WIZARA YA ELIMU NA COSTECH KWA KUSHIRIKIANA NA BENKI YA CRDB WATENGA SHILINGI BILIONI 4.6 KUWAWEZESHA VIJANA WABUNIFU
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia TUME ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB imetenga jumla ya Shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya kuwawezesha mitaji vijana wabunifu waliofikia hatua ya kupeleka bidhaa na huduma zao sokoni.
Uwezeshaji huo unafanyika kupitia Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu uliozinduliwa mwaka 2024, ambao umetambua jumla ya wabunifu 3,300 nchini, ambapo kati yao 300 wameendelezwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) unaosimamiwa na COSTECH.
Akizungumza Februari 13, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwatambua wanufaika saba waliopata mikopo ya masharti nafuu kupitia mfuko huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir, amesema Serikali imeielekeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuhakikisha wabunifu, ambao wengi wao ni vijana, wanawezeshwa kukabiliana na ushindani wa soko.
Amesema uwekezaji huo unawalenga watanzania wenye bunifu zilizo tayari kuingia sokoni lakini wanakosa mitaji, akisisitiza kuwa mfuko huo uko wazi kwa wabunifu wote wenye bidhaa au huduma zilizo tayari kuwafikia walaji.
“Wizara ilitenga Sh. bilioni 2.3 kwa ajili ya kutoa mikopo nafuu kwa wabunifu, fedha ambazo ziliwekwa kwenye Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu. Kutokana na wingi wa wabunifu nchini, Serikali iliingia makubaliano na Benki ya CRDB ambayo nayo ilichangia shilingi bilioni 2.3, hivyo kufanya mtaji wa mfuko huo kufikia bilioni 4.6,” amesema.
Naibu Waziri Wanu amewapongeza baadhi ya wanufaika akiwemo kijana Paul Kitema ambaye amebuni teknolojia ya utambuzi wa thamani ya asali na mazao ya nyuki na kufanikiwa kusafirisha nje ya nchi zaidi ya tani 60 za asali na nta, hatua iliyomuingiza zaidi ya Sh. milioni 200 ya fedha za kigeni. Pia George Buchafwe kwa kuanzisha vituo viwili vya teknolojia ya kuchakata chikichi katika Halmashauri za Mlimba mkoani Morogoro na Kibiti mkoani Pwani.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo, ameeleza kusikitishwa na kasi ndogo ya uchukuaji wa mikopo akisema kuwa katika kipindi cha miezi 10, ni vijana saba pekee waliokuwa wamenufaika na mfuko huo huku kiasi cha Sh. milioni 767 tu kikiwa kimetumika kati ya bilioni 4.6 zilizotengwa.
Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa vijana wenye bunifu zinazoweza kuwa bidhaa au huduma kuwasilisha maombi yao kupitia COSTECH ili kunufaika na fedha zilizopo, ambazo zitasaidia kuanzisha biashara, kutoa ajira na kuchangia uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Uendelezaji Sayansi na Teknolojia, Dkt. Beatrice Lyimo, amesema jukumu la mfuko huo ni kukuza sayansi na teknolojia kwa kubadilisha mawazo bunifu kuwa suluhisho la changamoto za jamii kupitia uwezeshaji wa kifedha.
Amesema kwa kushirikiana na CRDB, COSTECH imeendelea kusaidia wabunifu kuendeleza bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko, kuimarisha misingi ya viwanda na biashara, pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wanufaika.
Mkurugenzi wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema vijana wengi wana mawazo bunifu na suluhisho mbalimbali lakini changamoto kubwa imekuwa upatikanaji wa mitaji ya kuyapeleka sokoni. Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mfuko huo akisema umeanzishwa kwa wakati sahihi kusaidia vijana kubadili mawazo yao kuwa biashara zinazozalisha ajira.
Amesema katika awamu ya kwanza, maombi 152 yalipokelewa, ambapo 22 yalitimiza vigezo kikamilifu na hatimaye wabunifu saba walichaguliwa na kupatiwa jumla ya Sh. milioni 667, kila mmoja akipata fedha kulingana na mahitaji ya mradi wake. Vijana 15 ambao hawakukidhi vigezo waliingizwa kwenye mpango wa kujengewa uwezo.
Miongoni mwa wanufaika, Paul Kitema mmiliki wa kampuni ya ufugaji nyuki, amesema alipata mkopo wa sh. milioni 135 uliomwezesha kununua vifaa vya kisasa, kuanzisha kliniki ya nyuki na kuongeza uzalishaji wa asali kwa ajili ya soko la nje, hali iliyosaidia pia kuajiri vijana wenzake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya COSTECH, Profesa John Kondoro, amesema pamoja na kuwepo kwa mashindano na fursa mbalimbali za ubunifu, Alisisitiza kuongeza hamasa kutasaidia kijana wengi kupata mikopo hoyo na kuwawezesha kujiajiri, kukuza uchumi na kuvutia wadau zaidi kufadhili mfuko huo.
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji ubunifu ulianzishwa kutokana na utafiti ulioonesha kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya bunifu, lakini wabunifu wengi hukwama kutokana na ukosefu wa mitaji na uelewa wa kibiashara.
Amesema hadi sasa bunifu 300 zimepita katika mfuko huo na zinaendelea kuunganishwa na wadau mbalimbali, kupatiwa ushauri na mitaji ili kuhakikisha zinakuwa endelevu.
















Comments