Na Richard Mwaikenda, Ruvuma
BAADA ya kufanya uzinduzi wa kampeni kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe Jijini Dar es Salaam, leo Mgombea wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia kwa kishindo mkoa wa Ruvuma Ikiwa ni Mkoa wa 13 baada ya kufanikisha kwa kiwango kikubwa kampeni katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Singida, Tabora, Kigoma, Mkoa wa Kusini Unguja, Mkoa wa Kaskazini Unguja na jana Mkoa wa Kusini Pemba.
Akiwa katika mikutano hiyo, Dkt. Samia anajinadi kwa kuelezea mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika mikoa hiyo, pia kutoa ahadi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Aidha, Dkt. Samia amekuwa akisisitiza kudumisha Muungano na kuendelea kulinda amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, ambapo pia amewatoa wananchi wasiwasi kwamba hakutokuwa na vurugu kwani vyombo vyote vya ulinzi viko imara, hivyo siku ya Uchaguzi Oktoba 29 mwaka huu amewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi tena bila hofu kwenda kupiga kura na kurejea salama majumbani.
Pamoja na kuelezea kwa undani Ilani ya uchaguzi ya chama hicho, Dkt. Samia ambaye mgombea wake mwenza ni Dkt. Emmauel Nchimbi, atatumia fursa hiyo kuwanadi wagombea ubunge na madiwani wa chama hicho.
SASA DKT. SAMIA ANAINGIA MKOA WA RUVUMA AKIWA NA HAZINA HII
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha shilingi bilioni 249.7 kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Ruvuma ikiwemo miradi ya elimu, afya, maji, barabara, umeme, kilimo, mifugo, utaliii na kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Mkoa wa Ruvuma ulikuwa na shule za msingi 818, na za sekondari 214, pamoja na vyuo vya ufundi (Veta) 3. Aidha kwa sasa mkoa huo una shule za msingi 841, za sekondari 233, na vyuo vya ufundi (Veta) 4.
Kwa upande wa huduma za afya, mkoa huo ulikuwa na hospitali za wilaya 3, vituo vya afya 15 na zahanati 100. Aidha kwa sasa mkoa una hospitali za wilaya 13, vituo vya afya 34, zahanati 301, pamoja na majengo ya EMD 4.
Mkoa huo ulikuwa na miradi ya maji 15, ambapo wananchi 120,000 walikuwa wanapata huduma ya maji safi na salama.
Kiwango cha upatikanaji maji mijini ilikuwa asilimia 50 na vijijini ilikuwa asilimia 57. Kwa sasa kuna jumla ya miradi 35 ya maji yenye jumla ya bilioni 51.2 inayoendelea kuhudumia zaidi ya wananchi 264,000 na vijiji 81. Kiwango cha upatikanaji maji mijini imefikia asilimia 80.95 na vijijini imefikia asilimia 68.
Mkoa una vijiji 551 kati ya hivyo vijiji 480 sawa na asilimia 87.1 vimefikiwa na umeme katika Miradi ya REA na Vijiji 71 vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA awamu ya 3 Mzunguko wa pili kwa gharama ya shilingi Bilioni 99.6.
Baada ya uhamasishaji uliofanyika kupitia “Royal Tour” na mpango Mkakati umeandaliwa ambapo maeneo ya vivutio yamefanyiwa maboresho kwa kupeleka wanyama katika kisiwa cha Lundo na kuletwa boti kwa ajili ya kuwapeleka watalii katika kisiwa cha Lundo na Mbambabay.
Vilevile mkoa huo, unatekeleza miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo, ujenzi wa barabara ya Mbinga- Mbambabay kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 66 kwa gharama ya shilingi bilioni 129.3, ujenzi wa barabara ya Amani Makoro - Ruanda (kilometa 35) kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 60.481.
Miradi mingine ni ukarabati na ujenzi wa Kiwanja Cha Ndege Songea kwa gharama ya shilingi bilioni 37.09 pamoja na ujenzi wa Bandari kubwa na ya kisasa ya Ndumbi katika ziwa Nyasa kwa gharama ya shilingi bilioni 12.2.
Comments