SERIKALI kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TBA), imepunguza ada za leseni za uendeshaji Blogu na Televisheni za mtandaoni (Online Tv) na ada za usajili za mitandao hiyo.
Punguzo hilo limetangazwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA'katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji (ABC) Februari 12, 2026 jijini Dodoma.
Naibu Waziri Mwinjuma amesema kuwa ada ya leseni ya 'Online TV' imepunguzwa kutoka sh. 1,000,000 hadi Sh. 100,000 kwa mwaka na fomu ya usajili imepungua kutoka 100,000 hadi sh. 20,000. Ada ya leseni ya blogu imepungua kutoka sh. 500,000 hadi sh. 50,000 kwa mwaka na fomu ya usajili imetoka sh. 50,000 hadi sh. 10,000.
Awali katika mkutano huo, Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Andrew Kisaka ya alitangaza nafuu ya kutolipa ada kwa mwaka mmoja kwa waandishi wa habari wanaoanzisha mitandao ya habari.
Mhandisi Kisaka alisema kuwa wametoa nafuu hiyo ili kuwapa muda waandishi wa habari wa kujifunza na kupata uzoefu wa uendeshaji wa mitandao.
Awali anayetaka kuanzisha mtandao wa habari alitakiwa alipe ada ya maombi sh. 50,000 na ada ya leseni sh. 500,000 kwa mwaka.
Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na wamiliki wa mitandao waliohudhuria mkutano huo ambao baada ya Naibu Waziri Mwinjuma kutangaza walishangilia kwa kupiga makofi.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wa siku mbili ni wanachama wa Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN), Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), MOAT, NIBA, Wakongwe RTD, Baraza la Habari Tanzania (MCT), MISA Tanzania na EACO.

Comments