NMB YATOA MSAADA WA PIKIPIKI 20 ZA SH. MIL. 65 ARUSHA



Na Mwandishi Wetu, Arusha

 

Benki ya NMB imekabidhi pikipiki 20 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 65 zitakazosaidia kuimarisha ulinzi mkoani Arusha.

 

Mchango huo ambao umetolewa kwa Jeshi la Polisi mkoani humo unaendana na mpango mkakati wa benki hiyo wa kuendeleza sekta ya utalii unaolenga kuimarisha mifumo endelevu ya ikolojia ya utalii. 

 

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya pikipiki hizo ambayo ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda iliyofanyika katika Tawi la NMB Clock Tower jijini Arusha jana, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki ya NMB, Filbert Mponzi alisisitiza dhamira ya benki hiyo kuendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wote ikiwemo Serikali kusaidia maendeleo ya sekta ya utalii.

 

“Kwetu mkoa wa Arusha ni muhimu na ni wakimkakati kwa kuwa ni kitovu cha watalii ndomana leo tupo mahali hapa kukabidhi pikipiki 20 ili kuimarisha usalama. Kama benki, tunaamini kwamba usalama ukiimarishwa, sekta ya utalii itastawi kwa kiwango kikubwa,” alisemaa

 

Mponzi alionyesha matumaini kuwa juhudi za benki hiyo mkoani Arusha zitakuwa na athari kubwa zaidi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii nchini kote.

 

"Juhudi zetu zitakuwa chachu ya ukuaji wa sekta ya utalii kwa ujumla. Tunaamini kuwa watalii wakiwa salama hapa Arusha kama kitovu cha utalii, basi watakuwa tayari kwenda kufurahia maeneo utali katika maeneo mengine nchini kama vile Zanzibar,” Mponzi alisisitiza. 

 

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Wazawa nchini Samuel Diah wakati wa hafla hiyo aliipongeza Benki ya NMB kwa mchango huo akionyesha imani kuwa kwa kiasi kikubwa utachochea ukuaji wa sekta ya utalii mkoani humo.

 

“Kwa kweli mchango huu umekuja wakati muafaka kwani kuhakikisha usalama wa watalii wa ndani na nje ni kipaumbele kikuu kwetu kwa sasa. Juhudi za Benki ya NMB zitahakikisha usalama wa mkoa wa Arusha wakati wote na vile utachangia juhudi za Serikali ya awamu ya sita za kukuza sekta ya utalii,” alisema Diah.

 

Aliongeza, “Usalama ndio kivutio kikubwa kwa watalii wote. Pamoja na mkoa wa Arusha kuwa na vivutio vingi vya utalii, hatuwezi kuvutia watalii wengi kama mkoa hauko salama,”

 

Dia alitumia hafla hiyo kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kuanzisha kampeni ya kuliwezesha jeshi la polisi kwa kutumia pikipiki, huku akisisitiza kuwa mpango huo hatimaye utaongeza ufanisi wa jeshi hilo katika utoaji wa huduma. 

 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda wakati wa hafla hiyo alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele katika kutangaza vivutio vya kipekee vya Tanzania na kuwataka wananchi kulinda vivutio hivyo vya utalii.

 

"Hili ni tukio la kihistoria na hakika ni ishara ya kurudisha kwa jamii. Wananchi wanatakiwa kusaidia makampuni yanayowajibika kama Benki ya NMB,” alisema.

 

Makonda aliongeza, “Pikipiki ambazo zimetolewa leo hazitasaidia jeshi la polisi bali jamii nzima ya mkoa wa Arusha kwani zitasaidia kuimarisha ulinzi na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.

 

Katika hafla hiyo, alitoa wito kwa wakazi wote wa mkoa wa Arusha kuendela kushirikiana kwa karibu na jeshi la polisi kwa kuwabaini wahalifu wote mkoani humo


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

BALOZI NCHIMBI AONGOZA MAPOKEZI YA KATIBU MKUU, MGOMBEA URAIS WA FRELIMO

WAZIRI WA FEDHA AWASILISHA BAJETI YA 2024/2025

DKT NCHIMBI AUNGURUMA KILIMANJARO

PROF NDAKIDEMI AITAKA SERIKALI KUPELEKA VIFAA TIBA URU KUSINI

WANANCHI KIBOSHO WAIOMBA SERIKALI KUWAJENGEA VIVUKO VYA KUDUMU

VIONGOZI WA DINI, ASASI WAJITOKEZA KUTOA MAONI UBORESHAJI KANUNI ZA UCHAGUZI

BALOZI NCHIMBI ATINGA BUNGENI KUSIKILIZA UWASILISHWAJI WA BAJETI

TAMISEMI HAIVUNJI SHERIA KUANDAA KANUNI ZA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA