Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewahimiza Watanzania kutumia fursa ya maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane 2025) ili kujifunza mbinu mbalimbali za uzalishaji wa mazao kwa maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujumla.
Waziri Chana amesema hayo leo tarehe 4 Agosti, 2025 kwenye viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa kutembelea kwenye maonesho hayo itasaidia Watanzania katika kupata elimu ya uzalishaji wa mazao na kujifunza utalii wa vyakula.
“Naomba nitoe rai kwa Watanzania tutembelee maeneo haya ya maonesho kuna bidhaa nzuri, kuna utafiti, kuna elimu, kuna mbegu, vivutio vya kila aina na pia unapokuja katika maonesho haya unapata elimu unapata elimu ya aina mbalimbali” alisema Waziri Chana.
Aidha, Waziri Chana ameahidi kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao ili kuongeza mapato kwa taifa na wananchi na pia kuunga mkono Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayoendelea kufanya kazi nzuri kwa watanzania.
“Tunapozalisha bidhaa tunaongeza thamani tutapata na mapato lakini tunataka watalii waje kuona utajiri wa Tanzania wa vyakula mbalimbali na ndiyo maana leo tumekuwa na mabanda mahali hapa kuonesha bidhaa zetu za Wizara ya Maliasili na Utalii, tunataka waje kuona utalii wa vyakula, kama ni chai yote hiyo ni aina ya utalii” alisema Waziri Chana.
Comments