RAIS MSTAAFU DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE AWEKA SAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO CHA MAREHEMU KARDINALI PENGO

RAIS
Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete,
leo ameweka saini katika kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Askofu
Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam, marehemu
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu
jijini Dar es Salaam.
Baada
ya kuweka saini, Dkt Kikwete alimpa mkono wa pole Askofu Mkuu wa Jimbo
Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Thaddaeus S. Ruwa’ichi, na kueleza kuwa
marehemu Kardinali Pengo atakumbukwa daima kwa mchango wake mkubwa kwa
Kanisa na Taifa pamoja na moyo wake wa upendo kwa wananchi na kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema
Kardinali Pengo alikuwa rafiki wa wengi na kiongozi aliyegusa maisha ya
watu wengi kupitia huduma yake ya kiroho na kijamii.
Aidha,
Dkt Kikwete alitoa pole kwa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, viongozi na waumini
wa Kanisa Katoliki, akiwataka kuwa na subira katika kipindi hiki cha
majonzi huku akiungana nao kumuombea marehemu apumzike kwa amani.
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya kutoa pole, Rais huyo Mstaafu alisema
yeye na marehemu Kardinali Pengo walifahamiana kwa muda mrefu tangu
alipokuwa akihudumu wilayani Nachingwea katika kituo chake cha kwanza
cha kazi, wakati marehemu akiwa Askofu Mkuu aliyesimamia maeneo ya
Tunduru na Lindi.
Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Thaddaeus S. Ruwa’ichi,
alitangaza msiba huo tarehe 19 Februari 2026 saa 04:00 kwa masikitiko
makubwa, akieleza kuwa mpendwa baba yetu, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ameitwa
nyumbani kwa Baba wa Milele akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa ratiba rasmi ya mazishi, shughuli za kuaga mwili wa marehemu
zitaanza siku ya Jumamosi tarehe 28 Februari 2026 kwa kuwasili kwa mwili
katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu saa 03:00 asubuhi.
Kuanzia
saa 03:15 asubuhi hadi saa 10:00 jioni waombolezaji watapata fursa ya
kutoa heshima za mwisho katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.
Saa
10:00 jioni kutakuwa na Misa Takatifu ya kumuombea marehemu
itakayofuatiwa na mkesha wa sala na maombolezo utakaoshirikisha makundi
mbalimbali ya kijimbo, wakiwemo watawa, walei pamoja na vyama vya
kitume.
Siku
inayofuata, yaani Jumamosi, mwili wa marehemu utaondoka Kanisa Kuu la
Mtakatifu Yosefu saa 12:00 asubuhi kuelekea Kituo cha Hija Pugu, na
unatarajiwa kuwasili saa 12:45 asubuhi chini ya usimamizi wa Kamati ya
Mazishi.
Kuanzia saa 01:00 hadi saa 03:45 asubuhi waombolezaji watapata tena fursa ya kutoa heshima za mwisho katika Kituo cha Hija Pugu.
Misa ya Mazishi itaanza saa 04:00 asubuhi katika Kituo cha Hija Pugu, ikihitimisha rasmi shughuli za mazishi.
Waumini na wananchi wote wanaombwa kushiriki katika ibada na sala hizi kwa utulivu na heshima inayostahili.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 na kupadrishwa mwaka 1971.
Alisoma
Teolojia ya Maadili katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran mjini
Roma, ambako alipata shahada ya uzamivu mwaka 1977. Baadaye alifundisha
katika Seminari ya Kipalapala na kuwa Rektor wa kwanza wa Seminari ya
Segerea hadi mwaka 1983.
Aliteuliwa
kuwa Askofu wa Nachingwea mwaka 1983 na baadaye Askofu wa Jimbo la
Tunduru–Masasi mwaka 1985. Mwaka 1990 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu
Msaidizi wa Dar es Salaam na mwaka 1992 akawa Askofu Mkuu kamili wa
Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Mwaka
1998 alitangazwa kuwa Kardinali na Papa Yohane Paulo II, na alishiriki
katika mikutano ya kumchagua Papa mwaka 2005 na 2013.
Kardinali
Pengo alihudumu pia katika idara mbalimbali za Kanisa Katoliki la Roma
na kuongoza Baraza la Makanisa Katoliki Afrika (SECAM) tangu mwaka 2007.
Alistaafu mwaka 2019, akiacha alama ya uongozi thabiti na imani
isiyotetereka.

.jpeg)
Comments