Sehemu ya Kanuni mpya ligi kuu za NBC zitakazotumika msimu huu.
KANUNI MPYA LIGI KUU YA NBC
Kanuni : 31. KUTOFIKA UWANJANI
(1) Timu yoyote itakayokosa kufika uwanjani bila ya sababu za msingi
zinazokubalika kwa TPLB na/au kusababisha mchezo usifanyike itakabiliwa na adhabu zifuatazo:
1.1 Itapoteza mchezo huo na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu (3) na magoli matatu (3).
1.2 Kutozwa faini isiyopungua shilingi milioni hamsini (50,000,000/-) ambapo 50% ya faini itachukuliwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania na 50% italipwa kwa timu pinzani.
1.3 Kulipa fidia ya maandalizi/uharibifu wowote unaoweza kujitokeza.
1.4 Kupokwa alama 3 (tatu) katika msimamo wa Ligi na Mwenyekiti au Rais wa Klabu kufungiwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka mmoja (1) hadi mitano (5).
1.4.1 Endapo timu itakuwa na alama pungufu ya tatu (3), itakuwa na alama hasi kwa kiasi kinachopungua kwenye msimamo
wa Ligi.
1.4.2 Endapo timu itamaliza msimu wa Ligi ikiwa na alama hasi, itaanza na alama hizo hasi katika msimamo wa Ligi kwenye msimu unaofuata wa Ligi ya hadhi yake.
1.5 Kwa michezo ya hatua ya mtoano, timu iliyokosa kufika uwanjani katika mchezo wa mkondo mmoja, itakuwa imepoteza hadhi ya kuingia hatua inayofuata bila kujali matokeo ya mchezo wa mkondo mwingine.
1.6 Itapoteza haki ya kuchukua gawio lake la mapato ya mchezo huo.
1.7 Kiongozi mwingine yeyote atakayebainika kuwa alishiriki,
alishawishi au alikuwa chanzo au sababu ya timu kutotokea
uwanjani bila ya sababu za msingi atafungiwa kwa kipindi cha miezi kumi na miwili (12).
1.8 Inaweza kukabiliwa na adhabu zaidi kama ambavyo TFF/TPLB itahitaji kuchukua hatua zaidi kadiri itavyoona inafaa.
1.9 Timu ya Ligi Kuu itakayoshindwa kufika kituoni katika michezo mitatu (3) ya Ligi bila sababu za msingi zinazokubalika na TFF/TPLB
itakuwa imejiondoa kushiriki Ligi hiyo.
1.10 Timu yoyote iliyopewa adhabu ya faini chini ya kanuni 31:1(1.1, 1.2
na 1.3) haitaruhusiwa kucheza hadi itakapotekeleza adhabu hiyo kwa daraja ambalo itakuwa ipo.
Comments