezo na hoja zilizowasilishwa katika mkutano huo zitafanyiwa kazi.

Alisema PSSSF inalenga kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu masuala ya pensheni, hifadhi ya jamii na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo kwa manufaa ya wanachama na Taifa kwa ujumla.

Ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Njaidi na kuwajumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo.

Kwa upande wa TBN, mkutano huo ulihudhuriwa na Beda Msimbe, Rahel Pallangyo, Cathbert Kajuna na Issa Michuzi.


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

OWM–TAMISEMI YASHINDA TUZO YA MABADILIKO YA KIDIJITALI KATIKA TEHAMA AWARDS 2026

MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA KUAPISHWA NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS

MAFAO YA MAKAMU WA RAIS ALIYEJIUZULU

NI MAKOSA WANAFUNZI KUFIKA SHULE SAA 1:15 ASUBUHI

URUSI, CHINA, IRANI NA KOREA KASKAZINI WAPANGA KUUNDA JESHI MOJA LA KUJIHAMI

PANYA MAGAWA WA SUA TANZANIA AJENGEWA MNARA WA HESHIMA CAMBODIA