.WAHENGA walishasema maisha ni safari ndefu. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba viongozi wengi wanaolitumikia taifa hili katika nyadhifa kubwa na tofauti wamepita katika hatua nyingi za maisha tangu kuzaliwa kwao.
Miongoni mwa viongozi hao ni Profesa Mark Mwandosya ambaye 2005 alikuwa miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya Urais jijini Dodoma.
Baada ya hatua hiyo ya kuchukua fomu, Profesa Mwandosya alipaswa kutafuta wadhamini katika mikoa mitano, kabla hajairudisha fomu hiyo kwa ajili ya mchakato wa ndani ya chama.
Mchakato huo ulienda safi kwa upande wake alifanikiwa kupata wadhamini na akarudisha Fomu na kuiachia kamati kuu kupendekeza majina matano ambayo yatapelekwa kwenye halmashauri kuu ya CCM. Kikao hicho cha halmashauri kuu, kilipendekeza majina matatu na yeye alitokea kwenye Tatu bora hiyo sambamba na Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Majina matatu alivyopelekwa kwenye mkutano mkuu jina la Dr. Jakaya Kikwete lilupitishwa.
Mjue Mwandosya
Pamoja na kupanda vyombo vingi vya usafiri, ndege, magari, pikipiki na baiskeli, ukweli ni kwamba Profesa Mwandosya ametoka katika kijiji kimoja kilichoko ndani sana kutoka mji wa Tukuyu wilayani Rungwe.
Ni umbali wa karibu kilometa 50 kutoka Tukuyu mjini hadi Kitongoji cha Mpulo, Kijiji cha Kipapa katika Kata ya Lufilyo.
Mark ameishi maisha ya kijijini na kucheza michezo ya kitoto akiwa na vijana wa enzi zake ambao sasa ni wazee wa Kitongoji cha Mpulo au Kijiji cha Kipapa chenye vitongoji vitano ambavyo babu yake aliyekuwa akiitwa Lyagilaga alikuwa akivitawala akiwa Chifu.
Makao makuu ya Chifu Lyagalaga Mwandosya ambaye alikuwa babu wa Mark, yalikuwa kitongoji cha Mpulo ambapo panaelezwa kwamba maana ya neno Mpulo ni eneo refu la wazi lililokuwa katikati ya nyumba mithili ya barabara maalumu yenye nyumba pande zote mbili, huku miti mikubwa ikiwa katikati ya barabara na wananchi wakifagia eneo hilo kila asubuhi na jioni.
Kwa mujibu wa mzee Gosmo Mwakatwila (78) ambaye yuko jirani na nyumbani kwa wazazi wa Profesa Mwandosya Chifu Lyagilaga alizaa watoto kadhaa akiwamo Isack James Mwandosya ambaye alikuwa baba mzazi wa Profesa Mwandosya.
Mwakatwila anasema Isack alikuwa msomi na alifanya kazi za Mkuu wa Posta katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Mbeya, Chunya na Manyoni.
Anasema Isack alikuwa na kaka yake aliyeitwa Mwakang'ata Mwandosya ambaye pia alikuwa baba mkubwa wa Profesa Mwandosya.
"Nakumbuka Mark akiwa mdogo alikuwa akija kwa baba mkubwa na ndipo sisi tulipomfahamu, akiwa mpole sana na hakuwa mzungumzaji," anasema.
Baada ya kufariki Mwakang'ata mji huo alikabidhiwa Isack ambaye ni baba yake Profesa Mwandosya.
Mji wa ukoo wa Mwandosya
Mji huo kwa sasa una nyumba mbili za kisasa zilizojengwa kwa matofali ya kuchomwa katika kipindi cha uongozi wa Profesa Mwandosya. Nyumba hizo zina huduma za umeme na maji, kwa sasa zinakaliwa na wanafunzi sita wa sekondari ya Lufilyo.
Eneo la mji huo limezungukwa na msitu upande wa kusini lakini pande zingine wapo majirani ambao wanaishi.
Mita 400 ukitoka kwenye mji wa familia ya Mwandosya, kuelekea Magharibi, lipo kanisa dogo la Lutherani ambalo lina eneo la Lutherani ambalo lina eneo la makaburi, yakiwamo ya familia ya ukoo wa Mwandosya.
Miongoni mwa makaburi ya familia ya Mwandosya ni pamoja na baba mzazi wa Profesa Mwandosya Isack aliyezaliwa 1919 na kufariki 1993. Kaburi lingine ni la marehemu Segelile Ifunga, mama mzazi wa Profesa Mwandosya aliyezaliwa 1927 na kufariki 2009.
Mkazi wa Kitongoji hicho, Ambele Mwakajabo (36) anasema Profesa Mwandosya ndiye anayetoa kazi ya kusafisha eneo la makaburi yote kila anapofika kijijini hapo.
Lakini Mzee Mwamedi Mwang'onda (70) anasema Profesa Mwandosya anashiriki kazi nyingi za kijamii katika kijiji hicho. Anasema kwenye misiba
anakaa kwenye mashina ya migomba na wakati wa chakula anatumia kijiko cha asili ya Wanyakyusa maarufu kwa jina la 'indundu' ambacho kinatokana na kushona majani ya mgomba.
Asimulia alivyotaka kumpora senti moja
"Nakumbuka akiwa mdogo, alikuja likizo hapa na wakati tunacheza 'skabu' (mchezo wa kurusha kitu mbele na kukirudisha kwa mguu mmoja huku mwingine ukiwa umeukunja) alirusha senti moja ya zamani yenye tundu. Basi nikamsukuma ili kumpora ile fedha," anasema.
Mwang'onda anasema kwa upole wake Mark alianza kukimbia kwenda nyumbani kumweleza dada yake ambaye alifika kumsaidia mara moja.
Wengi hawajui alizaliwa wapi
Pamoja na kumsifia Profesa Mwandosya kwamba enzi za utoto alikuwa mpole, mwenye huruma na hekima, wazee wengi akiwamo dada yake, Christina Mwandosya (68) hawajui alipozaliwa.
Christina akiwa kwenye nyumba aliyoijenga baba yao anasema yeye hakumbuki ni wapi alizaliwa mdogo wake.
Anasema anakumbuka walisoma pamoja na mdogo wake huyo katika shule moja iliyoko Mbozi, halafu walihamia Shule ya Msingi Majengo ya jijini Mbeya na hatimaye wilayani Chunya.
"Mdogo wangu akiwa mdogo nakumbuka alikuwa akipenda sana kusoma na alikuwa akicheza mpira na wenzake. Pia alikuwa mpole sana na mwenye huruma,” anasema.
Mzee Mwang'onda wa Kitongoji cha Mpulo anasema Profesa Mwandosya alizaliwa nje ya kijiji chao, na baadaye alikuwa akiletwa wakati wa likizo na wazazi wake.
Taarifa za mitandao
Katika mitandao Profesa Mwandosya anatajwa kusoma katika Shule ya Msingi Majengo jijini Mbeya kuanzia 1957 hadi 1958 na baadaye alihamishiwa kwenye Shule ya White Father ya Chunya ambako alisoma kuanzia 1959 hadi 1960 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Chunya 1961 hadi 1964.
1965 alijiunga kwenye Sekondari ya Malangali hadi 1968 na kwamba mwaka 1969 alijiunga na Chuo cha Ufundi Dar es Salaam kabla ya kujiunga kwenye vyuo vya juu vya Aston na Birmingharm kwa Shahada ya Kwanza, Uzamili na Uzamivu katika Umeme na Vifaa vya kielektroniki.
Mwandosya alikuwa kiongozi wa vijana wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kati ya Mwaka 1967 na Mwaka 1968 na kuwa mwanachama rasmi wa TANU mwaka 1971, na kubakia mwanachama wakati TANU ilipoungana na Chama cha Afro Shiraz Party (ASP) kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 1977.
Alifundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuanzia Mwaka 1977 hadi Mwaka 1987, akianzia ngazi ya chini kama mhadhiri (1977-1980), kisha kama mhadhiri mwandamizi (1980-1983), na kama profesa 1983-1987 Kitivo cha Uhandisi.
Credit: Kanyamala Media

Comments