KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali,Bw. Gerson Msigwa,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utendaji wa serikali katika siku 100 za uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Februari 26, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali,Bw. Gerson Msigwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya siku 100 zilizopita.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 26, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Msigwa amesema mafanikio yaliyopatikana yanadhihirisha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uchumi kupitia sekta za uchukuzi, reli, bandari, usalama wa majini na utalii.
Amesema sekta ya uchukuzi imeendelea kuimarika huku mchango wake katika Pato la Taifa ukiongezeka kutoka asilimia 7.1 mwaka 2021 hadi asilimia 7.5 mwaka 2024.
UWEKEZAJI MKUBWA VIWANJA VYA NDEGE
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 na nusu ya 2025/26, Serikali imeendelea kuboresha na kupanua viwanja vya ndege mbalimbali nchini kwa thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.154.
Miradi hiyo inatekelezwa katika viwanja vya Arusha, Moshi, Mwanza, Serengeti, Kyabajwa (Kagera), Msalato, Shinyanga, Tabora, Kigoma na Sumbawanga.
Aidha, amesema kuwa mashine 13 za kisasa za ukaguzi wa abiria na mizigo zimefungwa katika viwanja mbalimbali, hatua iliyoruhusu utoaji wa huduma saa 24 na kuongeza usalama.
Kutokana na maboresho hayo, mashirika saba mapya ya ndege ya kimataifa yameanza safari nchini, yakiwemo Air France, Saudia, South African Airways, Airlink na Zambia Airways.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya abiria imeongezeka kutoka milioni 5.15 mwaka 2023/24 hadi milioni 5.25 mwaka 2024/25, huku mizigo ikiongezeka kwa asilimia 8.8.
ATCL YAONGEZA NDEGE NA MAPATO
Serikali imeendelea kuimarisha Air Tanzania Company Limited (ATCL) kwa kuongeza ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, na kufanya shirika hilo kuwa na jumla ya ndege 16.
Abiria wa ATCL wameongezeka kutoka 822,232 mwaka 2021/22 hadi 1,178,025 mwaka 2024/25. Mapato yamefikia dola milioni 157.69, sawa na ongezeko la asilimia 87.88 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Shirika hilo pia limeongeza ajira kwa Watanzania hadi kufikia watumishi 1,031.
SGR YAPUNGUZA MUDA WA SAFARI
Kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), Serikali inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma zimeanza, zikipunguza muda wa safari kutoka saa 10 hadi 12 kwa basi hadi saa 3 hadi 4 kwa treni.
Tangu kuanza kwa huduma hiyo, zaidi ya abiria milioni 4.6 wamesafirishwa na tani zaidi ya 52,000 za mizigo kusafirishwa. Aidha, ajira zaidi ya 200,000 zimetengenezwa moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Serikali pia imesaini mkataba wa kufufua reli ya TAZARA kwa kushirikiana na Zambia na kampuni ya CCECC ya China.
BANDARI NA USAFIRI MAJINI
Serikali imeanza maandalizi ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga magati 10 mapya na matenki 15 ya kuhifadhia mafuta.
Mapato ya forodha yameongezeka kutoka trilioni 7.082 hadi trilioni 8.256 katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025.
Katika maziwa makuu, meli mpya ya MV New Mwanza imeanza kutoa huduma katika Ziwa Victoria, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo.
UTALII WAONGEZEKA KWA KASI
Amesema kuwa Sekta ya utalii imeendelea kukua, huku jumla ya watalii (wa ndani na nje) ikiongezeka kutoka milioni 5.36 mwaka 2024 hadi milioni 5.9 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 10.2.
Mapato ya utalii yameongezeka kutoka dola bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi dola bilioni 3.9 mwaka 2024.
Miongoni mwa vivutio vinavyoendelea kuitangaza Tanzania kimataifa ni Serengeti National Park, Mount Kilimanjaro na Ngorongoro Conservation Area.
Tanzania pia imeendelea kushinda tuzo za kimataifa za World Travel Awards, zikiwemo World’s Leading Safari Destination na World’s Leading National Park.
Hata hivyo Msigwa amesema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita, akisisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ni msingi wa kukuza uchumi, ajira na ustawi wa wananchi.
.”

Comments