Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki (COSOTA), Doreen Sinare akizungumza na waandishi wa habari, kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO, Dodoma, kuhusu mafanikio na mwelekeo wa ofisi hiyo ndani ya miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
TAARIFA
YA MAFANIKIO YA MIAKA MINNE YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA YA MHESHIMIWA DKT.
SAMIA SULUHU HASSAN RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA
HAKIMILIKI TANZANIA (COSOTA)
Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali
ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imefanikiwa
kwa kiasi kikubwa na yamefanyika mambo mengi yaliyosaidia kuimarisha usimamizi
wa hakimiliki nchini.
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipolihutubia Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza baada ya kuingia madarakani aliahidi
kuimarisha usimamizi wa hakimiliki na kuhakikisha Wasanii wananufaika zaidi na
kazi zao pamoja na kupata mirabaha na ametekeleza.
Kati ya mambo
yaliyofanyika ni pamoja na marekebisho katika Sheria ya Hakimiliki na
Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999 yaliyofanyika mwaka 2022 na 2023 kupitia Sheria
za Fedha za mwaka 2022 na 2023.
Mabadiliko
haya makubwa yalianzisha chanzo kipya cha mapato cha tozo ya hakimiliki
(copyright levy), ambapo vifaa vinavyotumika kusambaza, kuzalisha na kuhifadhi
kazi za sanaa na fasihi hutozwa asilimia moja nukta tano (1.5%) kila vinapoingia, kuzalishwa au kuundwa hapa nchini. Fedha
hizo hukusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Lengo
kuu la kuanzishwa kwa tozo hiyo ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi wadau wa sanaa
na uandishi nchini wakiwemo wasanii, waandishi na wabunifu ambao kwa muda mrefu
kazi zao zimekuwa zikitumika katika mazingira mbali mbali ya kijamii kama vile
kuhifadhi, kubebea na kusambaza kazi sanaa na uandishi na kuwanufaisha wadau
wengine pamoja na watu binafsi bila ya wenye kazi kupata haki zao.
Marekebisho hayo ya Sheria yaliweza kuweka
asilimia 1.5 kwa baadhi ya orodha ya vifaa yaani Radio/TV set enabling recording, analogue audio recorders, analogue
video recorders, CD/DVD copier, digital jukebox, MP 3 player, CD, DVD, Vinyl,
Mini Disc na SD Memory ili kuweza kulipishwa tozo hiyo ambapo ni vifaa 13
kati ya vifaa 25 vilivyoombwa.
Kupitia Kanuni ya Tozo ya Hakimiliki “The Copyright and Neighbouring Rights
(copyright Levy on blank devices) Regulations, 2023 GN No.378 published on
2/6/2023 (English) na GN No.385 published on 2/6/2023” mapato hayo yalianza
kukusanywa.
Kupitia chanzo hiki, COSOTA imekusanya
jumla ya Tshs. 1,428,105,241.44 kuanzia
Septemba, 2023 hadi Februari, 2025 ambapo Ofisi imefanikiwa kupokea fedha za
tozo ya hakimiliki za mwaka wa fedha 2023/2024 kutoka Wizara ya Fedha kiasi cha
Tshs. 847,985,594.26.
Aidha, Ofisi imeona kuwa vifaa
vilivyowekwa kwenye Sheria havitoshi kwani vingi vimepitwa na wakati na
havitumiki sana kama ilivyo kwa baadhi ya vifaa vilivyoachwa, hivyo kuna haja
ya kuongeza baadhi ya vifaa hasa simu, Computers,
External drives, printers, scanner, tablets, photocopier, printing plates na
flash disks ili kuhakikisha kuwa malengo ya kuwepo kifungu hiki yanafikiwa
lakini pia itaongeza mapato kwa Serikali na kwa wabunifu nchini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na
Hakishiriki pamoja na Mabadiliko Sheria ya Fedha Na. 5 ya mwaka 2022, kiasi cha
tozo ya Hakimiliki kilichokusanywa ndani ya mwaka husika hugawanywa kwa makundi
manne katika asilimia kama ifuatavyo: COSOTA 20%, Mfuko wa Utamaduni 10%, Mfuko
Mkuu wa Serikali 10%, na Kampuni za kukusanya na kugawa mirabaha (CMOs) kwa
ajili ya wasanii, waandishi na wamiliki wengine wa hakimiliki 60%.
Mgawanyo wa
Makusanyo ya Tozo ya Hakimiliki kwa Mwaka 2023/24 na 2024/25
Na |
Mwaka |
Jumla
ya Makusanyo |
COSOTA
(Asilimia 20) |
Mfuko
Mkuu wa Serikali (Asilimia 10) |
Mfuko
wa Utamaduni (Asilimia 10) |
CMOs
(Asilimia 60) |
1. |
2023/2024 |
847,985,594.26 |
169,597,118.85 |
84,798,559.43 |
84,798,559.43 |
508,791,356.56 |
2. |
2024/2025 (Julai – Februari,
2025) |
580,119,647.18 |
116,023,929.44 |
58,011,964.72 |
58,011,964.72 |
348,071,788.31 |
|
JUMLA |
1,428,105,241.44 |
285,621,048.29 |
142,810,524.14 |
142,810,524.14 |
856,863,144.86 |
Aidha,
Ofisi imeandaa mgao wa mapato haya kama mirabaha kutokana na fedha za tozo ya
hakimiliki utakaofanyika hivi karibuni. Mgao huu unategemewa kunufaisha makundi
ya kazi za muziki, filamu, maandishi, sanaa za ufundi na sanaa za maonesho –
Kila daraja litapata kiwango sawa na madaraja mengine.
Kiasi
cha Tsh. 508,791,356.56 kitagawiwa kwa wasanii ambacho ni asilimia sitini (60%)
ya tozo ya hakimiliki, na kiasi cha Tsh. 84,798,559.43 (asilimia 10) kinaenda
Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ambapo fedha hizo pia ni kwa ajili ya wasanii.
Hivyo wasanii na waandishi watanufaika na jumla ya kiasi cha Tsh. 593,589,915.98
zilizokusanywa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024. Gawio la Serikali ni
142,810,524.14 na gharama ya uendeshaji COSOTA ni 285,621,048.29.
Pia
mabadiliko hayo ya Sheria yamepelekea muundo wa COSOTA kubadilika na kuruhusu
uanzishwaji wa Makampuni ya Wasanii ya kukusanya na kugawa mirabaha (Collective
Management Organization - CMO) na COSOTA kubaki kama msimamizi wa masuala ya
hakimiliki na kusimamia Kampuni hizo.
Marekebisho
ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 2022 yalipelekea kuandaliwa kwa
Kanuni ya Kuanzishwa kwa Makampuni ya kukusanya na kugawa Mirabaha na kuruhusu
uanzishwaji wa Makampuni kwa ajili ya
kusimamia haki mbalimbali za aina za kazi za Sanaa na Uandishi - Kanuni za
Hakimiliki na Hakishiriki (Kampuni za Ukusanyaji na Ugawaji Mirabaha), kupitia tangazo
la Serikali Na. 215 la tarehe 24 Machi, 2023 na Copyright and Neighbouring
Rights (Royalty Collection and
Distribution Collective Management Organisations), Government Notice No. 211
published on 24/3/2023).
Katika
kuimarisha dhana ya kuhakikisha wasanii na waandishi wananufaika zaidi na kazi
zao, baada ya mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2022, COSOTA ilitoa leseni ya
kukusanya na kugawa mirabaha ya daraja la muziki kwa Kampuni ya Tanzania Music Rights Society (TAMRISO)
mnamo mwezi Julai 2023. Na Kampuni hiyo ilianza ukusanyaji wa fedha za mirabaha
mnamo mwezi Januari 2024 mpaka 16 Novemba, 2024 kwa mujibu wa vigezo vya leseni
hiyo.
Kwa
kipindi hicho TAMRISO ilikusanya kiasi cha Tshs. 256,448,440.00 kupitia baa, hoteli, kumbi za starehe, kumbi za
sherehe, migahawa, maduka ya biashara nk. Katika makusanyo hayo asilimia sabini
(70%) baada ya malipo ya kodi ya serikali (18% VAT) sawa na Tshs. 147,201,405
ndiyo zitagawiwa kwa wasanii wa muziki na asilimia thelathini (30%) baada ya
malipo ya kodi ya serikali (18% VAT) ni kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za
kiutawala TAMRISO.
Aidha,
hatua mbalimbali zinafanyika kupitia COSOTA, wasanii, waandishi na wadau
wengine ili kuanzishwa kwa Kampuni nyingine kwa aina nyingine za kazi kama vile
filamu, muziki, Sanaa za ufundi, Sanaa za maonesho na uandishi.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, usajili wa kazi zinazolindwa na Sheria
ya hakimiliki na hakishiriki umeongezeka kwa asilimia
70 Ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo
kuanzia mwaka 2021 mpaka Februari 2025, COSOTA, imesajili kazi za Sanaa na
uandishi 11,519 na Wabunifu 3,436. Idadi hii ya wabunifu pamoja na
kazi zao imetokana na zoezi la utoaji wa elimu na mafunzo mbalimbali ya
hakimiliki na usajili kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina
lakini pia kushiriki matukio mbalimbali ya wadau ambapo COSOTA ilipata fursa ya
kuelimisha wadau kuhusiana na hakimiliki na uhamasishaji wa usajili wa kazi za
hakimiliki.
Halikadhalika, katika kipindi hicho kamati
maalumu ya Usajili ndani ya COSOTA inayojihusisha na masuala ya usajili,
imefanikiwa kutoa mafunzo na ufafanuzi kuhusiana na hakimiliki kwenye kazi
zilizopokelewa katika kipindi hicho kwa idadi ya wabunifu 167.
Vilevile,
katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu sita COSOTA imetoa jumla ya
vyeti 7,679 vya uthibitisho wa
umiliki wa hakimiliki kwa wabunifu waliosajili kazi zao.
Kwa
mwaka 2021 - 2025 COSOTA imefanikiwa kufanya migao miwili kama alivyoahidi Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alipolihutubia
bunge mwaka 2021 ambapo alisisitiza katika kipindi cha uongozi wake, serikali itahakikisha
wabunifu wote wananufaika zaidi na kazi zao. Mgao wa kwanza ambao ulikuwa ni
mgao wa ishirini na tatu ulifanyika tarehe 28/01/2022
na ulikuwa wa kiasi cha Tshs. Tshs.
312,290,259,000, ambapo Wasani 1,123
walinufaika, na ulitokana na matumizi ya kazi 5,924 za muziki ambazo zilitumika katika vituo 11 vya redio, ikiwemo redio katika ngazi ya kitaifa, Mkoa, wilaya, kijamii
na za kidini.
Mgao
wa pili katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita ulifanyika tarehe
21/07/2023 na ulikuwa ni mgao wa ishirini na nne wa mirabaha kwa kazi za muziki
na COSOTA iligawa kiasi cha Tshs. 396,947,743.20
na wasanii wa muziki 8,165 walinufaika
kupitia kazi zao 61,490.
Hivi
ni viwango vikubwa zaidi kuwahi kufanyika katika migao ya mirabaha ambayo
COSOTA imekuwa ikigawa kwa miaka ya nyuma kabla ya uongozi huu wa serikali ya
awamu ya sita ambao ulianzisha kampeni ya kusisitiza watumiaji wa kazi za Sanaa
katika maeneo ya biashara kulipia matumizi ya kazi hizo.
Pamoja
na hayo uongozi wa Dkt. Samia umefanya mageuzi
makubwa ya kibajeti kwa COSOTA kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa
majukumu ya Ofisi kwa kutoa fedha za serikali kiasi cha Tshs. 1.5 bilioni. Fedha hizo zimesaidia kuboresha
usimamizi wa hakimiliki nchini, ununuzi wa vitendea kazi na utoaji elimu ya
hakimiliki pamojana ujenzi wa mfumo wa usajili.
Halikadhalika,
katika kuhakikisha tasnia ya hakimiliki nchini inaimarika serikali ya awamu ya
Sita kupitia uongozi wa Dkt. Samia COSOTA imepata ufadhili wa mradi wa Mpango wa Kuwezesha Mazingira ya Biashara
(MKUMBI) unaosimamiwa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji unaofadhiliwa
na Umoja wa Ulaya wenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara. Mradi hii
umewezesha COSOTA kupata ufadhili kwa ajili ya kutoa elimu ya uharamia na
hakimiliki kwa kazi za ubunifu, kuboresha mfumo wa COSOTA na kunganisha mifumo
ya COSOTA, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) ili iweze
kusomana pamoja na kuandaa Kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Hakimiliki na
Hakishiriki, zinazohusu usajili wa kazi zinazolindwa na Sheria ya Hakimiliki, zinazohusu
Watu wenye uoni hafifu na wasioona kuweza kupata machapisho na zinazohusu haki
ya Kunufaika na Mauzo Endelevu (resale rights).
Fauka
ya hayo, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julai 2022 iliundwa Kamati
maalum ya Kuratibu Ukusanyaji wa maoni ya namna bora ya kusimamia hakimiliki
nchini iliyokuwa na wadau mbalimbali wakiwepo wasanii na waandishi iliyoongozwa
na Mwenyekiti Bw. Victor Tesha pamoja na Mheshimiwa Hamis Mwinjuma (Mb) Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (kabla hajateuliwa katika nafasi
ya Waziri) ilifanya kazi ya kukusanya maoni ya wadau wa hakimiliki katika Kanda
tano nchini. Taarifa ya Kamati hiyo ilionesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu,
kusimamia masuala ya uharamia, kubadili muundo wa COSOTA na kuongeza idadi ya
watumishi pamoja na kusimamia kukamilika kwa mchakato wa kuanzishwa kwa Kampuni
za kukusanya na kugawa mirabaha ambazo husimamiwa na wasanii wabunifu wenyewe
na COSOTA kubaki msimamizi wa Kampuni hizo. Taarifa hiyo imefanyiwa kazi
utekelezaji wake na kupelekea nabadiliko mbalimbali katika tasnia ya
hakimiliki.
Kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu
ya sita COSOTA imefanikiwa kupokea jumla
ya migogoro 136 na kusuluhisha
migogoro 118. Migogoro 10 kati ya hiyo haikumalizika na
ilifunguliwa kesi mahakamani na migogoro 8 inaendelea COSOTA. Sambamba na
migogoro hii, COSOTA imehusika na kesi za hakimiliki 10.
Pia katika kipindi hicho maandiko ya Itifaki
za Kimataifa yaani Itifaki ya Kampala yaani
Kampala Protocol on Voluntary Registration of Copyright and Related Rights 2021,
Itifaki ya Beijing yaani Beijing Treaty on Audivisial Perfomances
na Maandiko ya Mikataba ya Internet yaani Internet Reaties ya WIPO Copyright
Treaty (WCT) ya mwaka 1996 na WIPO Performances and Phonograms Treaty (WPPT) ya
mwaka 1996 iliandaliwa na kikao cha kuwakutanisha wadau wa Sanaa katika
madaraja mbalimbali na kuwaelimisha wadau kuhusu Itifaki hiyo na faida ambazo
zinapatikana baada ya Tanzania kuiridhia imefanyika na sasa ushirikishaji
unaendelea ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaridhia mikataba hii mapema
iwezekanavyo ili kuboresha mazingira ya ulinzi na biashara ya kazi za
hakimiliki.
Katika
kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya Sita Ofisi ilifanikiwa kuendesha Semina ya
kujengeana uwezo kuhusu masuala ya hakimiliki na Sheria ya Hakimiliki na
Hakishiriki kwa makundi mbalimbali wakiwepo mahakama, bunge, wahariri, vyuo
vikuu, mashirikisho na vyama vywa waandishi na wasanii na mawakili wasio wa
serikali.
Hata
hivyo katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita kupitia uwezeshwaji wa
kibajeti Ofisi imefanikiwa kutoa elimu ya hakimiliki kuhusu mikataba, usajili
wa kazi, uhamasishaji wa ulipaji wa mirabaha, kupambana na uharamia kwa kuandaa
semina, kushiriki maonyesho mbalimbali, vipindi vya redio na televisheni na midahalo.
Elimu hiyo imetolewa kwa Mikoa ya Mbeya, Mwanza, Morogoro, Dodoma, Mtwara,
Arusha, Dar es Salaam, Pwani, Tanga, na Ruvuma. pia Ofisi ilifanikiwa kutoa matangazo ya kukemea uharamia,
kuhamasisha ulipaji wa mirabaha na kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu na
kusambaza taarifa mbalimbali kwa umma.
Halikadhalika,
katika kipindi hicho kumekuwa na kuimarika kwa mahusiano na mashirika ya
kimataifa yaliyochangia kupelekea utaratibu mahususi kuanza wa kuanzishwa kwa
Kituo cha kutoa Elimu ya Hakimiliki cha Intellectual Property Training
Institution (IPTI). Kituo hicho kitaanzishwa kwa ufadhili wa Shirika la Miliki
Bunifu Duniani (WIPO) kwa usimamizi wa taasisi zinazosimamia masuala ya
hakimiliki (copyright) na Miliki Bunifu za Viwanda (Industrial Property) kwa
Tanzania. Hii imetekelezwa kwa pamoja na kusainiwa kwa makubaliano ya pamoja baina
ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni (BRELA), Ofisi ya Hakimiliki Zanzibar (COSOZA) na Wakala wa Usajili
Biashara na Mali Zanzibar (BPRA). Kituo hicho kitakuwa kikitoa mafunzo ya miliki
ubunifu ya muda mfupi kutokana na mahitaji ya makundi mbalimbali.
Sambamba na hili, kupitia mashirikiano na
uridhiwaji wa Itifaki ya Marakesh yaani Marrakesh
Treaty to Facilitate Access to Published Works for Persons Who Are Blind,
Visually Impaired or Otherwise Print Disabled, Tanzania kupitia Taasisi ya
Chama cha Wasiiona Tanzania (Tanzania League of the Blind -TLB) imenufaika kwa
kupata vifaa vya VEVO 10 Daisy na
mafunzo ya matumizi ya vifaa hivyo kutoka Shirika la Miliki Ubunifu Duniani la
WIPO kwa Shule sita na Chuo kimoja cha wenye uoni hafifu na wasioona kama
ifuatavyo Tanga - Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Dar es Salaam - Shule
ya Uhuru Mchanganyiko, Shule ya
Sekondari Lugalo, Shule ya Msingi Toangoma, Ruvuma - Shule ya Msingi Ruhila, Tabora
- Shule ya Msingi Furaha, na Chuo cha Ufundi Mtwara kwa ajili ya kuwawezesha
kurekodi wakati walimu wanafundisha na kuweka masomo katika mfumo unaowawezesha
kusoma.
Pamoja na mafanikio hayo, mnamo Januari
2025 COSOTA ilisaini makubaliano na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
ili kulipia leseni kutokana na matumizi ya kazi za muziki kwenye viwanja vya
ndege ili wasanii wa muziki wanufaike na matumizi ya kazi zao.
Pia kwa kuzingatia
ulinzi wa kazi za ubunifu katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita COSOTA
ilifanya Operesheni mbalimbali za
kupambana na Uharamia katika mitandao na katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera,
Dodoma, Tabora, Shinyanga, Songwe, Mwanza, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro,
Lindi, Mtwara, Manyara na Mara Ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Hakimiliki na
Hakishiriki ya mwaka 1999, kanuni ya uzalishaji na usambazaji ya Mwaka 2006 na
kanuni ya Ufifilishaji wa makosa ya Hakimiliki ya mwaka 2020.
Katika kipindi cha serikali ya
awamu ya sita Muziki wa singeli ambao ni wa kipekee kutoka Tanzania umekuwa kwa
kasi na kupendwa naidi nchini na kuvuka mipaka ya nchi. Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano alieleza namna alishuhudia wazungu
wakifurahia Muziki huo. Katika kipindi hiki, COSOTA imetoa elimu kwa Wasanii,
watayarishaji, wafanyabiasha na wadau wa Singeli kwa kushirikiana na Taasisi
isiyo ya kiserikali ya Uswazi Got Talent na Kandoro Baba Entertainment chini ya
Meneja Kandoro na Kituo cha cha redio na televisheni kupitia Efm kikiendeshwa
na Samio Love kuwaeleza umuhimu wa usajili wa kazi zao na faida za kusajili
ambapo takribani wasanii 20 wa Muziki wa Singeli wamesajili kazi zao COSOTA.
Pia wamenufaika na mgao wa mirabaha kwa mwaka 2022 na mwaka 2023 na nimategemeo
yetu kuwa watanufaika Zaidi kutokana na kupendwa na kushiriki katika biashara
ya muziki wa singeli ndani nan je ya nchi.
Ni matarajio ya COSOTA kuwa
mafanikio haya ni chachu ya ukuaji wa biashara ya tasnia ya hakimiliki sasa na
miaka ijayo ambapo yataongeza kipato kwa wasanii, waandishi na wabunifu wenye
hakimiliki na kutengeneza ajira zaidi sambamba na kuongeza pato la taifa. Kazi
iendelee!
****ASANTENI KWA KUNISIKILIZA*****
Comments