Kuridhika kwa ngono ni hisia ya kibinafsi ambayo ni ngumu kuelezeka, na inategemea uzoefu wa mtu mwenyewe na uhusiano alionao.
Wanandoa wana mawazo tofauti kuhusu maisha yao ya ngono.
Badala ya kufafanua namna ya kufurahia ngono kwa kuzingatia ni mara ngapi unashiriki tendo la ndoa, itakuwa muhimu zaidi kuwa na uhusiano wa kihisia.
Mtaalamu wa masuala ya ngono na mwandishi wa vitabu viwili kuhusu ushiriki wa ngono vinavyouzwa sana, ambaye pia anatambuliwa katika ushauri wa masuala ya mapenzi Dk. Emily Nagoski alizungumza na BBC Mundo kuhusu suala hili.
"Mara nyingi wanandoa huenda kwa daktari kwa sababu matamanio ya kuonana kimwili na uhusiano wao haviendani," anasema Dk. Emily Nagoski.
Kulingana na yeye, baada ya kuzungumza na mamia ya wanandoa na kusikiliza maelezo ya uzoefu wao wa ngono, alishtuka kwa sababu wanandoa wengi hushiriki mapenzi kwa sababu ya kile ambacho watu wengine watasema.
Matatizo wakati wa kujamiiana
Alisema kuwa watu wengi wanaishi maisha ya unyumba bila kuchunguza kile kinachowasisimua, kinachowaridhisha, au mambo mengine yanayohusiana na kufanya mapenzi.
"Wanaelezea ngono kama wajibu wao na kuhisi kuwa tendo la ndoa hufanyika kulingana na sheria ambazo lazima zifuatwe."
Niliwafafanulia kwamba ikiwa hutaki kushiriki ngono katika uhusiano wako, sio kwamba 'una matatizo'.
"Ngono inapaswa kuwa kitu unachoweza kucheza nacho, kukufurahisha, na haupaswi kuhisi shinikizo kufanya tendo hilo."
Namna ya kuamua jinsi maisha yako ya ngono yalivyo
"Data kutoka kwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kupungua kwa mara ambazo wanandoa wanafanya tendo la ndoa," anasema Nagoski.
"Lakini, mojawapo ya mawazo niliyoyapa kipau mbele ni kwamba kuangalia ni mara ngapi tunafanya ngono sio njia nzuri ya kuamua kama maisha yetu ya ndoa yanakwenda vizuri au la."
"Hebu fikiria, wanandoa wanaofanya mapenzi mara kwa mara, lakini mmoja wao hafurahii, ungependelea hali hiyo au wanandoa ambao hawafanyi mapenzi mara kwa mara lakini wanapofanya, wote wawili hufurahia mno?"
"Chaguo la pili ndio zuri zaidi. Ndiyo maana hatupaswi kutumia ni mara ngapi kama kiashirio kikuu au hatua ya kuridhika au utimilifu wa kufurahia ngono."
"Kuna imani kwamba kufanya ngono au kufika kileleni wakati fulani ni muhimu kwa maisha ya ngono yenye mafanikio."
"Hii inaweka shinikizo kubwa kwa wanandoa na matokeo yake, hamu yao ya kufanya ngono inapungua?" alisema hivyo akijibu swali alilokuwa ameulizwa.
Anaendelea kusema, "Kwa kuongezea, kuna imani nyingi za kitamaduni juu ya ni mara ngapi unapaswa kushiriki ngono au kufika kileleni."
Kuna kisa cha wanandoa ambao waliamua kufanya ngono mara fulani kwa wiki. Kwa sababu walikuwa wamesoma mahali kwamba wastani huu ulikuwa sahihi. Walihisi kwamba kwa kufanya hivi, hakuna mmoja wao ambaye angeweza kusema kwamba hawakujaribu.
Tatizo ni kwamba walifanya hivi kama wajibu wao zaidi badala ya kuchukulia tendo la ndoa kama hamu yao ya kweli waliodhamiria kutimiza. Matokeo yake ni kwamba ingawa walirudia kufanya tendo la ndoa mara kwa mara, haikuleta mabadiliko yoyote katika furaha kwenye uhusiano wao.
Hatimaye, mpenzi wa kike alikasirika na uhusiano wao ukavunjika.
Hii inaonyesha kuwa sio tu ni mara ngapi, lakini jinsi ambavyo kila mmoja anaridhika ndio muhimu sana.
Sifa za wanandoa wenye uhusiano mzuri katika tendo la ndoa
"Ulisema kwamba ngono inapaswa kuwa jambo la kufurahia. Usiiangalie kama wajibu ambao ni lazima utimize. Tunawezaje kuwa na mtazamo ulio huru na wenye kufurahisha zaidi katika hili?", Alipoulizwa swali hili alisema:
"Niligundua kuwa wanandoa ambao wana uhusiano wa kimapenzi wenye nguvu wana sifa tatu zinazofanana.
Kwanza, wanapendana sana. Ni wazi kwamba wanaheshimiana na wanafurahia wanapokuwa pamoja. "Kuchukua jukumu la kupenda na kuheshimu kunaongeza sana ubora wa ngono na kulichukuliwa kuwa tendo la thamani."
"Pili, wanatanguliza ngono au uhusiano wa kimapenzi. Wanaelewa kuwa hii inaongeza kitu cha thamani na cha kipekee kwenye uhusiano wao."
"Hata kama wana muda mchache kufanya majukumu mengine, huwa wanajaribu kuhakikisha wametafuta muda kidogo kwa ajili ya kushiriki tendo la ndoa. Kwa sababu wanatambua umuhimu wake."
"Tatu, ninachokiona kigumu zaidi ni kuondokana na sheria za jinsi ngono inapaswa kuwa kwa misingi ya tamaduni, familia, au dini, na kujaribu kutafuta namna ambayo itakuwa inawafaa nyinyi."
"Mara nyingi hii ina maana ya kufikiria upya imani zenye kuzunguka ushiriki wa tendo la ndoa na kujifunza kuwasilisha matamanio na mapungufu yenu," aliongeza.
"Lakini unapochambua wanandoa ambao wanaelezea maisha yao ya ngono kama yenye kufurahisha, utagundua kuwa mara nyingi huwa wanazungumzia suala hii kama jambo la kawaida."
Anaendelea kusema, "Ni kama wanazungumza kile wanachopenda kufanya pamoja. Wanapenda kukumbuka walichofanya. Wanafikiria juu ya kile watakachofanya wakati mwingine."
"Lakini, kuna hofu mara mbili: kwanza, kumwambia mpenzi wako jambo ambalo litamshtua na kuhofia kwamba atabadilisha mtazamo wake juu yako ; na pili, kuumiza hisia zake."
Katika mahojiano na mtaalamu wetu, alisema mawasiliano ni muhimu sana. "Ni kawaida kuwa na hofu kwamba ikiwa unachotafuta ni kikubwa zaidi, kinaweza kisitimie," amesema "Ndiyo maana ninayaita 'mazungumzo juu ya mazungumzo.'"
Matatizo ya mawasiliano kuhusu maisha ya ngono
Nagoski anaamini kuwa wanandoa kufanya mazungumzo juu ya tendo lao la ndoa, hupunguza hofu ya pande zote mbili na inawasaidia kuacha kuona ngono kama mwiko au mada ambayo mtu hatakiwi kuizungumzia.
Anaongeza kuwa, "Uchungu na raha vyote hutokea kwenye ubongo. Haitokei tu katika homoni. Kwa mfano, ikiwa unatoroka simba na ukakatika kwenye mkono, ubongo wako unaweza kupuuza maumivu ya kwenye mkono. Inaona tishio kutoka kwa simba kama hatari zaidi na inaweza kukataa kuhisi maumivu ya kwenye mkono hadi utakapohakikisha kwamba sasa uko salama. Inategemea jinsi ubongo wako unavyotafsiri hisia katika muktadha uliopo."
"Vile vile, wakati mwanamke amejifungua akiwa amepitia tajriba mbaya, licha ya kupona kimwili, bado anapata uchungu wakati wa kuanza tena maisha yake ya ngono, inaweza kuwa mfumo wake wa neva bado uko katika "hali ya tahadhari," na unachukulia kusisimka kama tishio." Nagoski alisema.
Anaongeza zaidi, "Ningependa kusisitiza kwamba kufanya mapenzi kamwe hakupaswi kuwa uchungu; ikiwa unahisi hivyo, unapaswa kutafuta ushauri wa matibabu."
Jinsi ya kuboresha maisha ya ngono?
Mshauri wetu juu ya masuala ya ngono Bi. Nagoski ana hili la kusema kwa wale ambao wanataka kuboresha maisha yao ya ngono.
"Jielewe na ujue unachopenda na usichokipenda. Pia mwombe mwenzako afanye vivyo hivyo."
Kila mtu na kila mwili hubadilika kwa wakati. "Kilichofanyika hapo awali, kinaweza kisiwezekane sasa."
Anaendelea kusema, "Wasiliana kwa uwazi na utengeneze uhusiano ambao unahisi salama. Ikiwa ubongo wako utatafsiri kama tishio, itakuwa vigumu kupata furaha. Hatimaye, usisite kuomba msaada au kupata taarifa."
Nagoski anaamini kuwa kuridhika katika kushiriki tendo la ngono ni wakati ambapo wenzi wote wawili wana furaha sawa.
Jambo muhimu ni kwamba zaidi ya kushiriki tendo la ndoa kila mara, uzoefu ndio kitu cha kufurahisha na kinachoboresha uhusiano.
Comments