Jeshi la Polisi linapenda kujulisha Umma kuhusiana na taarifa za mtu anayefahamika kama Mchungaji Yanick Mbombo Cele ambaye kupitia mitandao ya kijamii kumesambaa taarifa zinazodai kuwa ametekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam.
Ifahamike kuwa mtu huyu raia wa Congo ambaye alishawahi kuwa mchungaji Kiongozi wa kanisa la Ebenezer Restoration Ministry for all Nations, alishawahi kukamatwa hapa nchini mkoani Iringa tarehe 15 Mei, 2025 kwa tuhuma za ubakaji na mauaji ya watoto wadogo yaliyokuwa yameshamiri kipindi hicho ambapo alikuwa akiwashawishi baadhi ya wafuasi wake kuwabaka watoto hao na kukinga damu zao kutoka sehemu za siri na kuwaua kisha wampelekee damu hizo kwa ajili ya kuzitumia kuwafanyia maombi.
Mbali na makosa hayo, mchungaji huyo pia alituhumiwa kujihusisha na vitendo vya utapeli na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kwa kuwalipa pesa baadhi ya waumini wake ambao walijifanya ni wagonjwa na wengine kujifanya ni walemavu ili wafike kanisani kwake kwa maombi na kujifanya kuwa wamepona huku wengine wakijifanya kupiga simu za ushuhuda wa kuponywa au kufanikiwa shida zao kupitia vyombo vya habari aliyokuwa akivitumia kutangaza kanisa lake mkoani Iringa.
Kutokana na kuripotiwa kwa matukio aliyokuwa akiyafanya, mwaka 2024 mchungaji huyo alitiwa kwenye kamati ya Usalama ya Mkoa wa Iringa na kupewa onyo kutokana na madai aliyokuwa akiyatowa kupitia kituo kimoja cha redio cha mjini Iringa ambacho kilikuwa kinalenga kuchochea chuki au uvunjifu wa amani kwa kuwa yalikuwa yanafanana na ramli chonganishi.
Ili kufahamu yaliyokuwa yakitendeka, timu ya upepelezi ilifanya uchunguzi wa kina na kutokana na ushahidi uliokusanywa ulifanikiwa kukamata watuhumiwa waliokuwa wakishirikiana na pamoja na vielelezo vilivyopatikana nyumbani kwake na kanisani kwake zikiwemo hirizi tano, pete tatu zenye picha za kutisha (magic face), magamba matano ya konokono, vitambaa vitatu vya rangi nyeupe vyenye matone ya damu, chupa mbili ndogo zenye mafuta yadhaniwayo kuwa ni ya nyama simba, na unga uliokuwepo kwenye chupa ndogo ya maji unaosadikika kuwa unatokana na gamba la kobe.
Tarehe 17 Juni, 2025 mchungaji huyo pamoja na wenzake watano walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kuendesha genge la uhalifu na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu, kesi namba ECO.00014959/2025, hata hivyo ushahidi dhidi ya mchungaji huyo kwa kesi ya mauaji na kubaka haukutosheleza hivyo hakuandaliwa mashitaka lakini wenzake walipelekwa mahakamani kuendelea na mashitaka hayo.
Tarehe 14 Julai, 2025 hukumu ilitolewa na mahakama ambapo watuhumiwa hao walitiwa kosa kwa njia ya plea bargaining na walihukumiwa kutenda kosa lolote la jinai kwa muda wa miezi kumi na miwili, kulipa faini kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiasi cha Tsh. 20,000,000/- pamoja na magari yao matatu kutaifishwa. Baada ya kulipa kiasi hicho cha pesa washitakiwa hao waliachiwa huru.
Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo kutolewa, ilibainika kuwa mchungaji huyo Yanick Mbombo Cele bado alikuwa akituhumiwa kuendelea kufanya udanganyifu kupitia kanisa lake la Ebenezer Restoration Ministry for all Nations na ufuatiliaji ulifanyika ambapo alikamatwa tena na kukiri kuendelea kutoa huduma katika kanisa hilo.
Baada ya kukamatwa, Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Iringa ilimkabidhi kwa Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Iringa ambapo mchungaji huyo aliondolewa nchini na kutakiwa asirudi tena.
Kutokana na hayo, Jeshi la Polisi limeshangaa kuona taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mchungaji huyo alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana. Hata hivyo, baada ya kuona taarifa hiyo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na linaomba kwa yeyote mwenye taarifa au ushahidi utakaoweza kuthibitisha taarifa hizo asisite kuwasilisha kwenye kituo chochote cha Polisi kilicho karibu naye.

Comments