TANGA YAPIGA HATUA KUBWA YA MAENDELEO AWAMU YA RAIS SAMIA

 

Mkuu wa Mkoa wa Yanga, BALOZI Batilda Baruani akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO jijini Dodoma Julai 14, 2025, kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Wanahabari wakiwa katika mkutano huo.


MUHTASARI WA TAARIFA YA MAENDELEO YA MKOA WA TANGA KWA VYOMBO VYA HABARI JUNI, 2025

 

1.0 UTANGULIZI.

Taarifa ya maendeleo katika Mkoa wa Tanga inalenga kuwahabarisha wananchi wa mkoa wa Tanga na umma wa watanzania kwa ujumla kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza Mipango ya maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala na ahadi mbalimbali zilizotolewa na viongozi wa Kitaifa. Maeneo yaliyotajwa kwenye taarifa hii ni yale yanayohusu sekta za Elimu, Afya, Barabara, Maji, Nishati, Kilimo ,mifugo ,utalii na Bandari. Aidha, taarifa pia imeelezea miradi  ya vitega uchumi pamoja na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

1.1  Eneo na Mipaka

Mkoa wa Tanga una eneo la kilometa za mraba 27,342, Kijiografia Mkoa wa Tanga unapatikana upande wa Kaskazini Mashariki mwa Tanzania Bara. Mkoa umelala  katika latitudo 4 na 6 Kusini mwa Ikweta na kati ya longitudo 37 na 39 Mashariki mwa Greenwich. Mkoa umepakana na nchi ya Kenya na Mkoa wa Kilimanjaro kwa upande wa Kaskazini, Mkoa wa Manyara upande wa Magharibi, Mikoa ya Morogoro na Pwani  upande wa Kusini na Bahari ya Hindi, Visiwa vya Unguja na Pemba upande wa Mashariki..

 

1.2 MUUNDO WA UTAWALA


Mkoa umegawanyika katika Wilaya nane (8) za Handeni, Kilindi, Korogwe,  Lushoto, Muheza, Pangani, Mkinga na Tanga. Halmashauri kumi na moja (11) za Handeni Vijijini, Handeni Mji, Kilindi, Korogwe Vijijini, Korogwe Mji, Lushoto, Bumbuli, Muheza, Pangani, Mkinga na Tanga Jiji. Mkoa una jumla ya Tarafa 37, Kata 245, Vijiji 763, Mitaa 270 na Vitongoji 4,531.

 

1.3 WAKAZI NA IDADI YA WATU

Kwa mujibu wa takwimu za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi, 2022 Mkoa wa Tanga una idadi ya watu 2,615,597 (wanaume 1,275,665 na wanawake 1,339,932) na Ongezeko la watu kwa mwaka ni asilimia 2.5.Inayopelekwea idadi ya watu kufikia 2,861,741 kwa  mwaka 2025 (wanaume 1,406,476 na wanawake 1,455,265)

1.4 ULINZI NA USALAMA

Hali ya ulinzi na usalama ni shwari. Vyombo vya dola vimeendelea kufanya doria za mara kwa mara ili kuimarisha usalama wa ndani na mipaka ya nchi kavu pamoja na baharini. Katika kipindi hiki hakuna matukio makubwa yaliyojitokeza yenye kuhatarisha usalama wa Mkoa.

 

1.5  PATO LA MKOA NA HALI YA UCHUMI

Kwa mujibu wa Takwimu wa NBS   kwa mwaka 2024, pato la Mkoa (GDP) limeongezeka kutoka wastani wa shilingi Trilioni 6.818 kwa mwaka 2020 hadi shilingi Trilioni 9.581 kwa mwaka, 2024 sawa na asilimia 4.7 ya Pato la Taifa ambalo ni shilingi Trilioni 205.846.

Aidha, wastani wa pato la Mtu mmoja (Per Capital Income) limeongezeka kutoka wastani wa shilingi milioni 2.783,908.00  kwa mwaka 2020 hadi shilingi milioni 3,433,368.00 kwa mwaka, 2024. Ikiwa ni juu ya wastani wa kitaifa wa shilingi 3,204,244.00. Takwimu hizi zinauweka Mkoa wa Tanga kushika nafasi ya sita (6) kati ya Mikoa yote ya Tanzania Bara katika vita dhidi ya umaskini pamoja na mchango wa pato la Taifa.

Shughuli za kiuchumi na uzalishaji zinazotekelezwa na Wananchi wa Mkoa wa Tanga zipo kwenye maeneo mbalimbali zikiwemo Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Maliasili na Utalii. Aidha, Shughuli nyingine za uzalishaji zinatokana na ukuaji wa Sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji unaozingatia ujasiriamali katika sekta za umma na binafsi. Hata hivyo, Wananchi walio wengi zaidi ya asilimia 80 wamejikita katika shughuli za Kilimo, mifugo na uvuvi, asilimia tisa (9) wanajishughulisha na shughuli za mazao ya misitu, ufugaji nyuki na uchimbaji madini, asilimia sita (6) wanajishughulisha na shughuli za biashara, uendeshaji wa viwanda,usafirishaji na uchukuzi na Sekta ya Fedha. Halikadhalika asilimia tano (5) wameajiriwa katika sekta za umma na binafsi kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za kijamii.

 

2.0 MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA MAENDELEO KISEKTA

Kwa kipindi cha Serikali ya awamu ya sita Mkoa umepokea fedha shilingi 3,091,742,180,252.12 (Trilioni 3.091)  kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Maendeleo ya Kisekta kama ifuatavyo hapo chini:-

 

2.1 SEKTA YA AFYA

Mafanikio yaliyopatikana ya katika uboreshaji wa huduma za Afya ikiwemo Ongezeko la Vituo vya kutolea Huduma za Afya, dawa na vifaa tiba  limesaidia   kuwasogezea wananchi huduma bora za  Afya karibu na maeneo yao, hivyo kupunguza Vifo vya wakina mama na watoto kabla, baada na wakati wa kujifungua na umepunguza rufaa zisizo za lazima kwenda nje ya Mkoa.  

Mafanikio katika Sekta ya Afya ni kama ifuatavyo;-

i. Mkoa wa Tanga  katika kipindi cha  mwaka 2020 hadi 2025 umeongeza vituo vya kutolea huduma za Afya vya serikali kutoka 325 hadi 417 ikiwa ni ongezeko la vituo 92.

ii. Zahanati zimeongezeka kutoka 287 hadi 361 sawa na ongezeko la zahanati 74,

iii. Vituo vya Afya vimeongezeka kutoka 31 hadi 46 sawa na ongezeko la Vituo 15,

iv. Hospitali zimeongezeka kutoka 7 hadi 10 sawa na ongezeko la Hospitali 3.

v. Ununuzi wa Dawa na Vifaa Tiba Mkoa umepokea shilingi 19,751,050,000.00 za vifaa tiba, ikiwemo CT Scan, Digital X-ray Machine, Vitanda vya wagonjwa na Ambulance.  

vi. Mkoa umepokea kiasi cha shilingi 3,600,000,000.00   kwajili ya ununuzi wa Magari 12 ya kubebea wagonjwa.

vii. Mkoa  umepokea jumla ya shilingi  17,575,497,902.00 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali  6 za Wilaya, ukarabati wa Hospitali 3 pamoja, ukarabati na umaliziaji wa Hospitali moja katika Halmashauri za Jiji la Tanga, Mji wa Handeni, Wilaya ya Handeni, Mji wa Korogwe, Wilaya ya Kilindi, Wilaya ya Mkinga, Wilaya ya Muheza,Wilaya ya  Lushoto, Wilaya ya  Bumbuli, Wilaya ya Pangani na Wilaya ya  Korogwe.

viii. Mkoa umepokea shilingi 1,000,000,000.00 kwa ajili ya Majengo 3 ya dharura (EMD) katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, Wilaya ya Kilindi na Handeni

ix. Mkoa umepokea shilingi 1,137,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa   nyumba za watumishi wa afya 19 na kusaidia kupunguza tatizo la makazi kwa watumishi.

x. Mkoa umepokea shilingi 250,000,000.00 kwa ajili ya  ujenzi wa Jengo la Wagonjwa Mahututi (ICU) katika hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.

xi. Mkoa umepokea jumla  ya shilingi 4,463,960,376.00 kwajili ya kuboresha miundombinu ya maji na Vyoo,Watu wenyenye mahitaji maalumu,Miundombinu ya kunawa mikono na vichomea taka katika vituo 71 katika  vituo vya kutolea huduma za  Afya.

xii. Mkoa ulipokea jumla ya Watumishi ajira mpya wa Afya 926 na kupangiwa kazi katika vituo vya kutolea huduma za afya. Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi kufikia Mei, 2025  kuna jumla ya ongezeko la watumishi wapatao 1,195 kati ya waliokuwepo 3,185 hivyo kufikia jumla ya watumishi 4,380 waliopo kwa sasa.

 

2.2 SEKTA YA ELIMU

Sekta ya Elimu katika Mkoa wa Tanga inajumuisha Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu,kupitia fedha za ujenzi wa miundombinu zilizotolewa na Serikali, mafanikio mengi yamepatikana katika sekta ya Elimu ikiwemo ongezeko la ufaulu, idadi ya Shule pamoja na  miundombinu ya  shule  ikiwemo,Ujenzi wa shule mpya,  vyumba vya madarasa,nyumba za walimu, mabweni, mabwalo  ambavyo  vimerahisisha shughuli za ufundishaji wa wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari.

 

Mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Elimu Kuanzia Mwezi mwaka  2020 hadi Mei, 2025

i. Elimu bila Malipo na uendeshaji wa MitihaniKumekuwa na ongezeko la fedha za Elimu bila malipo kutoka shilingi 13,041,269,636.00 mwaka  2020 hadi shilingi 65,917,375,000.00 mwaka 2025.

ii. Fedha za uendeshaji wa mitihani zimeongezeka kutoka  shilingi 8,208,700,680.00 mwaka 2020 hadi shilingi 60,325,111,000.00 mwaka 2025. 

iii. Kwa upande wa elimu ya Msingi, Ufaulu wa mtihani wa upimaji wa Darasa la Nne umeongezeka kutoka  asilimia 84.71 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 89 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 4.29

iv. Asilimia ya Ufaulu Darasa la saba umeongezeka kutoka asilimia 70.23 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 77.52 mwaka 2025 sawa na asilimia 7.29

v. Kwa upande wa shule za Sekondari ufaulu wa Kidato cha pili umeongezeka kutoka asilimia 87.36 hadi asilimia 89.6 sawa na ongezeko la asilimia 2.24

vi. Ufaulu kidato cha nne umeongezeka kutoka asimilia 81.95 hadi asilimia 89.10 sawa na asilimia 7.15

vii. Ufaulu wa Kidato cha sita umeongezeka kutoka asilimia 99.68 hadi asilimia 99.9 sawa na ongezeko la asilimia 0.22.

viii. Shule za msingi zimeongezeka 94 kutoka  shule 1,054 mwaka 2020 hadi shule 1,148 mwaka 2025

ix. Shule za Sekondari zimeongezeka kutoka shule 290 mwaka 2020 hadi shule 336 mwaka 2025 sawa na ongezeko la shule 46

x. Madarasa kwa shule za msingi  yameongezeka  1,031 kutoka madarasa 7,048  mwaka 2020 hadi madarasa 8,079 mwaka 2025.

xi. Kwa shule za Sekondari kumekuwa na ongezeko la Madarasa 1,232 kutoka madarasa  2,712 mwaka 2020 hadi madarasa 3,944 mwaka 2025.

xii. Kumekuwa na ongezeko la uandikishaji darasa la awali 7,035 kutoka wanafunzi 58,098 mwaka 2020 hadi 65,133 mwaka 2025.

xiii. Kumekuwa na  ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza 6,128 kutoka wanafunzi 72,254  mwaka 2020 hadi 78,382 mwaka 2025.

xiv. Kwa shule za Sekondari kumekuwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wa Kidato cha kwanza  kutoka 35,301  mwaka 2020 hadi 44,108 mwaka 2025 sawa na ongezeko la wanafunzi 8,807.

xv. Kwa shule za msingi Kuongezeka kwa nyumba mpya  45 za walimu kutoka nyumba 15 mwaka 2020 hadi kufikia nyumba 60 mwaka 2025.

xvi. Kumekuwa na ongezeko la Ujenzi wa nyumba  13 za walimu kwa Shule za Sekondari   kutoka nyumba 28 mwaka 2020 hadi 41 mwaka 2025

xvii. Kwa upande wa  shule za msingi Kuongezeka kwa  mabweni 48  kutoka mabweni 38 mwaka 2020 hadi mabweni 86 mwaka 2025

xviii. Kwa shule za Sekondari kumekuwa na ongezeko la mabweni 31 kutoka mabweni 48 mwaka 2020 hadi mabweni 81 mwaka 2025

xix. Kuongezeka Kwa matundu ya vyoo 2331 kutoka 1289  mwaka 2020 hadi 3620 mwaka 2025 kwa shule za msingi na Sekondari.

xx. Kumekuwa na ongezeko la Ujenzi wa Maabara 117 katika shule za Sekondari kutoka maabara  40 mwaka 2020 hadi maabara 157 mwaka 2025.

xxi. Kuongezeka kwa vyuo vya Ufundi stadi VETA kutoka chuo kimoja(1) mwaka 2020 hadi vyuo 7 mwaka 2025 vyuo hivyo vipo katika maeneo ya Wilaya ya Kilindi vipo viwili (02), Korogwe kimoja (01), Mkinga kimoja (01),Lushoto kimoja (01), Pangani kimoja (01) na Tanga Jiji kimoja (01). Aidha vyuo viwili vinaendelea kujengwa katika Wilaya za Muheza na Handeni.

xxii. Kuongezeka kwa viwango vya ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo kwa vidato vyote vya Mitihani  na kufanya Mkoa wa Tanga  kufanya vizuri kitaaluma,kwa baadhi ya Halmashauri.

xxiii. Kufanya ufuatiliaji kabambe wa ufundishaji na ujifunzaji katika Halmashauri zote kwa ufanisi.

xxiv. Ujenzi wa miundombinu umefanyika katika Shule zake 17 za Kidato cha 5 na 6, jumla ya madarasa 249 yamejengwa, mabweni 33 na matundu ya vyoo 384.

xxv. Ujenzi wa shule mpya ya wasichana ya Mkoa iliyopo Wilaya ya Kilindi ambayo kwa sasa ina Kidato cha kwanza na cha tano.

 

2.3  MTANDAO WA BARABARA NA HALI YA BARABARA MTANDAO WA BARABARA NA HALI YA BARABARA

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Tanga unasimamia mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa km 7,373.70 kati ya hizo km  165.68 ni za lami, km  2,071.38 za changarawe na km 5,136.64 ni za udongo. Aidha, barabara zenye hali nzuri km 2,907.66 ambayo ni sawa na 39%, zenye hali yakuridhisha km 2,745.18 ambayo ni sawa na 37% na zile zilizoko katika hali isiyoridhisha km 1,720.87 ambayo ni sawa 23%. Pia Mkoa wa Tanga una jumla ya madaraja 104, Box kalavati 496, makalavati 5,398 na daraja Mfuto 306.

 

Mafanikio ya miradi ya Barabara TARURA

Kumekuwa na  mafanikio makubwa katika kuboresha mtandao wa Barabara, katika kipindi hiki cha chini ya Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ifuatavyo;-

i. Barabara za kiwango cha  lami zimeongezeka kutoka km 124.08 hadi km 165.68

ii. Barabara changarawe zimeongezeka kutoka km 1395.87 hadi km 2,071.38.

iii. Barabara za udongo zimepungua  kutoka km 5839.2 hadi km 5,136.64,

iv. Tumeongeza vivuko kutoka madaraja 91 hadi 100.

v. Tumeongeza Daraja mfuto (drift) kutoka 202 hadi kufikia 306,

vi. Tumeongeza Kalavati kutoka 5019 hadi kufikia kalavati 5,398

vii. Tumeongeza Boksi kalavati kutoka 428 hadi kufikia boksi kalavati 498.

 

2.3.1 UTEKELEZAJI WA MRADI WA UBORESHAJI MIJI (TACTIC)

Mradi wa kuboresha Miji (TACTIC) ambao utekelezaji wake upo katika Jiji la Tanga ambapo zitajengwa km 4 kwa kiwango cha lami, soko la samaki,soko la makorora, ukarabati wa fukwe raskazone na ujenzi wa mifereji yenye urefu wa km 4. Wilaya ya Korogwe zitajengwa km 10.4 kwa kiwango cha lami na ujenzi wa mifereji yenye urefu wa km 1.9  na Wilaya ya Handeni zitajengwa km 4.1 kwa kiwango cha lami. Aidha,hadi kufikia Januari, 2025 kazi zote za mradi huu zipo katika maandalizi huku usanifu ukiendelea kufanywa na Mshauri elekezi ‘‘Consultant’’ kwa Wilaya ya Tanga, Korogwe na Handeni, mradi upo katika hatua za awali za manunuzi.

2.3.2 UTEKELEZAJI WA MRADI WA BARABARA WA UJUMUISHWAJI NA UFUNGUAJI FURSA ZA KIUCHUMI NA ZA KIJAMII ((RISE)

TARURA inaendelea kutekeleza mradi wa ujumuishwaji na ufunguaji fursa za kiuchumi na za kijamii (roads to inclusion and social economic opportunities project) (rise). Katika mkoa wa Tanga mradi huu unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ambapo jumla ya kilomita 105.11 zinategemewa kutengeneza kwa kiwango cha lami. Barabara hizo ni Sindeni-Kwedikwazu kilomita 37.7, Kabuku - Mzundu kilomita 17.6,  Michungwani-Bondo-Kwadoya kilomita 18.8,  Mkata - Kwasunga kilomita 21 na Kwachaga - Kwankonje kilomita 10.01.

Mradi huu una sehemu ya utekelezaji wa kuondoa Vikwazo “Bottle neck Removal” katika maeneo yafuatayo ya Pangani DC, Muheza DC, Korogwe TC na DC, Bumbuli DC na Mkinga DC bajeti iliyopangwa ni Tshs. 2,573,100,000.00.

 

2.4 SEKTA YA BARABARA - WAKALA WA BARABARA (TANROADS)

Mtandao wa barabara unaohudumiwa na TANROADS ni km 1,809.30. Kati ya hizo, barabara ]kuu zina urefu wa km 327.25 za lami, barabara za Mkoa zina urefu wa km 198.26 za lami na km 1,283.79 za changarawe/udongo. Aidha, kuna jumla ya madaraja na makalvati makubwa yapatayo 470, kati ya hayo madaraja 156 yapo katika barabara kuu na madaraja 314 yapo katika barabara za Mkoa.Mtandao wa barabara wa Wakala ya Barabara (TANROADS) uliongezeka kutoka km 1,528.54 mwaka 2007 hadi km 1,809.30 za sasa. Hii ikiwa ni ongezeko la km 280.76.

Miradi ya Barabara Mikubwa ya Kitaifa ya Maendeleo Mkoani Tanga

Miradi mikubwa ya kitaifa ya maendeleo inayoendelea Mkoani ni kama ifuatavyo:-

i. Ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge) – Saadani – Pangani-Tanga (256km) kwa kiwango cha lami

ii. Ujenzi wa Barabara ya Tanga – Pangani kwa kiwango cha lami (50km) -sehemu ya kwanza

iii. Ujenzi wa daraja la mto Pangani lenye urefu wa mita 525 pamoja na barabara ya maungio yake (approaches) yenye km 14.3, barabara ya mchepuko ya Ushongo yenye urefu wa km 5.9 na barabara za mchepuo za Pangani mjini zenye urefu wa km 5.4 - Sehemu ya pili

iv. Ujenzi wa barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange kwa kiwango cha lami (95.2km) pamoja na barabara ya mchepuo ya Kipumbwi (3.7km) -Sehemu ya tatu  (Lot 3)

v. Ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge)-Mkange Lot 4

vi. Ujenzi wa Barabara ya Muheza – Amani (40km) kwa kiwango cha lami

 

2.5 SEKTA YA MAJI

SEKTA YA MAJI

Mkoa wa Tanga kwa mwaka wa fedha 2020 hadi 2023/2025 tumepokea takribani kiasi cha Shilingi 1,229,959,984,625.11 kwa ajili ya utekelezaji wa Huduma ya Maji katika Wilaya zote nane za Mkoa wa Tanga.

2.5.1 Mafanikio ya Sekta ya Maji kwa kipindi cha 2020  hadi 2025.

Katika kipindi cha Tajwa hapo juu sekta ya maji katika Mkoa wa Tanga imekuwa na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu kama ifuatavyo:-

i. Kiwango cha upatikanaji maji katika Mkoa wa Tanga kimeongezeka kutoka 54%  hadi kufikia 79% na katika maeneo ya vijijini kimeongezeka kutoka 49.7% hadi kufikia 75% na miundombinu imefikia 95% mwaka  2020 hadi kufika mwaka 2025.

ii. Kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yanayohudumiwa  na Mamlaka za maji HTM kimeongezeka hadi kufikia 71.9%, Mamlaka ya Maji Mji mdogo wa Songe - Kilindi kufikia 59.6% Mamlaka ya Maji Mji mdogo wa Lushoto kufikia 68.66% na Mamlaka ya maji Tanga UWASA kufikia 95%  hadi Januari, 2024

iii. Idadi ya vijiji vinavyopata huduma ya maji imeongezeka kutoka vijiji 476 mwaka 2020 hadi kufikia vijiji 601 mwaka 2025.

iv. Jumla ya miradi 151 imetekelezwa kupitia RUWASA ambapo katika miradi hiyo miradi 96 imetekelezwa na kukamilika na inatoa huduma, miradi 65 yenye thamani ya Shilingi 88,567,399,016.47 inaendelea na utekelezaji katika maeneo ya vijijini na mabwawa ya maji mawili yamejengwa na kukamilika (Handeni 1 na Mkinga 1).

v. Jumla ya visima virefu 175 vimechimbwa ambapo kati ya visima hivyo visima 63 vimeendelezwa na vituo 1,193 vya kuchotea maji vimejengwa katika maeneo ya vijijini na Miradi ya majisafi 20 yenye thamani ya Shilingi 161,460,391,816.00 inaendelea kutekelezwa chini ya usimamizi wa Tanga UWASA, ambapo katika miradi hiyo miradi 7 imekamilika na wananchi wanapata huduma.

vi. Serikali kupitia mamlaka ya maji Tanga UWASA imewezesha ujenzi wa miundombinu ya uondoshaji majitaka katika miji ya huduma ambapo jumla ya miradi 6 yenye thamani ya shilingi 4,274,737,622 inaendelea kujengwa.

vii. Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuweka mazingira mazuri na wadau mbalimbali wa maendeleo (Wordvision, Islamic Help, Water Aid, AMREF, Nyota Foundation) katika Sekta ya maji kwa kutuchimbia visima 108 na kujenga miundombinu ya maji  wananchi katika Mkoa wa Tanga.

 


2.6  NISHATI


2.6.1 SHIRIKA LA UMEME - TANESCO MKOA WA TANGA

Mkoa wa Tanga unapata umeme kupitia gridi ya Taifa, Mahitaji ya juu ya umeme katika Mkoa wa Tanga ni 120MW. Mkoa umepokea shilingi 430,236,577,294.15 kwa ajili ya Kuboresha upatikanaji wa Umeme Mijini na Vijijini kwa upande wa TANESCO na REA III mzunguko wa Pili kwa ajili ya kutekeleza miradi ifuatayo;-

• Miradi ya kuondoa umeme hafifu na ukarabati wa miundombinu, Ujenzi wa miradi mipya pamoja na uunganishaji wa wateja wapya na Miradi ya Kimkakati- GRIDI IMARA.

 

 

 

 

UTEKELEZAJI WA UMEME WA REA

• Mkoa wa Tanga una jumla ya vijiji 763 ambapo vijiji vyote sawa na asilimia 100 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya awali kama vile REA awamu ya kwanza (REA I), REA awamu ya pili (REA II), REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza (REA III Round I), na REA awamu ya tatu mzunguko wa pili (REA III Round II).

 


• Jumla ya Vitongoji 2382 vimefikiwa na huduma ya umeme kati ya vitongoji 4531 vya mkoa wa Tanga ikiwa ni sawa na asilimia 52.6 ya vitongoji vyote. Sambamba na miradi inayotekelezwa, wakala umepanga kufikisha umeme katika vitongoji 180 kupitia mradi wa HEP 2A ambapo Mkandarasi amepatikana mwezi April, 2025 na pia vitongoji 673 viko katika mpango wa kufikishiwa umeme kupitia mradi wa vitongoji HEP 2B unaotegemewa kuanza utekelezaji wake katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026

Mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi  2025.

Kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 idadi ya wananchi wanaotumia umeme imeongezeka kutoka 145,496 mpaka kufikia 248,213 ikiwa ni ongezeko la 41.4%

2.6.2 MATUMIZI NISHATI SAFI KWA  MKOA WA TANGA

Mkoa umetoa na unaendelea kutoa elimu juu ya matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa wananchi na Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali. Hadi sasa Taasisi 1,493 za Serikali zenye watumiaji 735,372 zimetambuliwa.

 

2.7 SEKTA YA UCHUMI NA UZALISHAJI

2.7.1 KILIMO:

Mkoa umepokea Fedha kiasi cha shilingi 33,302,931,461.50 kwa ajili ya shughuli za kilimo kama ifuatavyo •​Hali ya Chakula ni nzuri kwani Katika msimu wa kilimo wa 2023/24  Mkoa wa Tanga ulilima jumla ya hekta 909,076 za mazao ya chakula na kuzalisha tani 2,659,802 (ghafi), sawa na tani 1,314,292.4 za chakula kikavu. Uzalishaji huu umetosheleza mahitaji ya wakazi wapatao 2,600,000 wa mkoa huu, na kuwa na ziada ya chakula kwajili ya kufanya biashara na hifadhi.

Mafanikio katika kilimo ni kama ifuatavyo; -

• Pembejeo za ruzuku - Katika kuboresha upatikanaji wa chakula na usalama wa lishe, Serikali inaendelea kusambaza mbegu bora na mbolea kwa wakulima kupitia ruzuku. Wakulima 134,527 wamesajiliwa katika mfumo wa kidigitali wa ruzuku ili waweze kunufaika na ruzuku ya pembejeo za kilimo inayotolewa na Serikali ya Awamu ya sita.Wakulima 11,198 walinufaika na tani 4,235.35 za pembejeo kwa gharama ya shilingi 8,100,000,000.00, huku Serikali ikitoa ruzuku ya shilingi 2,500,000,000.00.

• VITENDEA KAZI SEKTA YA KILIMO - Mkoa umeendelea kuboresha huduma za ugani kwa kusambaza vifaa vifuatavyo:

• Pikipiki 380 kwa maafisa ugani zenye thamani ya shilingi 950,000,000.00

• Vishkwambi 371 vyenye thamani ya shilingi 296,800,000.00 kwa ajili ya ukusanyaji wa takwimu,

• Vipima udongo (Soil Scanners) 7 zenye thamani ya shilingi 153,000,000.00 kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kupima udongo na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.

• MPANGO WA JENGA KESHO ILIYO BORA (BBT) - Mkoa uliendesha mpango wa Building a Better Tomorrow (BBT) kwa vijana 45 ili kushiriki katika mafunzo ya kilimo cha mazao ya biashara katika Chuo cha Kilimo Mlingano na walishahitimu. Mradi huu uligharimu shilingi 63,000,000.00.

• Bodi ya korosho Tanzania iliajiri maafisa ugani 22 (internship) kupitia mpango wa BBT kwa ajili ya kuendeleza zao la korosho (BBT Agricultural Extension Enterpreurship Scheme).

• Ununuzi wa mashine za kuchakatia Mkonge (CORONA) AMCOS ya Kibaranga Muheza DC.

• Miradi ya Umwagiliaji Bonde la Mto Umba, Mradi wa ujenzi wa bwawa la Umwagiliaji Mkomazi Kijiji cha Manga Mtindiro, Ujenzi wa miundombinu ya skimu ya Mahenge.

• Uanzishwaji wa TANZANIA SISAL BOARD-TSB ambayo inasaidia ununuzi wa korona za kuchakata Mkonge, usambazaji bure wa miche ya Mkonge kwa wakulima na Uboreshaji wa vitendea kazi.

 

2.7.2 MAZAO YA BIASHARA

2.7.3 Mkonge

Mkoa wa Tanga unazalisha zaidi ya 50% ya mkonge nchini. Uzalishaji wa mkonge umeongezeka kutoka tani 14,835 mwaka 2021 hadi tani 22,620 mwaka 2023. Serikali inatekeleza mpango wa kuongeza viwanda vya usindikaji wa mkonge kwa kushirikiana na sekta binafsi.

 

 

 

2.7.4 Chai

Mkoa unashirikiana na sekta binafsi katika kuboresha masoko na miundombinu ya usindikaji wa chai ili kuongeza thamani ya zao hili na kuongeza kipato kwa wakulima. Uzalishaji wa chai kwa sasa ni tani 31,492 ambazo zinaingizia Mkoa takribani shilingi 1,337,120,000.00.

 

2.7.5 Korosho

Mkoa umepokea jumla ya viuatilifu vya maji lita 22,890 na vya unga (Sulphur) tani 229,822 vyenye thamani ya shilingi 1,900,000,000.00 sambamba na upatikanaji wa mbegu bora za korosho kg 5,943 zenye thamani ya shilingi 29,715,000.00 na kusambazwa kwa wakulima wa korosho bure. Aidha, mkakati wa kufufua mashamba ya zamani unaendelea ambapo hadi sasa, kiasi cha ekari 980 zimefufuliwa. Jumla ya kilo 366,966 zenye thamani ya shilingi 925,885,856.00 ziliuzwa kwa kutumia mfumo wa soko la bidhaa Tanzania TMX (Tanzania Merchantile Exchange).

2.7.6 Pamba

Mkoa ulizalisha jumla ya tani 1, 200 zenye thamani ya shilingi 2,400,000,000.00 na malengo ni kuzalisha tani 2,500 ifikapo msimu wa mwaka 2029/30.Wakulima wanaendelea kuongeza maeneo ya kilimo cha pamba kila msimu.

 

2.7.7 Muhogo

Serikali inaendelea kuhamasisha wakulima kuingia kwenye kilimo cha muhogo kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya kiwanda na masoko ya nje. Kwa sasa uzalishaji wa muhogo ni kiasi cha tani 1,681,121. Malengo ya mkoa ni kufikia uzalishaji wa tani 2,256,150. Zao hili linaingiza kiasi cha shilingi 16,810,000,000.00 kwa mwaka kwa wazalishaji wa mkoa wa Tanga.

 

2.7.8 MAZAO YA VIUNGO

Mkoa umeanzisha ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha tunaongeza uzalishaji wenye tija katika mazao ya viungo vya mdalasini, iliki, karafuu, na pilipili manga kupitia Zanzibar State Trading Corporation (ZSTC). Mpango huu unalenga kuimarisha ushirikiano wa masoko na viwanda vya usindikaji wa mazao ya viungo vilivyopo. Kwa sasa uzalishaji wa viungo kwa mkoa ni tani 4,016 ambazo zinaingiza kwenye mkoa kiasi cha shilingi 42,106,000,000.00 kwa mwaka.

 

2.7.9 KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Mkoa wa Tanga una eneo lenye uwezo wa kumwagiliwa la hekta 32,348, kati ya hizo hekta 5,430 zinatumika kwa sasa. Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya umwagiliaji ikiwemo:

i. Ujenzi wa bwawa la umwagiliaji Mkomazi (shilingi 18,000,000,000.00),

ii. Ukarabati wa skimu ya umwagiliaji Mahenge (shilingi 2,100,000,000.00), na

iii. Uchimbaji wa visima kwa wakulima wadogo.

 

Upembuzi yakinifu wa Bonde la Mkomazi  kwa gharama ya shilingi 296,000,000.00

 

2.8. MIFUGO NA UVUVI

Katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Aprili 2025 Mkoa umepokea Fedha kiasi cha shilingi 20,155,690,197.00 kwa ajili ya shughuli za Mifugo kama ifuatavyo;-

 

Mafanikio katika sekta ya mifugo nikama ifuatavyo:-

• Majosho 42 yamejengwa kwa jumla ya shilingi 966,000,000.00. Halmashauri za Wilaya ya Mkinga, Kilindi, Handeni, Lushoto, Korogwe na Mji wa Handeni zimefaidika na ujenzi wa majosho na kupunguza vifo vya mifugo vinavyotokana na kupe na wadudu wengine.

• Ujenzi wa majosho 8 Halmashauri za Handeni Wilaya (3), Mkinga (2) na Kilindi (3), utoaji wa  Lita 1,097.5 za dawa ya kuogeshea mifugo Handeni DC, Handeni TC, Mkinga, Lushoto, Bumbuli, Pangani, Korogwe DC, Kilindi na Korogwe Mji.

• Ununuzi wa Boti 14 za uvuvi na Ujenzi wa Soko la kimataifa la Samaki la Kipumbwi ambalo liko hatua za maandalizi ya ujenzi.

• LIVESTOCK TRAINING AGENCY- BUHURI Kuongeza fursa ya ajira kwa vijana kwa kuanzisha kituo atamizi kwa vijana 30 kufuga kibiashara kwa kunenepesha ng’ombe 600.

• Ununuzi wa Boti 50 za unenepeshaji wa viumbe Bahari na Ununuzi wa Boti 43 za uvuvi.

• Minada 5 imejengwa na kukarabatiwa kwa kiasi cha shilingi 2,628,175,197.00. Minada hii ni muhimu katika kuwezesha biashara ya mifugo na kutoa fursa za masoko kwa wafugaji. Minada hii imejengwa katika Halmashauri za Wilaya ya Mkinga - Horohoro, Handeni - Msomera, Lushoto – Lunguza na Mji wa Handeni – Nderema, na Pangani- Masaika. Pia, katika kuboresha biashara ya mifugo, minada ya Nderema, Kibirashi, Msomera na Horohoro inasimikwa mizani ili kuwezesha mifugo kuuzwa kwa uzito badala ya kukadiriwa.

• Serikali iligawa pikipiki 36 zenye jumla ya shilingi 90,000,000.00 kwa maafisa ugani.

• Mashamba 13 ya malisho yameanzishwa katika Halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Handeni na Korogwe, kwa jumla ya shilingi 186,515,000.00.

• Serikali imefanikiwa kutoa mitamba ya ng’ombe wa maziwa 464 yenye thamani ya shilingi 1,180,000,000.00 kwa wafugaji ili kuboresha uzalishaji wa maziwa.

• Madume ya kisasa ya ng’ombe aina ya boran 10 yenye thamani ya shilingi 30,000,000.00 yamegawiwa kwa wafugaji wa ng’ombe wa asili katika kijiji cha Msomera ili kuboresha koosafu zao.

• TALIRI kuongeza fursa kwa vijana 30 waweze kufuga kibiashara kwa kunenepesha ng’ombe 300.

• Kupitia mradi wa Maziwa Faida unaosimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) wenye thamani ya zaidi ya shilingi 7,000,000,000.00, mkoa unazalisha mbegu za malisho, kutoa elimu ya malisho na kuhamasisha umuhimu wa malisho kwa wafugaji. Mkoa upo kwenye mchakato wa kuanzisha kampeni ya Mifugo ni Malisho ili kuhamasisha wafugaji wazalishe malisho kwa ajili ya mifugo yao.

 

2.9 MALIASILI NA UTALII

  Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:-

• Kuongezeka kwa ajira za moja kwa moja katika Sekta ya Utalii ambapo zaidi ya watu 856 wameajiriwa na zaidi ya watu 1,120 wanajihusisha na shughuli za usafirishaji, uongozaji na malazi ya watalii;

 

• Kuongezeka kwa kiwango cha uzalishaji wa mazao ya misitu na nyuki kutoka asilimia 23 hadi asilimia 71;

• Kuongezeka kwa vikundi vya wazalishaji wa mazao ya misitu na nyuki kutoka vikundi 86 hadi vikundi 243;

• Kuongezeka kwa maeneo ya ufugaji wa nyuki kutoka 12 hadi 19;

• Kuongezeka kwa misitu iliyohifadhiwa kwa ajili ya biashara ya kaboni kutoka 0 hadi 3; na

• Kuongezeka kwa miti iliyopandwa kutoka miti 8,142,122 hadi miti 11,902,125.

 


2.10 SEKTA YA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA

Sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ni miongoni mwa mihimili mikuu katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Mkoa kufikia Juni, 2025, una jumla ya Viwanda 4,117 kati ya hivyo 4,013 ni Viwanda Vidogo na vidogo sana, 69 ni Viwanda vya Kati na 35 ni Viwanda Vikubwa.

Viwanda hivi vina jumla ya Wafanyakazi 65,275 ambapo kati ya hao wafanyakazi wa kudumu ni 6,747 na wa muda ni 58,528.

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020 hadi Juni 2025 Mkoa umefanikiwa kama ifuatavyo;-

• Kuongeza idadi ya viwanda vikubwa kutoka 16 hadi 35 ongezeko la viwanda (19),

• viwanda vya kati kutoka 23 hadi 69 ongezeko la viwanda (46) na

• viwanda vidogo na vidogo sana 2,402 hadi 4,013 ongezeko la viwanda 1,611.

• Ongezeko la ajira takribani 65,275 kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kufikia Juni, 2025.

 

2.10.1 Uzinduzi wa Ugawaji wa Vitambulisho vya Wafanyabiashara ndogo ndogo

Mkoa wa Tanga una jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 60,253 wanaume 37,137 wanawake 23,116 (Ofisi za takwimu -Taifa NBS). Mkoa umeweza kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara ndogondogo wapatao 2,306 wanawake 1,448, wanaume 858. Mkoa umepokea vitambulisho 1,151 na kuvigawa kwa Walengwa, uhamasishaji na usajili unaendelea;

 

2.11 Uwezeshaji Wananchi kiuchumi

2.11.1 kupitia Mikopo ya asilimia kumi (10) ya mapato ya ndani ya halmashauri

Mkoa wa Tanga katika kipindi cha mwaka 2020 hadi Juni, 2025 ulikusanya na kutenga shilingi 18,503,547,911.00 kwa ajili ya kutoa mikopo ya asilimia kumi (10%) kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Mikopo iliyotolewa ni jumla ya shilingi 13,818,105,148.00 kati ya hizo 8,821,759,263.00 zilitolewa kabla ya mikopo kusitishwa mwezi Machi, 2023 na shilingi 4,996,345,885.00 zilitolewa kipindi cha awamu ya pili baada ya dirisha la mikopo kufunguliwa Septemba, 2024. Aidha, fedha ambazo zipo katika Taasisi za fedha kwa ajili ya kukopeshwa ni jumla shilingi 4,685,442,763.00. Katika kipindi hicho jumla ya vikundi 1,590 vya wanawake (907), Vijana (492) na watu wenye ulemavu (191) vilinufaika na mkopo huo.

 

2.11.2 TASAF

Mpango huu ulikuwa unatekelezwa katika Vijiji/Mitaa 656 vyenye idadi ya Kaya 46,745 na hadi kufikia Mwezi March 2024/2025 Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulikuwa na idadi ya Vijiji/Mitaa 1,039 vyenye kaya 68,609  Katika Mkoa wa Tanga.Uhawilishaji fedha umefanyika kwa awamu kumi na nane (18) na jumla ya fedha kiasi cha  Sh. 26,574,810,628.00 zilipokelewa kwa ajili ya Uhawilishaji kwa Walengwa ambapo fedha hizo zilipokelewa katika Mitaa/ Vijiji.

 

Mafanikio ya TASAF

• Kupitia uanzishaji wa Miradi midogo midogo ya biashara kupika mama lishe, kuuza samaki, kuuza kuku. Kaya Maskini zimeanza kuwa na uhakika wa kujikimu katika maisha yao ya kila siku ambapo jumla ya Walengwa 38,952 sawa na asilimia 57 wamefanikiwa kuanzisha biashara ndogo.

• Walengwa wa Mpango kuwa na uhakika wa kupata huduma muhimu za afya kwa wakati kupitia matumizi ya Bima ya Afya (CHF) ambapo jumla ya walengwa 48,645 sawa na asilimia 71 wameweza kujiunga na Bima ya Afya (CHF)

• Jumla ya Walengwa 44,234 sawa na asilimia 64 wameweza kuanzisha ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku pia kujishughulisha na shughuli za kilimo ambapo wamenufaika kwa kiasi kikubwa.

 


2.12 MIRADI MKAKATI MKOA WA TANGA

Mkoa wa Tanga umeendelea na utekelezaji wa miradi mkakati ili kuwezesha wananchi katika shuguliza kiuchumi na kujiletea maendeleo

i. Uwekezaji wa Jengo la Kibiashara la Dkt. Samia Suluhu Hassan Bussines Centre.  Mradi huu ni wa kimkakati ambao unalenga katika kuhakikisha Jiji linatanua mahitaji kwa wafanyabiashara ili kuweza kuwafikia wananchi katika kufanikisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ndani ya Halmashauri za kibiashara.

ii. Ujenzi wa Soko la Kisasa la wafanyabiashara wadogo-Machinga. Mradi huu utakapokamilika utaweza kuhudumia wafanyabiashara wadogowadogo.

iii. Mkoa wa Tanga ulipokea kiasi cha shilingi 4,513,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Michezo cha Shirikisho la Michezo Tanzania (TFF) katika eneo la Mnyanjani kilichopo katika Halmashauri ya Jiji la Tanga.Mradi huu unasaidia kukuza vipaji vya wananchi wa mkoa wa Tanga.

2.13. MRADI WA BOMBA LA MAFUTA


Mkoa wa Tanga miundombinu ya mradi inayojengwa inahusisha bomba lenye urefu wa km 205.91 Pia inahusisha ujenzi wa Kambi na Miundombinu mingine ni ujenzi wa Kituo cha Kupokelea, Kuhifadhi, kusafirisha, usimamizi na uendeshaji wa Mradi na Matangi 4. mradi umekamilika kwa asilimia 53%.


Hali ya Utekelezaji wa Bomba la Mafuta kwa sasa.


1. Fidia kwa wananchi waliopisha Mkuza wa Bomba Mkoa wa Tanga imefikia 98.7% ambapo kati ya wananchi 1580, wananchi 1560 wameshapokea malipo ya fidia jumla Shilingi billion 9.38, Aidha Wananchi 40 wamejengewa nyumba 43 za makazi mbadala ambazo ujenzi wake umekamilika kwa 100% na kukabidhiwa kwa wahusika;

 

Mradi wa Bomba la Mafuta.

i. Wananchi wamepata ajira kwenye maeneo yote mradi ulipopita, kwa eneo la Chongoleani pekee kuna ajira 810.

ii. Biashara za huduma kama vile Mama/baba lishe.

iii. Kuongezeka kwa mzunguko wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii,  na huduma ndogo za kifedha.

 

2.14 UBORESHAJI  WA BANDARI YA TANGA

Mradi wa Maboresho ya Bandari Katika kipindi cha mwaka 2020 hadi Aprili 2025, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) umetekeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa maboresho ya Bandari ya Tanga kwa awamu mbili yenye thamani ya  shilingi bilioni 429.1.

 

Mafanikio Baada ya Maboresho Kukamilika.

(i) Ufanisi umeongezeka katika kuhudumia meli na shehena ambapo muda wa kuhudumia meli umepungua kutoka siku 5 hadi siku 2.

(ii) Ongezeko la meli 198 mwaka 2021 hadi meli 307 mwaka 2025 na shehena kutoka tani 888,130 mwaka 2021 hadi tani 1,191,480 zinazopakuliwa na kupakiliwa na makasha TEUS 7,036 hadi makasha 7,817  katika Bandari ya Tanga.

(iii) Mapato yameongezeka pamoja na ajira za muda mrefu na muda mfupi.

 

Aidha, Mkoa umepokea kiasi cha thamani ya shilingi 1,118,092,480.00 kwajili ya Ukarabati mkubwa wa kivuko cha MV Tanga ili kusaidia wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.

 

2.15 UTAWALA BORA, RUSHWA, KERO ZA WANANCHI

Mkoa unaendelea kutekeleza misingi ya Utawala bora kwa kufanya yafuatayo:-

Kutenga siku ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati – taarifa ya utatuzi wa kero za wananchi huratibiwa na Mkoa na kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kila mwezi.

i. Kila Taasisi imeunda Kamati ya Kudhibiti Uadilifu kwa watumishi wake ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wananchi bila upendeleo wala ubaguzi wa aina yoyote.

ii. TAKUKURU inaendelea na jukumu lake la Kuzuia na Kupambana na Vitendo vyote vya rushwa kwenye Taasisi za Umma na binafsi. Aidha TAKUKURU wameendelea na kazi ya kuokoa mali na rasilimali za Umma ambazo zilikuwa zinaelekea kupotea kupitia watumishi wasio waaminifu.

iii. Kwa kipindi cha mwaka 2020 Mkoa ulikuwa na mahakama  za mwanzo 65 na  wilaya 6 hadi kufikia mwaka 2025 Mkoa una mahakama za mwanzo 67 na Wilaya 8 hii inaonyesha kuna ongezeko la mahakama za mwanzo 2 na wilaya 2.

iv. Ujenzi wa majengo ya ofisi za wakurugenzi na nyumba za viongozi, Mkoa umepokea fedha kwajili ya ujenzi wa Majengo ya Utawala,Samani za Ofisi, Nyumba za wakurugenzi na Wakuu wa Idara.

3.0 HITIMISHO

Wananchi wa Mkoa wa Tanga kwa pamoja tunaishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza kwa weledi mkubwa ahadi zilizowekwa kwa vitendo kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, na ahadi yao ni kufanya makubwa kwa kujitoa kwa wingi na kushiriki katika uchaguzi mkuu mwaka huu 2025.

Naomba Kuwasilisha.

 

Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian

MKUU WA MKOA

TANGA

34

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

DUNIA NI KATILI SANA KWA MWANAUME MASIKINI

MAKUNDI YA VILABU VINAVYOSHIRIKI KOMBE LA DUNIA 2025.

DIARRA KIPA BORA TANZANIA

MWANAUME USIPITWE NA HILI, INASIKITISHA...?!!!

HUYU NDIYE MWANAMKE WA KUOA

CHINYELE ACHUKUA FOMU KUOMBA RIDHAA YA KUGOMBEA UBUNGE DODOMA MJINI