Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuzuiwa kufanya shughuli zake za kisiasa umetokana na maamuzi ya Mahakama Kuu, na siyo uamuzi wa CCM wala Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Laban Kihongosi, Machi 19, 2025, Mzee Joseph Butiku alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kwa hali ya kutoielewa misingi ya kisheria, kuwa CHADEMA imefungiwa kufanya shughuli zake wakati chama hicho kikiendelea.
Taarifa hiyo ya leo Januari 21 imefafanua kuwa kuzuiwa kwa CHADEMA kulitokana na uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri la maombi madogo namba 8960 la mwaka 2025. Shauri hilo lilifunguliwa na wanachama watatu wa CHADEMA ambao ni Said Issa Mohammed, Ahmed Rashid Khamis na Maulidah Anna Komu, waliodai kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA ameshindwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa kuitisha vikao muhimu vya chama.
Mahakama iliamua kuzuia CHADEMA kuendelea na shughuli zake zote za kisiasa na matumizi ya mali za chama hicho hadi shauri la msingi namba 8323 la mwaka 2025 litakapofikishwa mahakamani na kuamuliwa.
CCM imesisitiza kuwa suala hilo ni la kisheria na linahusu chama cha CHADEMA pekee, hivyo si sahihi kwa CCM au Serikali kulaumiwa kwa uamuzi wa mahakama. Aidha, chama hicho kimewataka wananchi na wadau wa siasa kuheshimu utawala wa sheria na kuepuka kutoa kauli zinazoweza kuchochea chuki au kuvuruga amani na mshikamano wa taifa.

Comments