Kuna wakati Mtanzania unafika mahali halafu moyo wako unasimama kwa sekunde chache ukitafakari. Unajiuliza: “Hii kweli ni Tanzania yetu?” Ndivyo nilivyojisikia leo nilipofika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Nimelemewa hadi machozi yamenitoka. Yamenitoka si kwa sababu ya ugonjwa si kwa sababu ya huzuni, bali kwa sababu ya kuona picha halisi ya Tanzania inayowezekana. Tanzania ambayo watu wake tunaweza kuishi kwa heshima na upendo. Tanzania ambayo huduma zinaweza kumfanya mwananchi ajione ana thamani.
Kuanzia nje ya hospitali hii, unapokewa na mandhari yenye kuvutia. Maua yaliyopangwa kwa ustadi. Maegesho ya magari yaliyopangika. Bustani safi za kuvutia na miti inayosafisha hewa. Majengo meupe makubwa yanayong’aa kwa ustaarabu wa kisasa ni kivutio murua. Haya ni majengo yenye hadhi, uimara na taswira ya taifa ambalo wenye kulitakia mema wangetaka liwe zuri.
Ndani ya hospitalu hii kuna utulivu wa ajabu. Hakuna vurugu. Hakuna makelele yasiyo na mpangilio. Wagonjwa wanaitwa kwa namba kwa utaratibu unaompa kila mmoja heshima yake. Sehemu za kukaa ni nzuri na za kisasa. Wahudumu wanazungumza kwa upole. Nimepokewa na kuelekezwa kwa daktari wa moyo. Ni binti mwema. Yeye na mwenzake wa mapokezi wamenifanya nihisi ugonjwa ulionileta hapa umetoweka!
Wafanyakazi wengi wana bashasha kwenye nyuso, na bila shaka mioyoni. Madaktari na wauguzi wanampokea mgonjwa kama binadamu mwenye thamani, si mzigo.
Vyoo vipo vya kutosha. Visafi. Vinatumia maji ya kuflashi. Hili linaweza kuonekana jambo dogo kwa wengine, lakini kwa wengi usafi wa vyoo ni kipimo cha ustaarabu.
Mghahawa wake nao ni wa kiwango kinachostahili kuitwa mghahawa wa hospitali ya taifa. Siyo yale mabanda ya nje yenye mazingira yasiyo na hadhi ambayo mara nyingi huonekana katika baadhi ya hospitali nyingine. Hapa unaona kuwa mgonjwa na ndugu yake wanastahili mazingira bora hata wanapokula. Hapa watu wa hadhi zote wanashiriki chakula.
Kila mahali kuna televisheni. Vibao vya matangazo na maelekezo vimeenea kwa mpangilio unaorahisisha huduma. Maabara zina teknolojia ya kisasa kiasi kwamba majibu yanaweza kupokewa kwenye simu ya mgonjwa au ndugu yake. Rekodi zote za mgonjwa zinawekwa kidijitali kwenye mfumo maalumu. Hii ndiyo Tanzania ambayo wapenda nchi wote wanatamani kuiona.
Nilipotazama haya yote, swali moja lilinigonga moyoni: “Kama tunaweza kufanya hivi hapa, kwa nini isiwe kote nchini?”
Hapo ndipo moyo wangu unapouma na machozi kuanza kunitoka.
Tatizo letu mara nyingi si ukosefu wa uwezo. Tatizo ni kasoro zetu wenyewe kama taifa. Tukiondoa uzembe, ufisadi, wizi wa mali za umma, ubabe wa baadhi ya vyombo vya dola, ukosefu wa haki, na tabia ya kutokujali mambo ya msingi ya wananchi — Tanzania inaweza kuwa moja ya nchi bora kabisa barani Afrika.
Tuna ardhi nzuri. Tuna watu wazuri. Tuna amani iliyotikiswa. Tuna rasilimali. Tuna watu wenye akili na uzalendo. Kinachotukwamisha mara nyingi ni sisi wenyewe ndiyo maana mara zote nimeamini matatizo au mafanikio yetu ni mazao tunayosiha, kuyapalilia na kuyavuna sisi wenyewe.
Ni kwa sababu kama hizo, Hospitali ya Benjamin Mkapa inapaswa kuwa somo la taifa. Inapaswa kutukumbusha kwamba maendeleo yanawezekana. Kwamba fedha za umma zikitumika vizuri, matokeo yanaonekana. Kwamba taasisi zikiendeshwa kwa nidhamu, wananchi watapata huduma nzuri..
Tukitofautiana kisiasa, tutofautiane kwa hoja na ustaarabu. Tuache mambo mabovu kama haya mawazo ya kufuta vyama vya siasa. Tuache kuwa taifa linaloota uchaguzi tu kila leo. Tuifanye Tanzania iwe nchi ya demokrasia ya kweli ili Watanzania wote washiriki kufurahia matunda ya uhuru na kodi zao.
Tusibomoe taifa letu kwa chuki, tamaa, au vita vya maslahi binafsi kwa kundi fulani pekee. Nchi hii si yetu peke yetu. Ni urithi wa watoto na wajukuu wetu.
Watoto wa kesho wanapaswa kurithi Tanzania yenye hospitali bora, shule bora, barabara bora, haki bora na maisha yenye utu na haki.
Ninapotoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, naondoka na jambo moja moyoni: Tanzania yetu ni nzuri, kinachohitajika ni kuipenda kwa vitendo.
Manyerere J.N
Dodoma
Mei 16, 2026


Comments