Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 18, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
1. MAFANIKIO NA MUELEKEO WA TBS
KATIKA MIAKA MINNE YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA
Kipindi
cha miaka minne (2021-2024) ya Serikali ya awamu ya Sita, kimekuwa cha
mafanikio makubwa kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika utekelezaji wa
majukumu yake. Mafanikio hayo yameendelea kutimiza azma ya Shirika katika masuala
mbalimbali ili kutimiza matamanio ya wadau na Taifa kwa ujumla kama ifuatavyo:
a)
Kusogeza Huduma Karibu na Wateja
Katika
kutekeleza azma ya Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa ukaribu na
kupunguza gharama, Shirika limeanza ujenzi wa maabara katika mikoa
ya kimkakati ya Dodoma na Mwanza.
Kwa upande wa Dodoma, maabara zitakazojengwa zitahudumia mikoa mitatu ya Kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora pamoja na mikoa mingine ya karibu. Aidha, maabara za Mwanza zinatarajiwa kuhudumia mikoa sita, ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu. Pia Shirika limeshapata Mshauri Mwelekezi (Consultant) wa kuchora michoro ya jengo pamoja na kusimamia ujenzi wa maabara na ofisi jijini Arusha. Hatua hiyo ya ujenzi wa maabara itasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa majibu ya vipimo vya sampuli.
Shirika
limetenga kiasi cha TZS bilioni 2.7 kwa ajili ya kuimarisha ofisi saba za kanda
(Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma na Mbeya) pamoja na
ofisi za mipakani (Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili, Tarakea, Namanga,
Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro, Sirari, Kabanga, Rusumo, Mutukula, Bandari ya Bagamoyo, bandari ya
Mbweni, bandari ya Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Kambarage Nyerere – Dar es Salaam na Bandari ya Tanga) kwa kuongeza wafanyakazi
na vitendea kazi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakati na kuimarisha zoezi la
ukaguzi wa mara kwa mara sokoni ili kupunguza bidhaa hafifu sokoni na hatimaye
kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama.
a)
Kuwezesha Biashara
Shirika lina Kamati za Kitaalam (Technical Commitees) za Uandaaji Viwango 115 katika sekta ya chakula, kemikali, uhandisi mitambo, uhandisi umeme, uhandisi ujenzi, nguo na ngozi, madini na mitambo ya uchimbaji madini, mazingira na mtambuka (general tecniques). Katika mchakato wa kuandaa viwango Kamati hizo zinashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu, taasisi za utafiti, wafanyabiashara, wazalishaji, vyama vya walaji, vyama na bodi za wataalam, taasisi za udhibiti na watunga sera. Kwa kipindi cha miaka minne Shirika limefanikiwa kuandaa viwango 1,823 vya sekta mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya soko ambavyo vitasaidia wafanyabiashara, wajasiriamali na watoa huduma kuzalisha bidhaa bora zenye kukidhi matakwa ya viwango, hivyo kuwawezesha kufanya biashara ndani na nje ya nchi, hatua ambayo italeta tija na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha,
jumla ya vyeti na leseni za ubora 2,402 vimetolewa
kwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali
wadogo 1,066. Serikali kupitia TBS imekuwa
ikitenga zaidi ya sh. milioni 350 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia
wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote. Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuweza
kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na
pia kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji
wa uchumi wa Taifa.
Katika
kipindi cha miaka minne, Shirika limeendelea na huduma za usajili wa maeneo ya
uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula na vipodozi kwa lengo la
kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji
ambapo jumla ya maeneo 31,592 yalisajiliwa.
Pia, katika kuimarisha ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazoingia nchini kutoka nchi za nje, TBS huhakiki ubora wa bidhaa na magari yaliyotumika kabla ya kusafirishwa kuja nchini ambapo kwa kipindi cha miaka minne, jumla ya shehena za bidhaa 18,588 zilikaguliwa, sanjari na magari 162,160. Bidhaa hizi
zinakaguliwa
kwa lengo la kuiepusha Tanzania kuwa
jalala la bidhaa duni pamoja na kulinda afya, usalama na mazingira ya
watumiaji.
Kwa
upande wa mafunzo, TBS imeweza kutoa mafunzo kwa jumla ya wadau 5,052
wakiwemo wazalishaji
wa bidhaa za viwandani na wasindikaji. Mafunzo hayo yalihusu dhana nzima ya
viwango na ubora ambayo yatawawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi
matakwa ya viwango na yamewawezesha kupata uelewa mpana kwenye masuala ya udhibiti
ubora, hivyo kuwaandaa kuhimili ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na
kimataifa. Pia kupitia Mradi wa Qualitan TBS na SIDO mwaka 2024
waliwezeshwa kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa za chakula 1000 katika
mikoa 10 (Dar es Salaam, Singida, Mwanza, Geita, Kagera, Kigoma, Shinyanga, Tanga,
Ruvuma na Kilimanjaro)
Vilevile,
TBS imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kukuza uelewa
juu ya masuala ya viwango na udhibiti ubora. Njia hizo ni pamoja
na kushiriki katika makongamano, maonesho, warsha na semina; kuandaa
mikutano na wadau wa masuala ya viwango, kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu
masuala ya ubora na usalama; na kuendesha kampeni za elimu kwa umma katika
ngazi za wilaya. Aidha, elimu imekuwa ikitolewa kupitia vyombo vya habari zikiwemo
redio jamii, redio za kitaifa, runinga, magazeti, mitandao ya kijamii,
matangazo, majarida na vipeperushi.
a)
Kuongeza Ufanisi wa Maabara
TBS
ina jumla ya maabara 12 na zote zimeweza kupata ithibati za umahiri,
ambapo maabara hizo zimehakikiwa na kupatiwa vyeti vya ithibati ya umahiri wa
kimataifa. Hatua hiyo inamaanisha kuwa majibu ya sampuli kutoka katika maabara
hizo yanaaminika kokote duniani na hivyo kurahisisha biashara ndani na nje ya
mipaka ya nchi yetu. Katika kipindi hicho TBS imeweza kupima sampuli zaidi ya ya
118,059 na kufanyia ugezi vifaa 36,808
ambapo suala hili litasaidia kuhakikisha katika soko kunakuwa
na bidhaa zenye ubora.
Maabara za TBS zina mashine za kisasa (state-of
-art-equipment) zinazopelekea kupata majibu kwa wakati na sahihi, pamoja
na mashine nyingi zilizopo katika maabara hizo, kuna mashine za kipekee kama
ifuatavyo;
i)
Mashine ya hydrostatic pressure test ya kupima
mabomba ya maji na yenye uwezo wa kupima mabomba yenye kipenyo cha milimita 12
sawa na inch 0.5 hadi milimita 800 sawa na inchi 32. Mashine hii ina uwezo pia
wa kupima sampuli 120 kwa wakati mmoja na kati
ya nchi 54 za Barani Afrika inapatikana katika nchi tano tu ikiwemo Tanzania;
ii) Mashine
ya automatic conductor resistance tester ya kupimia waya (cables)
za umeme za aina zote zenye kipenyo hadi kufikia milimita 40 sawa na milimita
za mraba1200. Mashine hii ni ya kipekee kwa kuwa ni ya kidigitali na ina uwezo
wa kupima na kutoa majibu kwa haraka;
a)
Kuimarisha Mifumo ya TEHAMA
Shirika linatumia mifumo ya
TEHAMA katika utoaji wa huduma zake mbalimbali kama vile leseni ya ubora,
ukaguzi wa shehena zinazotoka nje ya nchi na usajili wa bidhaa za chakula na
vipodozi, majengo, maeneo ya uzalishaji, uuzaji, vyombo vya usambazaji wa
bidhaa za chakula na vipodozi. Mifumo hiyo ni OAS na i-SQMT. Aidha, Shirika
limeboresha huduma zake kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini kwa
kuunganisha mfumo wake unaoitwa Online
Application System na mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Tanzania electronic
Single Window System – TeSWS) ambapo mfanyabiashara anatuma maombi na
anapata huduma za taasisi zote na kibali kupitia mfumo huo.
b)
Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya
Kupikia
TBS inatambua na kusifu juhudi za Serikali
katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi, kupunguza athari za mabadiliko ya
tabianchi, na kutunza mazingira huku ikiokoa maisha kupitia suluhisho endelevu
la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.TBS ina jukumu muhimu kama taasisi ya
viwango nchini katika kuhakikisha utekelezaji wa viwango vya kitaifa vya
nishati unasaidia kufanikisha malengo hayo.TBS inashirikiana na
washirika wa maendeleo na Wizara ya Nishati kuandaa
viwango vya ufanisi wa nishati kwa vifaa vya umeme vya majumbani. Vilevile
vifaa vya Maabara vya kisasa vinaendelea kununuliwa kwa ajili ya kuhakikisha
vifaa vinavyoingia sokoni vinakidhi viwango vilivyowekwa kabla ya kuwafikia watumiaji.
Hatua hii inalenga kupunguza uzalishaji wa gesi joto, kupunguza upotevu wa
nishati, na hivyo kupunguza gharama kwa watumiaji.
a) Tuzo na Umahiri
Mnamo
mwaka 2023, TBS ilipata mafanikio makubwa kwa kushinda Tuzo ya kuwa Mdhibiti
Bora Barani Afrika kwa Mwaka 2023. Tuzo hii inaonesha dhamira ya TBS katika
utendaji bora na mchango wake chanya katika kukuza viwango na kudhibiti ubora.
Vilevile,
TBS imekuwa taasisi ya kwanza katika Jumuiya ya Nchi za Kusini
mwa Afrika
(SADC) kupata ithibati (accreditation) ya mifumo ya udhibiti ubora wa bidhaa
(Product Certification) ya kimataifa katika wigo
mpana (wide scope) ndani ya muda mfupi na ni ya taasisi ya tatu kupata
ithibati hiyo iliyotolewa na SADCAS Septemba, 2024 hivyo kufanya mifumo
hiyo kutambulika kimataifa.
Comments