Nchi ya Peru imejikuta tena kwenye msukosuko wa kisiasa baada ya rais aliyepo madarakani kuondolewa na bunge, akiwa amehudumu kwa miezi minne ya muhula wake.
Rais wa saba wa Peru katika muongo mmoja, José Jerí, alipigiwa kura na wengi kumuondoa madarakani kutokana na tuhuma za kufanya mikutano isiyojulikana na mfanyabiashara wa China na uteuzi usio wa kawaida wa wanawake kadhaa katika nyadhifa za kiserikali.
Jeri, mwenye umri wa miaka 39, alikuwa kiongozi mkuu wa Bunge Julai mwaka jana na alikuwa mrithi wa pili baada ya kuondolewa madarakani kwa Dina Boluarte.
Lakini kipindi chake cha uongozi kilighubikwa haraka na utata. Kilichojulikana zaidi kilikuwa kuhusu mikutano ya siri na mfanyabiashara wa China Zhihua Yang, ambaye anamiliki maduka, mkataba wa nishati na tayari alikuwa chini ya uangalizi wa serikali.
Jeri alirekodiwa akiwa amevaa fulana yenye kumfunika kichwa alipokuwa akikutana na Yang katika mgahawa wa Kichina, katika kashfa ambayo ilipata jina la "Chifagate," lililotokana na jina la migahawa ya Kichina.
Jeri aliomba radhi baada ya mkutano huo na kusema kwamba hakuna kosa lililofanyika. Licha ya hayo, hakuweza kupambana na shinikizo la kisiasa linaloongezeka huku uchaguzi ujao wa rais ukikaribia.

Comments