Na Mwandishi wetu, Shinyanga
BENKI ya NMB imezindua tawi maalum la NMB Tinde Mnadani mkoani Shinyanga ikiwa ni sehemu ya kuzingatia dhamira yake ya muda mrefu ya kusambaza huduma za kifedha kwa jamii ambazo hazijafikiwa.
Uzinduzi huu umeambatana pamoja na uzinduzi wa matawi mengine maalum ya Itobo(Nzega, Tabora), Iboregero(Igunga, Tabora), Mkongeni(Mvomero, Morogoro) na Dosidosi(Kiteto, Manyara)
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi hilo ,Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi ameeleza kuwa Benki hiyo inatambua nafasi muhimu ya minada ya mifugo katika uchumi wa vijijini na uwepo wake katika mnada wa Tinde unaashiria utoaji wa huduma za kifedha na dhamira ya Benki ya NMB kusogeza huduma hizi kwa kila mtanzania huku wakiziwezesha jamii ambazo kihistoria zimekuwa zikikabiliwa na vikwazo vya kufikiwa na huduma za kifedha.
Amesema eneo hilo la kimkakati la Tawi hili jipya maalum linalenga kuleta mapinduzi katika hali ya kifedha ya wafanyabiashara na wafugaji kwa kutoa huduma salama, rahisi na zenye ufanisi huku zikirahisisha na kuboresha shuguli zao kwa maslahi makubwa ya uchumi wa binafsi na wa mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.
"Kwa kuanzisha tawi hili maalum ndani ya mnada wa Tinde, tunatatua changamoto za moja kwa moja za matumizi makubwa ya pesa taslimu kwa kituo hiki kitatoa huduma kamili, zikiwemo kuweka pesa na kutoa pesa, kufanya miamala mbalimbali, programu za elimu ya kifedha hususani zeney mlengo wa ufugaji na mkopo maalum iliyoundwa kuongeza tija ya mifugo na biashara kwa ujumla, " Mponzi alisema.
Ameongeza kuwa, kabla ya hapo washiriki wa minada ya mifugo, wanunuzi na wafanyabiashara walilazimika kubeba pesa taslimu ili kuweza kufanya manunuzi au baada ya mauziano ya bidhaa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, Dk Kalekwa Kasanga
"Uwekezaji huu wa Benki ya NMB utakuwa na faida kubwa kwa jamii yetu. Kwa kutoa njia salama na rahisi za kusimamia fedha, kupitia tawi hili maalum, uchumi wa Tinde utazidi kuimarika na watu wengi watanufaika zaidi na huduma hizi za kifedha na hivyo tutatengeza fursa za ajira na kuboresha hali ya jumla ya maisha kwa wakazi wetu." Dk.Kasanga alisema.
"Kwa upatikanaji wa mikopo na fursa ya kuweka akiba, wafugaji wataweza kuwekeza katika mifugo iliyoboreshwa, lishe bora na mbinu za kisasa za ufugaji, na hivyo kusababisha tija kubwa na kuongeza kipato. Hii pia itachochea mahitaji ya bidhaa na huduma nyingine, na kujenga mzunguko mzuri wa ukuaji wa uchumi," aliongeza.
Naye mfanyabiashara na mfugaji kutoka Tinde, Gerald Mwandu ameishukuru benki ya NMB kwa kujenga kituo hicho katika kata ya Tinde. Amewaomba wafugaji, wakulima na Wafanyabiashara kutumia huduma za benki mbalimbali za benki ya NMB
Comments