Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 19 anaunguruma kwenye viwanja vya Kuzuite Sumbawanga mkoani Rukwa.
Ameingia Mkoa huo jana kwa kuanza kampeni wilayani Nkasi, akitokea Mkoa wa Katavi alikofanya mkutano mkubwa kwenye Uwanja wa Azimio Mjini Mpanda na baadaye, Kibaoni ,Mpimbwe.
Baada ya kufanya uzinduzi wa kampeni kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe ijini Dar es Salaam Agosti 28, 2025, leo Oktoba 19, 2025 Dkt. Samia ameingia mkoa huo wa Rukwa ukiwa ni Mkoa wa 27 siku ya 53lp baada ya kufanikisha kwa kiwango kikubwa kampeni katika mikoa mingine 26.
Tanzania Bara ni; Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Singida, Tabora, Kigoma, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Arusha, Manyara, Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera na Katavi.
Tanzania Visiwani; Mkoa wa Kusini Unguja, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkoa wa Kusini Pemba.
Bado mikoa ya; Dar es Salaam, Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kaskazini Pemba
Akiwa katika mikutano hiyo, Dkt. Samia hujinadi kwa kuelezea mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika mikoa hiyo, pia hutoa ahadi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa miaka mingine mitano endapo atashinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29.
Aidha, Dkt. Samia amekuwa akisisitiza kudumisha Muungano na kuendelea kulinda amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Pia amewatoa wananchi wasiwasi kwamba hakutokuwa na vurugu kwani vyombo vyote vya ulinzi na usalama viko imara, hivyo siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu wajitokeze kwa wingi tena bila hofu kwenda kupiga kura na kurejea salama majumbani.
Pamoja na kuelezea kwa undani Ilani ya uchaguzi ya chama hicho, Dkt. Samia ambaye mgombea wake mwenza ni Dkt. Emmauel Nchimbi, hutumia fursa hiyo kujinadi yeye, wagombea ubunge na madiwani wa chama hicho.
IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA - 0754264203
Comments