Mwaka 1994 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma watu wawili waliojulikana kwa majina ya Mbushuu Mnyaroje na Kalai Sungula walikutwa na hatia ya kosa la mauaji. Hawa watu wawili waliua mtu na kupora mifugo yake. Walikutwa na kosa la mauaji ya kukusudia (murder) kinyume na Kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Penal Code, Cap 16). Hivyo, walitakiwa kupewa hukumu ya kifo kwa mujibu wa Kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu yaani kunyongwa mpaka kufa kwa mujibu wa Kifungu cha 26. Kesi hii ilikuwa mbele ya Jaji James Mwalusanya.
Kabla Jaji Mwalusanya hajatoa hukumu hiyo ya kuwanyonga wawili hawa, wakili wa Mbushuu na Sungula Wakili Rweyongeza aliibua hoja kuhusiana na adhabu ya kifo kwamba hukumu ya kifo ni kinyume kabisa cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ibara 13(6)(d) na (e) kwa maana kwamba hukumu ya kifo ni ya kikatili, ya mateso yaani inayotweza utu wa mtu na isiyo ya kibinadamu. Wakili Rweyongeza alienda mbali zaidi na kusema hukumu ya kifo ni kinyume cha Katiba ibara ya 14 inayotoa haki ya kuishi. Kwa hoja hizo aliiomba mahakama isitoe hukumu ya kifo kwa wateja wake kwani hukumu hiyo ni siyo ya kikatiba (unconstitutional).
Mheshimiwa Jaji Mwalusanya (kama alivyokuwa) alikubaliana moja kwa moja na hoja za wakili Rweyongeza kwamba hukumu ya kifo ni adhabu ya mateso, kinyume cha utu na ubinadamu na ya kikatili. Jaji Mwalusanya alisema ukatili wa hukumu ya kifo unaonekana katika utekelezaji wa hukumu kwani si wa kistaarabu hata kidogo, unapingana na Katiba yetu na pia na Haki za Binadamu.
Katika kusisitiza ubaya wa hukumu ya kifo Jaji Mwalusanya akaandika kwenye hukumu yake maneno haya, ninayanukuu: ".......the process as slow, dirty, horrible, brutal, uncivilized and unspeakably barbaric"
Jaji Mwalusanya alisema hukumu ya kifo ni kinyume na ibara ya 14 ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayotoa haki ya kuishi kwa kila mtanzania. Sababu zingine ni ucheleweshwaji wa utekelezaji wa hukumu hiyo ya kifo na mazingira mabaya ambayo wafungwa wanaosubiri kunyongwa huhifadhiwa.
Jaji Mwalusanya baada ya kupinga vikali Kifungu cha Sheria cha Kanuni ya Adhabu ya Makosa ya Jinai (Penal Code) Kifungu cha 197 na kukitangaza kuwa kinapingana na Katiba yaani "Unconstitutional", aliwahukumu Mbushuu Mnyaroje na Kalai Sungula kifungo cha maisha jela kila mmoja badala ya hukumu ya kifo.
Jaji Mwalusanya alizaliwa tarehe 8/9/1943 huko mkoani Mbeya wilayani Rungwe na kufariki tarehe 1/10/2010 akiwa anaishi mkoani Dodoma ambako ndiko alikoweka makazi yake ya kudumu.
Kwa wanaopenda kusoma maswala ya kisheria watakubaliana nami kuwa huyu Mnyakyusa alikuwa maarufu sana katika utetezi wa maswala ya Haki za Binadamu, na hata hukumu zake nyingi zilijipambanua hivyo. Wakati wa uhai wake aliandika machapisho na vitabu vingi sana, baadhi yake ni pamoja na hivi vifuatavyo:
*Sheria ya Haki za Binadamu (1988)
*Upanuzi wa Demokrasia na Uimarishaji wa Haki za Binaadamu Katika Mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi Tanzania: Matumizi ya Katiba na Sheria Zilizopo ili Kudumisha Utulivu, Amani and Mshikamano (1993)
*Utaratibu wa Sheria wa Kutatua Migogoro ya Kazi: Pale Mfanyakazi Anaapoachishwa Kazi, Kufukuzwa Kazi, Kupunguzwa Kazi, Kupewa Likizo Isiyo na Muda Maalum na bila Malipo au Kustaafishwa kwa Manufaa ya Umma (1993)
*Sheria ya Mirathi: Maswali na Majibu Kuhusu Haki za Wajane (1993).
Je unataka kujua zaidi kuhusu historia ya Mnyakyusa huyu? Kama jibu ni ndiyo, basi endelea kuniombea ili mpango wangu wa kukiandika kitabu cha "WANYAKUSA MASHUHURI" ufanikiwe. Kwenye kitabu hicho utajua mengi kuhusu Wanyakyusa wengi waliopata kuwa mashuhuri kwenye mambo mbalimbali ya kielimu, kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kadhalika.
Ahsanteni sana, ndaga fijo!!
Lusako Mwang'onda
Kihesa TRM, Iringa.
26 Februari, 2026.

Comments