Baraza limesajili jumla ya miradi 8,058, ambapo kati ya hiyo, 5,784 ni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na 2,274 ni ya Ukaguzi wa Mazingira.
Vikao 3,836 vya wataalam vilifanyika kwa ajili ya kufanya mapitio ya taarifa za TAM na Ukaguzi wa Miradi na kutoa mapendekezo ya maboresho ya masuala ya msingi ya kuzingatiwa katika taarifa hizo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Immaculate Semesi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 24, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Aidha amesema kuwa Miradi 4,570 iliidhinishwa na kupewa vyeti vya mazingira. Kati ya hivyo, 3,058 ni vya TAM, 765 ni vya Ukaguzi, huku vyeti vingine vikiwemo vya kubadili masharti 169, vyeti vilivyohamishwa umiliki 552, vyeti vya muda (PEC) 53 na cheti kilichorudishwa (certificate of surrender) 1.
"Katika kuboresha utoaji wa huduma za vibali vya TAM, Baraza lilianzisha mfumo wa kielectroniki unaotumika kusajili hadi kuidhinishwa kwa miradi ya TAM ambao umeongeza ufanisi. Kabla ya mfumo Baraza lilikuwa linasajili takribani miradi 900 kwa mwaka na baada ya mfumo Baraza linasajili zaidi ya miradi 2,000 kwa mwaka, haya ni mageuzi makubwa ya Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
....Katika kipindi cha mwaka 2020/21- 2024/25, Baraza limefanikiwa kusajili wataalam Elekezi wa Mazingira 1,023 na kutoa vyeti vya utendaji kwa Wataalam Elekezi 503 baada ya kukidhi vigezo kwa mujibu wa Kanuni za Usajili na utendaji wa Wataalam Elekezi wa Mazingira za mwaka 2021. Kanuni hizi mpya zimeongeza ufanisi kwa kuruhusu usajili kufanyika wakati wowote. Usajili wa Wataalam Elekezi wa Mazingira unafanyika kupitia mfumo wa kielektroniki ambao umeongeza ufanisi wa kushughulikia maombi," amefafanua Semesi.
Comments