Na Paul R.K Mashauri
Kwenye maisha onyesha msimamo wako toka mwanzoni. Binadamu ana tabia ya kukusoma mwanzoni hata awe mwanao wa kuzaa au mfanyakazi ofisini au waziri wako au dada wa nyumbani “house girl”. Ukikosea mwanzo, ukitaka kubadilika katikati unaonekana mkorofi au mbinafsi. Twende taratibu.
Mfano dunia nzima, wananchi wanaheshimu Polisi hata huyo Polisi awe mtoto mdogo. Kwanini? Kwa sababu Polisi anafundishwa kuweka msimamo toka mwanzo. Wanafundishwa hata jinsi ya kusimama kimsimamo. Ndio maana mtu yoyote akiingia Polisi anajua hapa siwezi kuleta utani. Kisa nini? Msimamo wa Polisi.
Kwahiyo katika malezi, mapenzi, uongozi, biashara n.k. onyesha msimamo toka mwanzo mtu ajue wewe ni nani. Unatuma SMS kila siku mistari 10 yeye anajibu kwa neno moja.. Hi! Tayari kuna shida kwenye mawasiliano. Ukikosa msimamo kwenye mawasiliano toka mwanzo, hata ukiolewa au kuoa akinuna miezi 12 au akikufyonza usishangae.
Mwaka 2010 tulimualika Mzee Felix Mosha kuongea na “professionals” pale Serena Hotel. Tulikuwa na CEOs na “Managers”. Akasema alipokuwa msaidizi wa Nyerere, kila mtu alikuwa anajua kwamba huwezi kwenda kumuambia Nyerere upuuzi. Kabla hujaenda kwa Nyerere ulikuwa unajiuliza maswali na kujijibu mwenyewe.
Achilia mbali uongozi. Hata katika ndoa. Lazima toka mwanzo ijulikane nani ameoa na nani ameolewa. Mtu ajue kwamba akienda “kucheat” abakie huko huko kama mateka wengine asirudi. Kwa sababu uki “cheat” maana yake umehama kambi. Hatujui umejiachia kiasi gani na umetoa siri gani na siri ngapi kwa huyo mkaka au mdada au mmama au mbaba aliyekuteka huko mlipokutana.
Ndio maana kuna msemo unasema ni bora kufa umesimama kuliko kuishi umepiga magoti. Wengi tunaishi tumepiga magoti sababu hatuna misimamo. Unakuta hata mtoto wako wa kuzaa anakufokea kama mtoto mdogo. Kwa sababu umemuacha akagundua kuwa unaheshimu mtoto mwenye hela. Na yeye hela anazo. Kwahiyo unatakiwa umsikilize yeye sio akusikilize wewe.
Ok angalia mafanikio ya Sir Alex Ferguson aliyeshinda vikombe 3 vya Champions League, Premier League na FA miaka ya 2000. Akina Beckham walikuwa wanajua hakuna mchezaji mkubwa zaidi ya “team”. Na kwamba kila mchezaji ni “replaceable”. Yule mzee alikuwa na misimamo na ndio siri ya mafanikio yake. Bora atafune “bigjii” kuliko kunyanyaswa na mchezaji.
Usipokuwa na msimamo toka mwanzo utapata shida sana na wanadamu. Kuna mwanadamu akigundua huna msimamo anakuwa “mpuuzi”. Atakuwekea hata vidole machoni. Lakini akijua mipaka yake, ataamua kula au kutema. Haiwezekani umelala usiku mtu anachunguza simu yako! Alishakusoma toka mwanzo. Kwanini asichunguze mchana? Kwa sababu unaficha simu.
Mtu mwenye msimamo hafichi chochote ni wewe kuamua kuishi nacho au kuondoka zako. Toka mwanzo mpe mtu uhuru anaoutaka lakini ajue kwamba akivuka mipaka imekula kwake. Angalia simu yangu lakini usithubutu kunivunjia heshima kwa utakachokikuta. Usipofanya hivyo siku akivizia simu yako akakuta ulimtumia hela mama yako huo ugomvi wake mpaka majirani watakuja.
Kimsingi suala la msimamo halikwepeki kama unataka kuwa “treated” kama mwanadamu sio mbwa. Nimekumbuka hata mbwa koko anadharaulika kwa sababu hana msimamo. Mdharau mbwa anayejitambua uone shughuli yake. Hata mbwa anafyata kwa paka mwenye msimamo. Hata tajiri anaheshimu masikini mwenye msimamo.
Ndio maana huwa nawashangaa sana watumishi wa Mungu wanaosema ukiwa masikini huna haki ya kuheshimiwa na mke au mume. Huwa najiuliza huo ni msimamo wa Mungu au mtumishi mwenyewe? Kwa sababu hata Mungu mwenyewe ana msimamo kiasi kwamba anajua watumishi wa hivyo ni manabii wa uongo.
Hata Serikali ina misimamo yake na ikikupa dhamana ukateleza, inasema “huo ni msimamo wake binafsi sio wa nchi.” Hata Rais wa Marekani aliwahi kuambiwa “huo ni msimamo wako binafsi sio wa Taifa la Marekani.” Kwa sababu hata Rais anaapa kulinda misimamo iliyo katika katiba.
Ndugu! Usipokuwa na msimamo toka mwanzo utaishi kama njiwa. Na sifa kubwa ya mtu mwenye msimamo ni hii; haogopi kuachwa au kuchukiwa au kupoteza “fear of rejection”. Msimamo na kutaka kumridhisha au kukubalika au kupendwa na kila mtu haviendi pamoja.
Ndio maana Mungu hapendwi na kila mtu. Ana misimamo yake na ameiweka wazi tuijue toka mwanzo. Mwanzo kabisa akaweka Amri Kumi. Hutaki tafuta muungu mwingine. Kama Mungu mwenyewe yuko tayari kwa lolote kwa mtu asiyeheshimu misimamo yake wewe una hekima sana kuliko yeye?
Usipokuwa na msimamo toka mwanzo unaonekana mkorofi na mbinafsi na huo ni ukweli mchungu “a painful reality”. Lakini angalia maisha ya wazee wetu wa zamani. Tuliwaita wanoko na wakoloni sababu ya misimamo yao lakini hatukuwaita wakorofi na wabinafsi kwa sababu toka unazaliwa mzee kanyooka hapindishi.
Lakini leo mzazi unakaa na mtoto kukubaliana aende shule au asiende ati akaimbe muziki! Kwani shule inakuziba mdomo usiimbe?

Comments