Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ina mpango wa kujenga reli ya kisasa kutoka Mtwara-Mbambabay.
Rais Dkt. Samia ametoa ahadi hiyo, alipokuwa akihutubia katika mkutano wa Kampeni kwenye viwanja vya Polisi Mbambabay, wilayani Nyasa, Ruvuma Septemba 21, 2025.
Amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza nchi kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, Serikali itafikiria kujenga reli hiyo itakayorahisisha usafirishaji wa abiria, mazao na hasa madini ya chuma na makaa ya mawe kutoka Liganga na Mchuchuma.
Aidha, Rais Dkt. Samia ambaye katika mkutano huo aliungana na Mgombea Mwenza Balozi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameahidi kujenga Soko la Kimataifa la mazao mbalimbali na samaki kutoka ziwa Nyasa.
Ameahidi pia kujenga mtambo wa kukausha samaki wanaovuliwa katika Ziwa Nyasa ili kuwaongezea thamani.
Rais Dkt. Samia ambaye ameanza Kampeni Mkoani Ruvuma baada kufanikisha Kampeni Mkoa wa Kaskazini Pemba, leo amepita kuwasalimia na kuwaomba kura wananchi wa Wilaya ya Mbinga na hatimaye Mbambabay.
Kesho Jumatatu anatarajia kufanya mkutano mkubwa wa Kampeni mjini Songea na baadaye Namtumbo na Tunduru.
Comments