Na Richard Mwaikenda, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali yake ya Awamu ya Sita imeandika historia nyingine kubwa kwa Taifa kwa kuzindua Makao Makuu ya kwanza ya Ulinzi wa Taifa (MMUT) mkoani Dodoma na kwamba hatua hiyo imekamilisha maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1964 wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilipoundwa.
"Leo tumeandika historia nyingine kubwa kwa Taifa letu
kwa kuzindua Makao Makuu ya kwanza ya Ulinzi wa Taifa eneo la Kikombo mkoani
Dodoma. Hatua hii imekamilisha maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Nyerere ya mwaka 1964 wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
lilipoundwa."
"Majengo haya ambayo tumeyajenga kwa fedha na wataalamu
wa ndani ni uthibitisho wa ukomavu wa Taifa letu katika kupanga, kuamua na
kutekeleza kwa ufanisi miradi mikubwa. Kuziweka pamoja ofisi za JWTZ na Wizara
ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kutaongeza tija na ufanisi wa kazi, na ni
kielelezo cha dhamira yetu ya kujenga taasisi imara za kulinda uhuru, mipaka,
rasilimali na watu wetu," amesema Rais Samia huku akishangiliwa.
"Mafanikio ya mipango tuliyojiwekea yanategemea sana
uwepo wa amani na utulivu. Hivyo, wito wangu kwetu sote ni kuendelea kuimarisha
ulinzi, usalama, umoja na mshikamano wa nchi yetu." Amesema Rais Samia.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa JKT ,Dkt
.Rhimo Nyansaho amesema ujenzi wa makao makuu hayo unaonesha dhamira ya
wazi ya serikali katika kuimarisha suala la ulinzi na usalama nchini.
Amesema jengo hilo la kisasa litaongeza ufanisi katika
uratibu wa shughuli za kiulinzi na kutoa mazingira bora ya utendaji kazi kwa
maafisa na askari.
“Uwepo wa makao makuu ya kudumu ni hatua muhimu katika
kujenga taasisi imara, zenye mifumo madhubuti ya kiutendaji na mawasiliano,
jambo litakalosaidia kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazoibuka katika
ulimwengu wa sasa.”amesema Dkt.Nyansaho.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkuu
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe amesema serikali
imeandika historia mpya kwa kuwa na makao makuu ya kudumu ya ulinzi wa taifa.
Amesema zaidi ya shilingi bilioni 121 zimetumika katika
kufanikisha ujenzi huo wa awamu ya kwanza ambao umetekelezwa na wataalamu wa
ndani ya jeshi hilo.
“Matumizi ya wataalamu wa ndani yamepunguza gharama na
kuongeza uzoefu kwa wanajeshi katika sekta ya ujenzi na usimamizi wa miradi
mikubwa ya kimkakati. ameongeza kuwa mradi huo umezingatia viwango vya kisasa
vya ubora na usalama.”amesema Dkt.Mnyepe.
Kwa upande wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania,
Jenerali Jacob John Mkunda amesema jengo hilo ni sehemu ya kurahisisha utendaji
kazi na kuchochea uimarikaji wa ulinzi na usalama wa taifa. amesema makao makuu
hayo yatawezesha upangaji na utekelezaji wa mikakati ya kiulinzi kufanyika kwa
haraka na ufanisi zaidi.
Aidha amewahimiza wanajeshi kuendelea kufanya kazi kwa
nidhamu, uadilifu na uzalendo, wakitambua kuwa jukumu lao ni kulinda uhuru,
umoja na mshikamano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taswira ya Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo Mkoani Dodoma mara baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 24 Februari, 2026.
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)




Comments