Rais wa Senegal atangaza likizo ya kitaifa kufuatia ubingwa wa Kombe la Afrika.
Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, ametangaza kuwa leo ni siku ya mapumziko ya kitaifa ili kuwapa wananchi wa Senegal fursa ya kutosha kusherehekea ushindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) walioupata usiku uliopita.
Kupitia taarifa rasmi, Rais Faye amesema uamuzi huo unalenga kuunga mkono furaha ya wananchi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa baada ya mafanikio makubwa ya timu ya taifa. Alisisitiza kuwa ushindi huo ni fahari kwa taifa zima na ni matokeo ya juhudi, nidhamu na mshikamano wa Wachezaji pamoja na sapoti ya wananchi.
Akizungumza kuhusu maamuzi hayo, Rais Faye alinukuliwa akisema, “Nimetangaza siku ya leo kuwa ni likizo ya kitaifa ili wananchi wa Senegal wapate muda wa kutosha kusherehekea ushindi wa Kombe la Afrika tulilolinyakua usiku uliopita.”
Tangazo hilo limepokelewa kwa shangwe kubwa nchini kote, ambapo wananchi wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi katika maeneo mbalimbali kushiriki shamrashamra za ushindi huo wa kihistoria. Serikali imewahimiza wananchi kusherehekea kwa amani na kuzingatia usalama, huku ikitambua mchango wa kila mmoja katika safari ya mafanikio ya taifa hilo kwenye soka la Afrika.
Toa maoni yako

Comments